MADRID, HISPANIA
WABABE wa soka nchini Hispania Barcelona na Real Madrid, wanaendelea kupigana vikumbo kwa ajili ya kuwania saini ya mshambuliaji wa PSG, Neymar kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu nchini Hispania wiki ijayo.
Ligi ya Hispania inatarajia kuanza kutimua vumbi Ijumaa ya wiki ijayo, huku uhamisho wa Neymar ukisubiliwa kwa hamu kubwa nchini humo.
Nyota huyo raia wa nchini Brazil, amethibitisha anataka kuondoka katika klabu hiyo ya PSG katika kipindi hiki cha majira ya joto ambapo dirisha la usajili nchin Hispania bado lipo wazi hadi Septamba 2 mwaka huu.
Neymar ambaye aliwahi kuitumikia Barcelona kwa mafanikio makubwa kuanzia mwaka 2013 hadi 2017, aliweka rekodi ya uhamisho wake kwa kitita cha pauni milioni 198, lakini sasa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 ameonesha dalili za kutaka kurudi katika klabu hiyo ya zamani, lakini Madrid na wao wanataka kuonesha jeuri ya fedha kumsajili mchezaji huyo.
Madrid wamedai wapo tayari kuvunja benki yao kumsajili mchezaji huyo baada ya kushindwa kuipata saini ya kiungo mshambuliaji wa Manchester United, Paul Pogba ambapo dirisha la usajili la Uingereza likifungwa juzi.
Sababu za Manchester United kugoma kumuuza Pogba kwa Real Madrid ni kutokana na kukosa mbadala wake katika kipindi hiki cha kiangazi.
Matajiri wa soka nchini Ufaransa, PSG wameripotiwa kuwa tayari kumuacha Neymar akiondoka kwenye kikosi chao kwa uhamisho wa pauni milioni 110 pamoja na wapewe mchezaji mmoja. Kwa upande wa Barcelona waliwataja miongoni mwa wachezaji wao sita ili waweze kumchagua mmoja pamoja na kupewa fedha ili waweze kumrudisha Neymar kikosini, lakini PSG wanaonekana kuhitaji fedha zaidi kuliko mchezaji.
Uongozi wa PSG, unadaiwa kuchoshwa na tabia za mchezaji huyo alizozionesha katika msimu uliopita.