31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

NGOME YA MBOWE YAZIDI KUTIKISWA

Na OMARY MLEKWA – HAI


MADIWANI watano kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Jimbo la Hai, ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, wamejiuzulu nyadhifa  zao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Madiwani hao ni Yohana Laiza (Kata ya Kia), Everest Kimathi (Kata ya Mnadani), Abdalla Chiliwi (Kata ya Weruweru), Goodluck Kimaro (Kata ya Machame Magharibi) na Robsoni Kimaro (Kata ya Uroki).

Ikumbukwe kuwa, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015,  Chadema kilipata madiwani katika kata zote 17 za Jimbo la Hai.

Madiwani hao wamejiuzulu kwa nyakati tofauti na sababu mbalimbali. Diwani wa hivi karibuni kabisa kujiuzulu ni Yohana Laiza, ambaye alichukua uamuzi huo juzi jioni, kwa sababu ya kile alichokisema kuwa anaunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Sanya Station na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Laiza alisema amechukua uamuzi huo kutokana na kuridhishwa na uamuzi wa Mkuu huyo wa Wilaya ambaye ni mpya, kutembelea kata hiyo na kusikiliza kero za wananchi, hususan mgogoro uliopo kati ya wananchi na uongozi wa Kiwanja cha Ndege cha KIA.

“Nimeamua kuachia nyadhifa zangu zote ndani ya Chadema kutokana na DC kutembelea kata yangu na kusikiliza kero za wananchi, kitu ambacho hakikufanyika kwa muda na badala yake viongozi walikuwa wanakuja na kusikiliza upande mmoja, lakini kwa uamuzi wake wa kufika hapa nimepata imani kuwa CCM imedhamiria kumaliza mgogoro huo.

“Nilikwenda Chadema kwa ajili ya kutafuta mabadiliko, lakini kwa sasa nayaona mabadiliko ndani ya CCM, tumeona jinsi Serikali ilivyojizatiti kuleta maendeleo, ikiwamo kuboresha sekta ya miundombinu kwa kuleta ndege kubwa iliyotua katika Uwanja wa Kia mwisho wa wiki iliyopita,” alisema Laiza.

Baada ya maelezo hayo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Bazil Lema, alipoulizwa taarifa ya kujiuzulu kwa diwani huyo alisema hana taarifa rasmi za kujiuzulu kwake.

Alisema kama ni kweli diwani huyo kajiuzulu, uamuzi wake utakuwa umetokana na hofu ya kesi ya tuhuma za ubakaji na kumpa ujauzito mwanafunzi ambayo inamkabili katika Mahakama ya Wilaya ya Hai, kwamba ameona CCM inaweza kumsaidia katika kesi hiyo.

Agosti 1, mwaka huu, Laiza alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo na kusomewa maelezo ya awali ya makosa mawili ya tuhuma za kumbaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi ya Obrien.

Mwendesha Mashitaka Mkaguzi wa Polisi, Hawa Hamisi, mbele ya hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Devotha Msofe, alidai kuwa, upande wa mashitaka umejiandaa kuleta mashahidi kumi kwa ajili ya shauri hilo, linalotarajiwa kuanza kusikilizwa Agosti 29, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles