24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

New Zealand: Jacinda Ardern ashinda kwa kishindo

WELLINGTON, NEW ZEALAND

WAZIRI MKUU wa New Zealand, Jacinda Ardern amepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana. 

Ushindi huo unakipa chama chake cha Labour nafasi ya kuunda serikali bila ya kuvishirikisha vyama vingine.

Jacinda Ardern ameshinda kwa kishindo na kupata wingi wa viti bungeni utakaomwezesha kutekeleza mpango wake wa mageuzi.

Baada ya kuhesabiwa theluthi mbili ya kura zote, chama cha Waziri Mkuu Adern cha Labour kimepata asilimia 49.2 ya kura zote, huku kikitarajiwa kupata viti 64 katika bunge la New Zealand lenye viti 120.  

Hakuna kiongozi mwingine aliyeweza kupata ushindi mkubwa kiasi hicho tangu New Zealand ilipoidhinisha mfumo wa uchaguzi unaozingatia uwiano wa uwakilishi wa kivyama mwaka 1996. 

Kukosa ushindi wa moja kwa moja kumevilazimisha vyama vilivyoongoza katika kura tangu wakati huo, kuunda serikali zinazovishirikisha vyama kadhaa vingine.

Hata kabla ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu kura, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Judith Collins amekwishampigia simu Waziri Mkuu Ardern, akikubali kushindwa.

Chama cha kihafidhina cha National Party cha Judith Collins kinatazamiwa kuambulia viti 35 bungeni, hayo yakiwa matokeo mabaya zaidi kwa chama hicho kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.

”Hongera kwa ushindi wako, kwa sababu naamini ni ushindi mkubwa kwa chama cha Labour. Imekuwa kampeni ngumu sana,” alisema Collins mbele ya umati mjini Auckland.

Ushindi huu wa Jacinda Ardern ni mkubwa kuliko ilivyokuwa imetabiriwa katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura, na wa juu zaidi kwa chama cha Labour tangu mwaka 1946.

Rais wa chama cha Labour Claire Szabo amesifu kampeni iliyofanywa na Ardern, mwanasiasa mchangamfu ambaye amesababisha wimbi la ushabiki kwa chama hicho alipochukua uongozi wake mwaka 2017, wakati huo chama hicho kikiwa kinaburura mkia katika chunguzi za kura za maoni.

Szabo amesema ”bila shaka yoyote uongozi mahiri wa Jacinda Ardern umetoa mchango mkubwa katika maendeleo mazuri ya chama.”

Ushindi uliotokana na kuyakabili majaribu Jacinda Ardern alikuwa ameupachika uchaguzi huu jina la ”Uchaguzi wa Covid” na juhudi zake zilikuwa kunadi mafanikio ya serikali yake katika kusimamisha maambukizi ya ugonjwa huo. 

New Zealand yenye wakazi milioni tano, imekwisharekodi vifo 25 tu kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Uchaguzi huu ulisogezwa nyuma kutokana na kuripuka kwa ugonjwa wa COVID-19 lakini janga la virusi vya corona ni moja tu kati ya changamoto lukuki zilizodhihirisha sifa za uongozi wa Ardern katika muhula wake wa kwanza kwenye uongozi.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 40 alionyesha moyo wa huruma, lakini pia ujasiri wa maamuzi baada ya shambulizi la bunduki lililofanywa mwaka jana na mtu mwenye itikadi ya kuwatukuza wazungu, ambaye aliuawa watu 51 waliokuwa wakisali misikitini katika mji wa Christchurch.

Kiongozi huyo alijikuta pia akikabiliwa na jukumu la kulifariji taifa lake baada ya mripuko wa volkano katika kisiwa cha Whakaari, ambao uliuwa watu 21 na kuwaacha wengi kadhaa wakiwa na majeraha mabaya.

”Bila kujali ukubwa wa mzozo ninaokabiliana nao, nawahakikishieni kuwa nitajitolea kikamilifu kwa kazi hii, hata kama hali hiyo itanilazimu kulipa gharama kubwa,” aliyasema hayo Jacinda Ardern mapema wiki hii.

Uchaguzi huu ulikuwa umepangwa kufanyika Septemba 19, lakini ulisogezwa mbele kutokana na mripuko wa ugonjwa wa COVID-19 katika mji wa Auckland, ambao hivi sasa umekwishadhibitiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles