28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NHIF yaja na mapinduzi sekta ya afya

Na Mwandishi Wetu

MAFANIKIO kwenye Sekta ya Afya kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, yametokana na ushirikiano kati ya Wizara na Taasisi zake ili kuhakikisha huduma bora za matibabu zinawafikia wananchi.

Hatua ya kwanza iliyofanywa na Serikali ni kuhakikisha inakabiliana na tatizo la ukosefu wa dawa hospitalini kwa kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 69 hadi Sh bilioni 270 kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Ongezeko hilo la karibu mara nne limeimarisha na kuongeza upatikanaji wa dawa kwa asilimia 90 katika vituo vya kutolea huduma za matibabu.

Juhudi hizi za Serikali zimesaidia kwa kiwango kikubwa uimarishaji wa huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na kuondoa changamoto za kihuduma kwa wanachama wanapokwenda kutibiwa.

Ili kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu kwa gharama nafuu, Serikali kupitia mfuko huo imeanza mchakato wa uwekezaji wa kiwanda kitakachozalisha bidhaa mbalimbali za hospitalini zinazotokana na pamba.

Uwekezaji wa kiwanda hiki unafanyika katika Mkoa wa Simiyu ambapo mchakato wake tayari umeanza na kwa sasa uko katika hatua za utekelezaji lengo likiwa ni kuhakikisha kiwanda hiki kinaanza rasmi uzalishaji wa bidhaa za tiba ifikapo mwaka 2020.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, NHIF, unashirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pamoja na Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu ambayo imetoa ardhi itakayotumika kujenga kiwanda hicho. Mchakato wa usajili wa kiwanda hicho kinakachojulikana kwa jina la Simiyu Medical Products Company Limited, tayari umeshakamilika.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, anasema: “Mradi huo unatekelezwa kwa kushirikisha taasisi mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na Serikali ya Mkoa wa Simiyu, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Tanzania Engineering & Manufacturing Design Organization (Temdo), Benki ya Rasilimali (TIB) na Shirika la Utafiti na Mendeleo ya Viwanda la Taifa (TIRDO).”

Konga anasema kuwa upembuzi wa awali umefanyika na ujenzi wa kiwanda utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 29 ambapo asilimia 90 ya fedha hizo zitatolewa na NHIF pamoja na WCF kama wamiliki wa kiwanda hicho, wakati asilimia 10 iliyobaki itatolewa na Benki ya TIB kama mkopo kwa Kampuni kwa ajili ya kuwezesha gharama za uendeshaji wa kiwanda baada ya ujenzi kukamilika.

“Eneo ambalo kiwanda hicho kitajengwa lina ukubwa wa mita za mraba 72,800 katika mji wa Dutwa eneo la viwanda la Isenge katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi na kwa kuanzia kiwanda kitazalisha aina 24 ya bidhaa za hospitali zitokanazo na pamba,” anasema Konga.

Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Ibara ya 50, dhamira yake ni kuwa na wananchi wenye afya bora watakaoweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Ilani inasisitiza kuweka utaratibu utakaowezesha wananchi kuwa na Bima ya Afya ili kumudu gharama za matibabu.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, Mfuko umefanikiwa kufikia makundi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 18, kupitia huduma ya Toto Afya Kadi pamoja na wakulima kupitia huduma mpya ya Ushirika Afya, ambayo imezinduliwa mwezi Julai, mwaka huu na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Mbali na Toto Afya Kadi na Ushirika Afya, Mfuko umeendelea kuhudumia makundi mengine yakiwemo ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Mfuko pia umefanikiwa kusajili watumishi wa mashirika mbalimbali ya umma ambayo yalikuwa bado hayajajiunga na huduma za mfuko.

Mfuko kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani, umepanua wigo wa mradi wa akinamama wajawazito na watoto, ujulikanao kama Tumaini la Mama, unaotekelezwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Songwe na Mbeya.

Hadi kufikia Agosti mwaka huu mradi huo umeweza kunufaisha akina mama 1,044,000 katika mikoa hiyo.

Mafanikio mengine makubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia mfuko huo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kitaalamu ndani ya nchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za wananchi kwenda nje ya nchi kufuata huduma hizo.

Hospitali mbalimbali nchini zimewezeshwa kuwa na vifaa tiba vya kisasa zaidi vilivyowezesha upasuaji mkubwa wa moyo na upandikizaji wa figo kufanyika hapa nchini.

Akizungumzia suala hili, Mkurugenzi Mkuu Konga, anataja hospitali kubwa ambazo zimenufaika na uwekezaji huo kuwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (MOI), ambazo mbali na vifaa, MOI imenufaika na ujenzi wa majengo pacha ambayo yamesaidia kupunguza changamoto ya msongamano wa wagonjwa.

Hospitali nyingine ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Hospitali ya Rufaa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles