28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

NHIF yafunguka gharama vifurushi bima ya afya

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umevunja ukimya na kuzungumzia malalamiko mengi yanayotolewa na watu mbalimbali kuhusu gharama za vifurushi vipya vya matibabu.

Umesema kabla ya kufikia uamuzi wa kutangaza vifurushi vipya vya bima ya afya, ulifanya utafiti wa gharama ambazo Watanzania wanaweza kuzimudu kabla ya kuutangazia umma.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benernad Konga alisema kabla ya uamuzi huo walifanya utafiti wa wiki tatu kwa Mkoa wa Dar es Salaam uliolenga kuwafikia watu wengi zaidi, lakini wakajikuta wanavuka lengo walilokusudia.

“Tulianza kwa kufanya utafiti wetu ili kupata maoni ya msingi ya wananchi, katika eneo hili tulikusudia kuwafikia watu 100 hadi 200, nawaambieni wahariri tulipata watu 700, hii ni idadi kubwa ambayo ilitupatia mwelekeo mzuri wa malengo yetu.

“Kila mtu alitoa mawazo au kuchagua kifurushi chake ambacho anaona atakimudu kukigharamia, tukajikuta mfuko umepata Sh milioni 400, hili si jambo dogo, Watanzania wengi wana mwamko.

“Napenda kusisitiza jambo hili tumelifanyia utafiti na kulipeleka kwenye mamlaka husika ndugu zangu, hapo tulipo nasema tumechelewa sana, tusonge mbele, tuache blablaa.

“Tumekuja na vifurushi vya Najali Afya kinaanzia Sh 192,000, Wekeza Afya na Timiza Afya ambavyo vimewekewa mchanganuo mzuri na wa kueleweka,” alisema Konga.

Alisema utafiti ulifanyika wilaya za Kinondoni, Temeke na Ilala hata kabla ya kuomba kibali kutoka serikalini kuwatangazia Watanzania.

“Tulijikita kwenye utafiti wetu hata kabla ya kuomba kibali cha Serikali, baada ya kuona mambo yamekwenda vizuri, ndiyo tukaruhusiwa kutangaza,” alisema Konga.

Alisema idadi ya Watanzania wanaohudumiwa na mfuko ni asilimia 8.5 idadi ambayo ni ndogo, huku ikiacha kundi kubwa nje.

“Watanzania wengi hawako kwenye mfuko huu, ndiyo maana tumekuja na mkakati wa kuhakikisha tunatoa vifurushi ambavyo kila mwananchi anaweza kuvimudu ili mwisho wa siku apate matibabu. Si jambo jema kuhangaikia bima wakati mtu unaumwa,” alisema Konga.

Alisema Serikali ina mpango wa kupeleka muswada bungeni ili mwisho wa siku uwe sheria ambayo itamlazimisha kila Mtanzania kujiunga na NHIF tofauti na ilivyo sasa.

Kuhusu taarifa za mfuko huo kuwa na hali mbaya kiuchumi, Konga alisema hakuna ukweli wowote wa jambo hilo na kwamba wako imara.

“Mfuko uko imara, kila baada ya miaka mitatu tunafanya ukaguzi, hakuna hata kituo kimoja tulishindwa kukilipa, tumefanya mwaka 2016 mpaka sasa tuko vizuri.

“Hata kama wanachama hawatalipa, tutakwenda mpaka mwaka 2024 bila kugusa ‘asset’ hata moja. Katika hili, nawatoa hofu kabisa ndugu zangu,” alisema Konga.

Aidha Konga alitoa wito kwa Watanzania kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyokuwa ya lazima.

Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama wa mfuko huo, Christopher Mapunda alisema gharama za matibabu zimekuwa za ghali na kama mwananchi wa kawaida asipokata bima, hukumbana na usumbufu mkubwa.

Alisema matibabu ya saratani kwa mtu mmoja kwa mwaka yamefikia Sh milioni 69.9, matibabu ya figo Sh milioni 35 na upasuaji moyo ni Sh milioni 12.

“Ukiangalia gharama hizi ni kubwa kwa mwananchi wa kawaida kuzimudu bila kuwa na bima yake, lazima tufike wakati sasa tubadilike.

“Mnaweza kuchangishana au kuuza nyumba na bado msifikie gharama za kulipia saratani, mwisho wa siku mgonjwa anafariki,” alisema Mapunda.

Wiki iliyopita mfuko ulitangaza gharama za vifurushi vipya vua bima ya afya ambavyo gharama zake zinaanzia Sh 192,000 hadi Sh milioni 2.2 kwa familia moja.

VIFURUSHI VIPYA

Kwa mujibu wa NHIF, virushi vipya kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35, mtu binafsi ni Sh 192,000 (Najali Afya), Sh 384,000 (Wekeza Afya) na Sh 516,000 (Timiza Afya).

Kwa umri wa miaka 39 hadi 59, kwa kifurushi cha mtu binafsi ni Sh 240,000 (Najali Afya), Sh 440,000 (Wekeza Afya) nah 612,000 (Timiza Afya).

Umri wa miaka 60 na kuendelea, kwa mtu binafsi ni Sh 336,000 (Najali Afya), Sh 660,000 (Wekeza Afya) na Sh 984,000 (Timiza Afya).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles