27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

NEY WA MITEGO AMGUSA JPM

Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA


RAIS Dk. John Magufuli, ameliagiza Jeshi la Polisi kumwachia huru msanii wa muziki wa kizazi kipya, Elibariki Emmanuel, maarufu Ney wa Mitego, ambaye alikamatwa na jeshi hilo kwa tuhuma za uchochezi kupitia wimbo wake mpya wa ‘Wapo’.

Mbali na hilo, Rais Magufuli amelitaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuondoa katazo la kuchezwa kwa wimbo huo katika vyombo mbalimbali vya habari.

Akizungumza mjini Dodoma jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema Rais Magufuli ameagiza msanii huyo aachiwe huru bila kuhojiwa kwa kuwa wimbo wake ni mzuri na alichoimba ni mawazo ya mtunzi.

“Nilipozungumza na Rais Magufuli leo (jana) asubuhi, lilijitokeza suala la mwanamziki Ney, maana naye ni mpenzi wa muziki na huyo ni mmoja wa wasanii anaowapenda. Aliniuliza hivi kuna nini maana ninaona kwenye magazeti?  Nikamjibu na mimi nimekuja ku-prove sababu ni huo wimbo wake wa ‘Wapo’.

“Mh Rais akaniuliza umeusikiliza huo wimbo, nikamwambia bado. Ajaniambia hebu utafute huo wimbo ama nikutumie? Nikaona ni habari nzuri, kumbe anao na anausikiliza kila siku, akaniambia anaupenda na mimi nikausikiliza pia.

“Siyo kwamba Basata wamevunja sheria, bali wamefuata sheria iliyoanzisha hicho chombo na wana imani kabisa huo wimbo umekiuka maudhui ya sheria hiyo na kanuni zake, kwa hiyo wakatumia hiyo sheria kumkamata na kumpeleka jijini Dar es Salaam,’’ alisema.

 Dk. Mwakyembe alisema kuwa Rais Magufuli alimuuliza analionaje suala hilo ikabidi akutane na viongozi wakuu wa wizara na Naibu Katibu Mkuu kushauriana.

“Aliniuliza suala hilo waziri unalionaje, ikabidi na mimi nifanye consultation (ushauri) na viongozi wakuu wa wizara na Naibu Katibu Mkuu na kuwaeleza kwamba hata Rais naye ameshangaa.

 “Kwa hiyo hata mheshimiwa Rais mwenyewe ameomba niliangalie mimi mwenyewe nalionaje, nikasema sawa nitaliangalia, nadhani huyu kijana alichofanya ni ku-express opinion yake, ni uhuru wa kuongea na Mheshimiwa Rais akasema ni lazima tumlinde kwa kuwa hajavuka mipaka,’’ alisema.

Dk. Mwakyembe, alisema kuwa Rais alimwambia kuwa kwa upande wake ni wimbo mzuri.

“Alinihakikishia kuwa hata mdundo wa wimbo huo unaweza kuchezesha hata mguu kutokana na mdundo mzuri, lakini hata hivyo Rais ameshauri wimbo huo uboreshwe ili uwe mzuri zaidi.

“Nilipozungumza tena na Rais ameniambia niongee na huyo msanii asiondoe kitu chochote, ila aongeze kitu katika ujumbe wake anaozungumzia changamoto zilizopo katika jamii huku watu wakiitikia wapo… watu wenye tabia hizi wapo…

“Rais alisema kuna vitu mwandishi amesahau kuviweka, wakwepaji kodi, wabwia unga na mihadarati, wanaokaa kwenye vijiwe bila kufanya kazi nao awaimbe na watu waitikie wapo…,” alisema Dk. Mwakyembe.

Aliongeza: “Nashauri Basata wamlete Dodoma, nitafurahi kumwona kesho ili nimwelekeze vizuri hata mambo ya kuongeza, naamini wimbo utakuwa mzuri kweli na mimi mwenyewe nimeisikiliza ile ‘biti’, nakubaliana na Rais.”

Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Magufuli, Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu Profesa J (Chadema), alisema hiyo ni habari njema kwa wasanii kwa kuwa wengi wao walikosa uhuru wa kuzungumzia mambo mbalimbali katika jamii kwa hofu ya Serikali na vyombo vya dola.

“Hii ni habari njema, nilikuwa sijui kama wimbo wa Ney umeruhusiwa, kila mtu ana uhuru wa kuwasilisha alichonacho, kama ni kibaya unaachana nacho, kama ni kizuri unachukua. Hii ni habari njema sana kwetu wasanii wote, sasa tutakuwa na uhuru wa kuzungumza,” alisema Profesa J.

 

ALIVYOKAMATWA

Nay alikamatwa na polisi juzi usiku mkoani Morogoro alikokwenda kwa shughuli za muziki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema msanii huyo alikamatwa maeneo ya Turiani akitokea Mpwapwa mkoani Dodoma.

 

MARUFUKU YA BASATA

Awali Basata kupitia kwa Katibu Mtendaji, Godfrey Mngereza, waliufungia wimbo huo kwa madai kuwa hauna maadili na unachochea vurugu, huku baraza hilo likionya mtu yeyote kutoupiga katika vyombo vya babari wala kuusambaza katika mitandao ya kijamii.

 

NYIMBO ZAKE ZILIZOFUNGIWA

Kabla wimbo huo, Nay amewahi kufungiwa nyimbo zake nyingine tatu; ‘Shika Adabu Yako’, ‘Pale Kati’ uliodaiwa kuwakashifu na kuwadhalilisha wanawake na  ‘Itafahamika’ aliowaimba wasanii wenzake hadi kumgombanisha na msanii Godfrey Tumaini aliye maarufu kwa jina la Dudu Baya.

 

TIMU MABADILIKO

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Ney aliongoza kundi la wasanii 50 kufanya kampeni za mgombea urais wa Chadema aliyeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa, huku akitamba na wimbo wake uitwao ‘Lowassa’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles