RIO DE JANEIRO, BRAZIL
TIMU ya taifa ya Brazil, itaikosa huduma ya mshambuliaji wake Neymar de Santos kwenye michuano ya Kombe la Copa America baada ya kuchanika enka ya kulia usiku wa kuamkia jana wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Qatar.
Michuano hiyo ya Kombe la Copa America inatarajia kuanza kutimua vumbi Ijumaa ya wiki ijayo huko nchini Brazil huku Brazil wakiwa wenyeji.
Shirikisho la soka nchini Brazil, limethibitisha kuumia kwa mchezaji huyo huku timu yake ikifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, lakini mchezaji huyo alionekana akitoka uwanjani huku akilia.
“Baada ya Neymar kuchanika enka ya mguu wa kulia usiku wa kuamkia jana kwenye mchezo dhidi ya Qatar, vipimo vinaonesha kwamba, atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.
“Kutokana na hali hiyo ni wazi kwamba, Neymar hatoweza kuwa fiti kwa ajili ya kushiriki michuano ya Copa America ambayo inatarajia kuanza kufanyika wiki ijayo hapa Brazil.
“Uongozi wa timu ya Brazil unatarajia kukutana mapema iwezekanavyo kwa ajili ya kuona nani anaweza kuchukua nafasi ya mchezaji huyo,” lilisema shirikisho hilo.
Katika mchezo huo wa juzi, Neymar aliongoza safu ya ushambuliaji akiwa pamoja na Richarlison na Gabriel Jesus, lakini mchezaji huyo aliumia katika dakika ya 21. Kuna uwezekano mkubwa wa nafasi ya Neymar ikazibwa na Everton Soares ambaye anakipiga katika klabu ya Gremio.
Msimu uliomalizika hivi karibuni Neymar alikuwa katika wakati mguu kutokana na kusumbuliwa na majeruhi, lakini amemaliza msimu huu akiwa na jumla ya mabao 23 kwenye michuano mbalimbali lakini kati ya hayo amefunga mabao 15 ya Ligi Kuu ndani ya timu yake ya PSG.
Mwishoni mwa mwezi uliopita Neymar alivuliwa unahodha kuelekea michuano hiyo mikubwa ya America ya Kusini na nafasi yake ikachukuliwa na beki wa pembeni Dani Alves, huku Neymar akidaiwa kukosa nidhamu.