27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

NEMC yahimiza ushirikiano na halmashauri kulinda mazingira

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

BARAZA la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira nchini (NEMC) limeziomba halmashauri nchini kuweka mazingira safi na salama ili kulinda afya za watu na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.

Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, amesema kwamba mafanikio ya nchi ya kiuchumi lazima yaendane na ustawi, usimamizi na utunzwaji wa mazingira ili kulinda afya za watu, uhai wa viumbe wengine na kuwavutia wawekezaji.

“Nchi yetu imepata mafanikio makubwa. Ili mafanikio haya yawe endelevu, lazima halmashauri zihakikishe mazingira ni rafiki kwa jamii,” alisema Dk. Gwamaka.

Alisema mazingira yakiwa mazuri na salama, yatavutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nje ya nchi na mapato yataongezeka kutokana na kodi na hata kuchagiza fursa za ajira kwa vijana nchini.

“Natoa rai kwa halmashauri zetu kutambua kwamba hawa wawekezaji wanaangalia vitu vingi, ikiwemo na mazingira ya eneo la kuwekeza, hivyo ni jukumu letu kushirikiana kwa pamoja kuweka maeneo yetu safi ili tuwavutie wawekezaji kuwekeza katika maeneo yetu,” alisema Dk. Gwamaka.

Alisema sasa ni wakati wa halmashauri kutambua fursa zilizomo kwenye taka.

Dk. Gwamaka alisema kuwa  taka zikichambuliwa vyema, zinapata soko viwandani na kutoa mfano wa plastiki na chuma chakavu kwamba hufanyiwa urejezwaji na kutumika kutengenezea bidhaa mpya.

“Tuache kuishi kimazoea. Halmashauri zetu zote ziwaongoze wananchi, na hasa vijana, wachangamkie fursa kwani taka kama vile chuma chakavu na plastiki ni aina ya taka zinazohitajika sana viwandani,” alisema Dk. Gwamaka.

Alitolea  mfano Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwamba imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na NEMC katika kutatua changamoto na matatizo ambayo yamekuwa yakiibuka mara kwa mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles