28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

NHC kuhakiki wapangaji mlango kwa mlango

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha linafanya uhakiki wa nyumba zote linazozimiliki ili kubaini wapangaji halali na wasio halali.

Lukuvi ameagiza uhakiki huo ufanyike nyumba kwa nyumba, mlango kwa mlango ili kubaini udanganyifu unaofanywa na wapangaji, ikiwamo majengo yenye maduka katika miji mikubwa.

Pia ameagiza uhakiki wa nyumba zilizotaifishwa na kukabidhiwa kwa Msajili wa Majumba ambazo baadaye zilirejeshwa kwa wahusika kwa minajili ya ‘huruma’, kuwa waishi hadi watakapofariki dunia, huku nyumba hizo zikiendelea kuwa mali ya Serikali.

Lukuvi pia ameagiza kupitiwa upya kwa miradi 192 ya ubia baina ya NHC na watu binafsi, akiitaka Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti kuangalia namna ya kuboresha mikataba, ili shirika hilo linufaike na miradi hiyo.

Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Lukuvi alisema amechukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa kumekuwa na udanganyifu miongoni mwa wapangaji wa nyumba hizo na wale waliowahi kupewa nyumba zilizokuwa zimetaifishwa, hivyo wanahitaji kuchukua hatua kudhibiti hali hiyo.

Alisema wizara yake imeona ni vyema uongozi wa NHC uanze uhakiki wa wapangaji wake kwa njia ya kielektroniki baada ya kubaini kuwa taarifa za wapangaji wengi hazipo kutokana na matumizi ya mfumo wa kizamani wa karatasi.

“Pitieni upya mikataba yenu na wapangaji. Kuna watu wameanzisha vishirika ndani ya shirika. Wanauza nyumba na kupokea wapangaji wapya. Kuna watu wanaopangisha nyumba, lakini wenyewe hawapo, waliopo ni wengine kabisa, kwa hiyo tunahitaji uhakiki huu ufanyike.

“Tena katika uhakiki huu, muanzishe mfumo wa kielektroniki ambao utahusisha moja kwa moja taarifa zao na zile za vitambulisho vya taifa vya Nida, kila mpangaji anapoingia kwenye nyumba ajulikane alikotokea na hata anakofanya kazi,” alisema Lukuvi.

Alisema katika uhakiki huo, wapangaji wote walioingia NHC kama wapangaji waliotozwa fedha zisizokuwa halali wajitokeze kwa kufika ofisini kwake na kuwasiliana naye, naye atahakikisha wanarudishiwa fedha zao zote.

 “Ninawahakikishia, yeyote aliyetozwa fedha kwa ajili ya kupata nyumba NHC kinyume na utaratibu, akija kwangu na vielelezo, nitahakikisha anarudishiwa fedha zake zote. Hata kama ikiwa ni Sh milioni 40, ninajua zitakapopatikana, wahusika watazitapika,” alisema Lukuvi.

Alisema hakuna mteja atakayelazimishwa kulipa kodi kwa mkupuo wa miezi mitatu, sita au mwaka, labda kwa maombi yake na ridhaa na hiyari yake mwenyewe.

WATENDAJI NHC

Akizungumzia utekelezaji wa uhakiki huo, Lukuvi alisema ana uhakika kuwa hautafanikiwa iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, kwa kuwa kuna baadhi ya watendaji wa shirika hilo ambao walihusika kwa namna moja au nyingine katika udanganyifu, ambao watataka kuzuia kubainika.

Alisema ili kuhakikisha uhakiki huo unakuwa na ufanisi, anaagiza uongozi wa juu NHC chini ya Mkurugenzi Mkuu, Maulidi Banyani kuondoa wafanyakazi wote waliopo katika maeneo ya miji mikubwa na kuweka wengine.

“Kama hapa Dar es Salaam, mameneja wote waliopo wanatakiwa waondolewe kwa ajili ya uhakiki, wapelekwe sehemu nyingine. Waondolewe hapa waletwe wengine kwa ajili ya uhakiki. Siyo mameneja tu, kuanzia wale maofisa wa chini.

“Hii inatakiwa kuwahusisha hadi maofisa wadogo kwa sababu hawa ndio wanaoweza kuchomoa mafaili na kuyapoteza, wanaweza kuchangia kukwamisha uhakiki,” alisema.

MAJENGO YA MSAJILI

Lukuvi alisema aliamua kuagiza uhakiki wa majengo yote yaliyotaifishwa na kuwekwa chini ya Msajili wa Majumba, baada ya kubaini kuna mchezo mchafu unaoendelea kufanywa na baadhi ya watu kwa kushirkiana na wanasheria na hata watumishi wa shirika hilo.

Alisema alifanya ziara ya kushtukiza katika nyumba moja, yenye namba 43 iliyopo Kinondoni Ursino, Dar es Salaam ambayo ilikuwa chini ya utaratibu wa msajili, ambayo kwa kuanzia tu walikuta ina shaka katika umiliki wake.

“Nyumba hii ni miongoni mwa zile zilizotaifishwa, lakini mmiliki alipewa aendelee kuishi kwa misingi ya huruma hadi atakapokufa. Makubaliano ni kwamba atakapokufa nyumba hiyo inarudi kwa Serikali, na nyumba hiyo alipewa Mhindi, lakini tumekuta inamilikwia na Mghana,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles