21.9 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Netanyahu ang’ang’ania madarakani

JERUSALEM, ISRAEL

WAZIRI Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amekataa katakata kuondoka madarakani baada ya kushtakiwa na tuhuma za kutoa hongo, kufanya udanganyifu na kuwavunja imani raia waliomchagua kuhusiana na kesi tatu tofauti.

Taarifa hizo zinajiri huku kukiwa na mkwamo wa kisiasa nchini Israel kufuatia chaguzi mbili kuu ambazo hazifanikiwa kufikia tamati mwezi Aprili na Septemba.

Jumatano wiki hii, mpinzani wa Netanyahu, Benny Gantz alisema ameshindwa kuunda serikali ya muungano na walio wengi bungeni.

Alipewa fursa kujaribu baada ya Netanyahu kushindwa kufanya hivyo.

Kiongozi wa chama cha Bluu na Nyeupe yani Blue and White party, Benny Gantz, amerejesha jukumu lake la kuunda serikali na kuibua uwezekano wa kufanyika uchaguzi wa tatu ndani ya mwaka huu. 

Kiongozi huyo alikuwa na muda wa siku 28 wa kuunda serikali baada ya waziri mkuu na kiongozi wa chama cha Likud Netanyahu naye kushindwa kuiunda serikali.

Mbunge yeyote akiwemo Gantz na Netanyahu watakuwa na siku 21, angalau kutafuta uungwaji mkono wa wabunge 61 na kisha kujaribu kuunda serikali ya muungano. 

Mbunge atakayepata uungwaji mkono kama huo atapewa muda wa siku 14 wa kuunda serikali.

Ikiwa itashindikana kutaitishwa uchaguzi mpya ambao huenda ukafanyika mwezi Machi

Pengine kutokana na hali hiyo, Netanyahu ameyashutumu mashtaka hayo kama jaribio la mapinduzi dhidi yake. 

 “Sitakubali uongo kushamiri,” alisema katika hotuba ya kupinga kesi hiyo na kuongeza;  “Nitaendelea kuongoza taifa hili , kulingana na sheria ya nchi,”. 

Netanyahu alidaiwa kukubali kuchukua zawadi kutoka kwa wafanyabiashara matajiri na kutoa hongo ili kuweza kuwa katika vyombo vya habari mara kwa mara.

Katika hotuba ya dakika 15, Netanyahu alishutumu Idara ya Mahakama , maofisa wa polisi na wengine kwa kupanga njama dhidi yake wakiwa na nia yenye madai ya msukumo wa kisiasa.

”Katika mchakato huu mzima uliotiwa doa wachunguzi hawakuwa wakitafuta ukweli bali walikuwa wakinitafuta” , alisema akiwashutumu wachunguzi hao kwa kuwahonga mashahidi ili kusema uongo.

Awali mwanasheria mkuu, Avichai Mandelblit alisema alitoa uamuzi huo kwa ‘moyo mzito’ lakini akasema imeonyesha kwamba hakuna asiyeweza kushtakiwa nchini Israel.

“Hatuna budi kufuata sheria – sio suala la kisiasa,” alisema.

Wafuasi wa Netanyahu walikusanyika nje ya ofisi ya waziri mkuu ili kupinga mashtaka hayo.

Maandamano pia yalifanyika dhidi ya Netanyahu.

Rais Reuven Rivlin aliwaomba wabunge Alhamisi wiki hii kukubaliana kuhusu mtu atakayechukua wadhfa wa uwaziri mkuu katika kipindi cha siku 21 ili kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mwingine wa tatu.

Baada ya mashtaka hayo kutangazwa, Gantz alichapisha ujumbe wa Twitter akimuunga mkono mwanasheria mkuu na maofisa wa polisi na kuandika “ni siku ya kuhuzunisha”.

Mwanasheria mkuu Mandelblit alisema mwezi Februari kwamba alilenga kumshtaki Netanyahu kutokana na kesi tatu tofauti zinazojulikana kama kesi 1000, kesi 2000 na kesi 4000 kabla ya kesi hiyo kusikilizwa mwezi uliopita.

Kesi ya 1000: Netanyahu ameshtakiwa na ulaghai na kuwavunja imani raia. Anadaiwa kupokea zawadi ya thamani ya juu ikiwemo mvinyo na sigara, kwa lengo la kumsaidia tajiri mmoja rafikiye. 

Netanyahu anasema kwamba alipokea vitu hivyo kama zawadi ya kirafiki na kwamba hakumfanyia hisani yoyote rafiki huyo. Rafiki huyo pia amekana kufanya makosa yoyote.

Kesi 2,000: Netanyahu anakabiliwa na mashtaka ya ulaghai na uvunjaji wa imani. 

Anadaiwa kukubaliana na mchapishaji wa gazeti moja kuweka sheria za kudhoofisha gazeti pinzani kwa lengo la kuangaziwa mara kwa mara na gazeti hilo. 

Mchapishaji huyo ameshtakiwa na mashtaka ya kutoa hongo . 

Sawa na waziri huyo mchapishaji wa gazeti hilo amekana kufanya makosa yoyote. 

Wote wawili wamesema kuwa hawakuwa na lengo la kukuza masuala waliozungumzia katika mkutano wao na kwamba hakuna sheria kama hiyo iliopitishwa.

Kesi 4,000: Haya ndio madai makali kwa sababu Netanyahu ameshtakiwa na tuhuma za kutoa hongo pamoja na ulaghai na uvunjaji wa imani za wengi. 

Imedaiwa kwamba alipitisha maamuzi ambayo yalikuwa yakipendelea kampuni moja ya mawasiliano kwa lengo la kuangaziwa mara kwa mara na vyombo vya habari, ikiwa ni miongoni mwa makubaliano na mwanahisa mkuu wa kampuni hiyo. 

Waziri mkuu amesisitiza kwamba wataalam waliunga mkono uamuzi huo na kwamba hakulipwa chochote. 

Mwanahisa huyo ambaye pia naye amefunguliwa mashtaka ya hongo amekana madai hayo.

Haijulikani hatua hiii ina maanisha nini kwa hatma ya Netanyahu kwani hajapatikana na hatia yoyote kufikia sasa na kwamba hakuna sheria yoyote inayomzuia kusalia katika ofisi kama waziri mkuu.

Inaelezwa kuwa inaweza kuchukua miezi mingi kabla ya kesi hiyo kuwasilishwa katika mahakama ya wilaya.

Iwapo atapatikana na hatia, Netanyahu hataruhusiwa kujiuzulu hadi pale kesi ya kukata rufaa uamuzi huo itakaposikilizwa na kukamilishwa suala ambalo linaweza kuchukua miaka kadhaa.

Waandishi wanasema kwamba wengi wataulizia uwezo wa waziri huyo mkuu kusimamia masuala ya serikali iwapo anaendelea na kesi mahakamani.

Mashirika yasio ya serikali yanaweza kuwasilisha kesi katika mahakama ya juu kushinikiza Netanyahu kujiuzulu.

Mahakama awali ilikuwa imeamuru kwamba waziri aliyeshtakiwa na tuhuma za uhalifu ni sharti kujiuzulu la sivyo aondolewa katika ofisi na itaamua iwapo hatua kama hiyo pia inaweza kumuathiri waziri mkuu.

Washirika wa waziri mkuu bungeni wanaweza kupitisha sheria ambayo inaweza kumpatia kinga ya kushtakiwa akiwa ofisini na kuruhusu wabunge kufutilia mbali uamuzi wa mahakama ya juu iliyomuondolea kinga hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,719FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles