21.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

NEYMAR AITIMUA MEXICO URUSI

SAMARA ARENA, URUSI


 

MSHAMBULIAJI wa Brazil, Neymar Jr, ameivusha timu ya Taifa ya nchi hiyo hatua ya robo fainali baada ya jana kufunga bao moja kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mexico, mchezo wa hatua ya 16 ya michuano ya Kombe la Dunia inayoendelea nchini Urusi.

Mabao ya Brazil yalifungwa na Neymar  dakika ya 51 na Roberto Firmino dakika ya 88.

Dakika ya saba, Neymar, alishindwa kuipatia Brazil bao la kuongoza akiwa katika nafasi nzuri baada ya  kipa wa  Mexico, Guillermo Ochoa, kupangua mchomo wake.

Mexico ilijibu kwa kufanya shambulizi dakika ya 10, lakini beki wa Brazil, Fagner Lemos, alikuwa imara kuokoa  mpira wa hatari usilete madhara langoni mwao.

Mexico ilionekana kuimudu vema Brazil dakika 15 za awali kutokana na kuokoa mipira mingi ya hatari ambayo ingeweza kuleta madhara.

Pia ilifanya mashambulizi kadhaa ya kushtukiza kupitia kwa Chicharito na  Hirving Lozano, lakini kikwazo kilikuwa kwa ukuta wa Brazil uliokuwa chini ya Thiago Silva na Filipe Luis.

Kwa upande mwingine, Neymar na Willian da Silva, mara kwa mara walilitia kashkashi lango la Mexico ambayo wa kiasi kikubwa ilibebwa na uhodari wa kipa wao Ochoa.

Pamoja na jitihada za kila upande kutaka kuandika bao la kuongoza, dakika 45 za kipute hicho zilimalizika kwa nyavu kubaki salama bila kutikiswa.

Kipindi cha pili, kasi ya mchezo huo iliongezeka kutokana na kila upande kusaka bao la kuongoza.

Hata hivyo, Mexico iliendelea na mbinu yake ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza na kuiacha Brazil ikimiliki mpira.

Mbinu hii ndiyo iliyoisaidia Mexico kuichapa Ujerumani, ikimuacha mshambuliaji wao, Jesus Gallardo, karibu na eneo la wapinzani.

Dakika 51, Willian aliwahadaa mabeki wa Mexico kabla ya kumdondoshea pasi makini, Neymar ambaye hakujiuliza nini cha kufanya zaidi ya kuukwamisha mpira wavuni.

Bao hilo liliilazimisha Mexico kufanya mabadiliko dakika ya 55, alitoka Edison Alvarez na nafasi yake kuchukuliwa na Jonathan Dos Santos.

Brazil nayo ilifanya mabadiliko dakika ya 86 kwa kumpuzisha Philippe Coutinho na nafasi yake kuchukuliwa na Roberto Firmino.

Mabadiliko hayo yalikuwa na manufaa kwa Brazil kwani dakika ya 88 ilifanikiwa kuandika bao la pili na la ushindi kupitia kwa Firmino.

Kiungo huyo wa Liverpool ya England alifunga bao hilo baada ya kumalizia wavuni mpira uliotemwa na Ochoa aliyepangua kiki ya Neymar.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,654FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles