NGULI WA HABARI AFARIKI DUNIA

0
627

Na ADAMU MKWEPU-DAR ES SALAAM


TASNIA ya Habari imepata pigo kubwa baada mwandishi wa habari mkongwe na Mhariri wa Mafunzo wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Chrysostom Rweyemamu maarufu ‘Mwalimu’ (63),  kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Rweyemamu alifariki dunia juzi Jumamosi saa 2:30 usiku katika hospitali hiyo, kwa mujibu wa maelezo ya daktari kwa watoto na mke wa marehemu ambao walijulishwa taarifa za kifo hicho jana alfajiri walipokwenda kumjulia hali.

Akizungumzia msiba wa baba yake mtoto mkubwa wa marehemu, George Chrysostom alisema kifo cha ghafla, kwani hadi hadi wanaondoka jana (juzi) jioni Muhimbili, hali ya baba yao ilikuwa ikiendelea vyema kwani alikuwa akizungumza vizuri  baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe uliokuwa tumboni.

“Baba alikuwa mzima na alikuwa akizungumza na hata kuwatambua watu wote waliokuwapo pale na aliweza kwenda kuoga vyema jioni ya jana kabla ya wao kuondoka,” alisema George.

Kwa mujibu wa maelezo waliyopewa na daktari aliyekuwa akimtibu, marehemu kabla ya kufikwa na umauti alianza kupata shida ya kupumua ghafla, hatua iliyosababisha daktari aliyekuwa akimhudumia kuitwa na kujaribu kuokoa maisha yake bila mafanikio.

Kutokana na hali hiyo alisema daktari aliwaeleza kwamba upo uwezekano mkubwa marehemu alipata tatizo la damu kuganda katika mapafu hali iliyosababisha apate mshituko wa moyo uliochukua maisha yake.

“Baba alikuwa mzima na alikuwa akizungumza na hata kuwatambua watu wote waliokuwapo pale na aliweza kwenda kuoga vyema jana (juzi) jioni kabla ya wao kuondoka,” alisema

Mtoto huyo wa marehemu alisema mipango ya mazishi inaendelea kufanyika nyumbani kwa marehemu na pindi itakapokamilika wanatarajiwa kusafirisha mwili kwenda kwao wilayani Muleba, Kishanda katika Kijiji cha Iyunga mkoani Kagera ambako mazishi yatafanyika katika siku ambayo itatangazwa baadaye.

Hivi sasa wanasubiriwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya kikao cha pamoja cha familia kinachotarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia jana jioni.

Mwalimu Chrysostom Rweyemamu ameacha mjane na watoto watatu wa kiume.

Marehemu Chrysostom Rweyemamu, alijiunga na Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Oktoba mwaka 1999 wakati huo ikijulikana kama Habari Corporation na kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Maarifa Media Trust (MAMET).

Akizungumzia msiba huo, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni New Habari (2006) Ltd, inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa, Dimba na The African, Absalom Kibanda alisema. “Marehemu alikuwa akisumbuliwa na uvimbe tumboni na kutokana na tatizo hilo, alilazwa wiki tatu akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili.

“Hata hivyo kabla ya kukutwa na umauti, juzi alifanyiwa upasuaji wa uvimbe huo lakini baadaye wakati akisubiri hali yake iimarike kabla ya kuruhusiwa ndipo tukapata taarifa ya kifo chake,” alisema Kibanda.

Kibanda alisema Kampuni ya New Habari kwa kushirikiana na familia wapo kwenye mipango ya mazishi inayofanyika nyumbani kwake Mbweni jijini Dar es Salaam.

Nafasi alizoshika

Akiwa ndani ya kampuni hiyo marehemu alifanikiwa kuongoza katika ngazi mbalimbali ambapo kabla ya kifo chake alikuwa Mhariri wa Mafunzo.

Desemba 2002 hadi Juni 2005  marehemu alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji wa kampuni ya Habari Corporation na baadaye Julai 2005 hadi 2006  alikuwa Mhariri wa Gazeti la siasa la Rai katika kampuni hiyo.

Aidha marehemu alifikisha umri wa kustaafu mwaka 2014 lakini kutokana na uzoefu wake na uchapakazi katika tasnia ya habari alipewa mkataba maalumu kuwa Mhariri Mshauri Mkufunzi katika Kampuni ya New Habari (2006) Ltd,  wadhifa alioushika hadi umauti ulipomkuta.

Mbali na kufanya kazi katika Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, marehemu alishika nyadhifa mbalimbali katika tasnia ya habari akiwa Mjumbe wa Kamati ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT), Msuluhishi na mkufunzi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Elimu yake

Marehemu Rweyemamu alizaliwa Machi 9, mwaka 1954 na baada ya kumaliza elimu yake ya msingi alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo Januari mwaka 1970 hadi 1973.

Baada ya kumaliza elimu yake Sekondari yaani O- Level Januari mwaka 1974 hadi 1975, alijiunga na Shule ya Mirambo High School.

Mwaka 1977 hadi 1978, Marehemu alifanikiwa kuhitimu ngazi ya Stashahada ya ualimu na mwaka 1981 hadi 1984 akasomea shahada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mwaka 1989 hadi 1990 Marehemu alihitimu Stashahada ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya.

Taaluma

Juni hadi Julai 1988, Marehemu alihitimu mafunzo ya uandishi wa habari, nchini Ujerumani yaliyokuwa yakitolewa na UNFP na CADA jijini Dar es Salaam Agosti mwaka 1991.

Mwaka 1992, alihitimu mafunzo ya ukufunzi katika chuo cha UDSM pamoja na mafunzo ya mazingira ya uandishi katika Chuo Kikuu cha Kampala, Uganda mwaka 1995.

Julai mwaka 1996, alipata mafunzo ya Bayoanuwai kutoka Taasisi ya IUCN jijini Nairobi nchini Kenya na mwaka 1999 alihitimu mafunzo ya ubunifu na usimamizi wa miradi katika mji wa  Nyeri nchini humo.

Marehemu alifariki akiwa mwanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAJA), Taasisi ya Kimataifa ya Waandishi wa Habari (IOJ), Baraza la Elimu ya Mawasiliano ya Vyombo vya Habari Afrika (ACCE), Chama cha Wakufunzi wa  waandishi  wa Habari Jumuiya ya Madola.

Mbali na hizo pia alikuwa mwanachama mwanzilishi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), Chama cha Waandishi na Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (AJM), Umoja wa Kimataifa wa Uandishi wa Habari (IFJ) pamoja na kuwa mshauri na mkufunzi kwa waandishi wa vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here