24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Nguvu inahitajika kuwezesha wanawake na wanaume kushiriki katika uchumi-RC Babu

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema nguvu ya ziada inahitajika ili kuwezesha wanawake na wanaume kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi nchini.

Babu ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 5, 2022 katika Tamasha la Jinsia lilionadaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) linaloendelea wilayani Same mkoani Kilimanjaro likiwa na kaulimbiu isemayo: “Haki ya uchumi rasilimali ziwanufaishe wananchi walioko pembezoni kwa maisha endelevu.

Babu amesema licha ya wanawake kuwa zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wote bado hawajaweza kushiriki kikamilifu katika uchumi kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ukatili wa kijinsia, mila na destruri potofu, elimu duni, kutomiliki raslimali za uzalishaji, na kuelemewa na mzigo wa kazi za kuhudumia jamii na familia.

Mkuu huyo wa mkoa amesema katika nchi nyingi za kiafrika ikiwamo Tanzania, wanawake wengi wanakosa haki ya kumiliki ardhi na rasilimali nyingine za uzalishaji huku ukuaji wa sekta ya kilimo ambayo ni uti wa wa uchumi wa nchi umekuwa mdogo kwa muda mrefu.

Ameongeza kuwa licha ya ukweli kwamba zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa Tanzania wanajishughulisha na kilimo huku wanawake wakiwa ni zaidi ya asilimia 80, bado wanawake hawajafaidika vya kutosha kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutokumiliki ardhi, kukosa uwezo wa kukopa mikopo mikubwa, kukosa sauti za maamuzi katika uuzaji na matumizi ya fedha zinazopatikana katika kilimo, kukosa taarifa sahihi za masoko, hali ya hewa na teknolojia sahihi.

“Ni matarajio yangu makubwa kuwa mijadala hii itasaidia kuelimishana na kubadilishana maarifa ambayo yatakuwa chachu ya kuimarisha mikakati ya fursa mbalimbali za kiuchumi zilizoko katika sekta mbalimbali hususani sekta ya kilimo,” ameongeza Babu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, amesema matamasha ya jinsia katika ngazi ya kitaifa yamekuwa chachu kubwa ya kuunganisha sauti ya pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kuendeleza usawa wa njinsia nchini na kwamba matamasha hayo yamekuwa fursa muhimu kwa wanawake na wanaume wa pembezoni kupata maarifa mapya kwa ajili ya maendeleo yao.

“Kama sehemu ya kuendelea kutanua harakati za ujenzi wa nguvu za pamoja nchini na kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki, ilionekana kuna uhitaji wa kuanzisha Tamasha la Jinsia katika ngazi ya Kanda ambalo litaleta pamoja washiriki toka kanda mbalimbali hapa nchini,” alisema.

Lilian amesema kuwa kupitia tamasha la mwaka huu zaidi ya washiriki 500 kutoka maeneo mbalimbali nchini watashiriki kujifunza, kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali kiuchumi, kijamii na kiutamaduni na hivyo kuchochea maendeleo ikiwemo usawa wa kijinsia.

Liundi amesema kutokana na Tanzania kuwa katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa miaka mitano ambao unalenga katika kuleta uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu ni vema kwa kuzingatia masuala ya kijinsia hususani wanawake ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya wananchi wote na vijana ambao ni zaidi ya asilimia 60 ili kuwawezesha kupata fursa ya kuweza kushiriki katika uchumi nchini.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TGNP, Gemma Akilimali amesema tamasha hilo ni moja ya majukwaa ya mtandao huo katika ujenzi wa nguvu za pamoja kwa kuwakutanisha wanawake na wadau wa haki za binadamu kila baada ya mwaka mmoja kubadilishana uzoefu, kusherekea, kutathmini na kupanga mipango ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Ameongeza kuwa tamasha hilo linawakutanisha pamoja mashirika yanayotetea haki za wanawake, katika ngazi ya jamii, na wadau wengine wa maendeleo kujadili masuala mbalimbali.

“Kwa muda mrefu TGNP imekuwa ikifanya uchechemuzi kuhusu suala la mgawanyo wa rasilimali, tunaamini kuwa nchi yetu ya Tanzania sio maskini ila kuna uhitaji wa kuwa na tafakuri ya kina kuhusu matumizi na mgowanyo wa fursa na rasilimali kwa wananchi wote ili kuleta usawa wa jinsia na kuleta chachu ya maendeleo endelevu na jumuishi kupitia bajeti yenye mrengo wa jinsia,” amesema Gema.

Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogolo amesema kuwa licha ya wilaya hiyo kuzalisha kwa wingi zao la Tangawizi bado haifanyi vizuri katika uuzaji wake hali inayosababisha wananchi wake kuendelea kuwa maskini.

Mpogolo ameongeza kuwa kufanyika kwa tamasha la jinsia katika wilaya hiyo ni fursa muhimu itakayowezesha wananchi kujifunza namna bora ya kufanya biashara ya tangawizi ili kuwezesha kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles