Ney wa Mitego afunguliwa, awekwa chini ya uangalizi

captureney-goodluck-mchik (1)

Na YASSIN ISSAH, DAR ES SALAAM

LICHA ya Baraza la Taifa la Sanaa Tanzania (Basata) kumfungulia msanii wa kizazi kipya, Emmanuel Elibariki (Ney wa Mitego kuendelea na shughuli za sanaa kwa sasa atakuwa chini ya uangalizi maalumu ili aendeshe shughuli za kisanaa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu sambamba na maadili katika kazi zake.

Baraza hilo limeeleza kumfungulia msanii huyo baada ya kutekeleza masharti ya adhabu aliyopewa ikiwemo kulipa Sh milioni moja huku likivitaka vyombo vyote vya habari na Watanzania kwa ujumla kuendelea kutoucheza wimbo huo hadi baraza hilo litakapotangaza upya.

Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Godfrey Mngereza, alisema msanii  huyu amefunguliwa baada ya kujutia na kukiri kuwa amejifunza na yuko tayari kujirekebisha ndiyo maana pia wamemkabidhi vyeti vya kusajiliwa na baraza hilo.

Julai 27 mwaka huu baraza hilo lilimfungia msanii huyo kwa kipindi kisichojulikana na kumtaka kutekeleza maagizo ya kuhakikisha amesajiliwa na kuwa na kibali cha kuendesha shughuli za sanaa, kulipa faini ya Sh 1,000,000 kuwaomba radhi Watanzania kupitia mikutano na waandishi wa habari ikiwa  ni pamoja na kufanya marekebisho ya wimbo wake wa ‘Pale Kati’ ili ubebe maudhui yenye maadili.

Hata hivyo, Mngereza aliwaasa wasanii kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za sanaa sambamba na kuzingatia maadili katika kila kazi wanazobuni ili waepuke matatizo yasiyo ya lazima.

Naye Ney wa Mitego, alipongeza baraza hilo kumalizana naye huku akisisitiza kujirekebisha kwa kutoa wimbo wa kuwafariji mashabiki wake na kuondokana na masuala ya kufungiwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here