Na Asifiwe George, Dar es Salaam
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umezindua kituo cha huduma kwa ajili ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanachama wao kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi wa NHIF, Michael Mhando alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kupunguza kero kwa wanachama wao.
Alisema huduma hiyo itapatikana bure kwa kupiga namba 0800110063 na kuuliza maswali au msaada wa haraka kuhusu kadi ya matibabu au huduma katika kituo cha matibabu, dawa na vipimo.
Alisema mfumo huo, una uwezo wa kuhudumia wateja 10 kwa wakati mmoja na uwezo wa kutoa majibu moja kwa moja kwa mlengwa.
Pia wametoa mafunzo kwa watoa huduma wa maduka ya dawa yaliyosajiliwa na NHIF namna ya kuwasilisha madai yao kwa kutumia mfumo wa kielektroniki.
Alisema mafunzo hayo, yametolewa na wahudumu wa maduka ya dawa ya Wilaya ya Kinondoni na Temeke.
Alisema lengo la kuanzisha mfumo huo ni kuondoa udanganyifu na ulaghai unaofanyika kwa baadhi ya watoa huduma ambao si waaminifu.
“Mfumo huo utaanza rasmi Januari Mosi mwakani na utasaidia kujua viashiria vinavyoelekea kugushi au kufanya udanganyifu katika huduma zilizotolewa,” alisema.