NI BAJETI YA TRILIONI 31.7

0
571

NA KULWA MZEE-DODOMA


SURA ya Bajeti ya mwaka 2017/2018 inaonyesha kuwa jumla ya Sh trilioni 31.7 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho.

Hayo ya yalisemwa jana bungeni wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2017/2018.

“Jumla ya mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 19.9 sawa na asilimia 63 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni  17.1 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani,” alisema.

Alisema mapato yasiyo ya kodi ni Sh trilioni 2.1 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh bilioni 687.3.

Waziri Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.9 ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote.

 “Misaada na mikopo hii inajumuisha miradi ya maendeleo Sh trilioni 2.47 mifuko ya pamoja ya kisekta Sh bilioni 556.1 na misaada ya kibajeti (GBS) Sh bilioni 941.2. Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 7.7 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara,” alisema.

Alisema mikopo ya ndani inatarajiwa kuwa Sh trilioni 6.16, ambapo Sh trilioni 4.9 ni kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zinazoiva na trilioni 1.2 sawa na asilimia moja ya pato la taifa ni mikopo mipya kwa kugharamia miradi ya maendeleo.

 “Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 1.59 kutoka soko la nje. Katika mwaka 2017/18, Serikali itaongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na mikopo ya ndani na nje ili kutekeleza miradi ya maendeleo.

 “Miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo awamu zinazofuata za ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge na uboreshaji wa bandari mbalimbali nchini, vitatekelezwa kulingana na mpangokazi kutegemea mwenendo wa mapato ya ndani na nje, utakaojidhihirisha baada ya kufanya mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2017,” alisema.

Waziri Mpango alisema mara baada ya ridhaa ya Serikali kupatikana, utaratibu wa kutoa hatifungani maalumu utatekelezwa ili kusaidia kupunguza madeni yaliyohakikiwa ya Serikali kwa mifuko ya hifadhi ya jamii.

 “Katika mwaka huo wa fedha, Serikali inapanga kutumia jumla ya Sh trilioni 31.712. Kati ya fedha hizo, Sh trilioni 19.7 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, ikijumuisha Sh trilioni 7.2 za mishahara na Sh trilioni 9.46 kwa kulipia deni la umma na huduma nyinginezo,” alisema.

Alisema matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 11.9 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote, ambapo Sh trilioni 8.9 ni fedha za ndani na Sh trilioni 3 ni fedha za nje.

 “Kiwango hiki kimezingatia wigo wa asilimia 30 hadi asilimia 40 ya bajeti yote iliyoidhinishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here