Mohamed Hamad, Kiteto
Barabara ya km 88.4 iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni sita kutoka Kata ya Nameleck, Lortepesi na Sunya, imeharibika vibaya na mifugo wakiwamo ng’ombe na punda wanaochungwa barabarani na wafugaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamimu Kambona amesema, barabara hiyo iliwekwa alama zote za barabarani lakini zimeng’olewa ambapo hata katika maeneo ya vivuko vya mifugo, ng’ombe hawapiti na badala yake mifugo hiyo imekuwa ikitembezwa barabarani kama magari.
“Miundombinu ya barabara imeharibiwa ikiwamo ya Kibaya Ndedo, Kibaya Kijungu na maeneo mengine kama Lengatei na Sunya kuna uharibifu mkubwa ikiwamo mifugo kutembezwa barabarani ikizingatiwa Serikali imetumia gharama kubwa,” amesema.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ndedo, Paulo Laiza akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kata yake amesema, kila mara mifugo imeendelea kugongwa katika eneo lake na kusababisha umaskini kwa wananchi hao na kuomba Serikali kuingilia kati.
“Mwenyekiti naomba Serikali itusaidie eneo langu la Ndedo ni juzi tu ng’ombe 24 waligongwa barabarani na kila mara nimekuwa nikilalamika hapa mifugo kugongwa cha ajabu mwenye mifugo tena ndiyo anayetakiwa kulipa gari, huu unyanyasaji utaendelea hadi lini,” amehoji Laiza.
Aidha, Diwani wa Kata ya Partimbo, Paulo Tunyoni ameiomba Serikali kuelimisha wafugaji kutotembeza mifugo hiyo barabarani sanjari na kuwekwa alama za barabarani, maeneo ya kuvukia mifugo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto na Diwani wa Kata ya Chapakazi, Lairumbe Mollel, amesema kwenye kikao cha madiwani cha taarifa za robo ya kwanza ya mwaka kuwa sheria zilizopo mfugo mmoja akikamatwa anatakiwa kutozwa faini ya Sh 5,000.
“Waheshimiwa madiwani tulipitisha sheria, jukumu letu ni kuelimisha watu wetu ili kupunguza madhara, ikumbukwe hili suala la mifugo kugongwa barabarani ni kila mara, cha kusisitiza hapa tengenezeni maeneo ya mapalio ya kupitisha mifugo,” amesema.