26.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 9, 2022

Contact us: [email protected]

NEMC: Elimu imethibiti magonjwa ya mlipuko

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeeleza kuwa kupungua kwa kasi ya magonjwa ya mlipuko hususani kipindupindu hapa nchini kumetokana na usimamiaji mzuri wa sheria na kanuni za mazingira na utoaji wa elimu hasa katika kipindi cha awamu ya tano.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, aliwapongeza Watanzania kwa  kuweka mazingira safi na salama kwa hiyari.

“Tabia ya kuchukia uchafu na kutunza mazingira ambayo imejengeka katika jamii yetu ni jambo zuri sana. Kuheshimu sheria ya mazingira na kanuni zake kwa hiari ni kitu muhimu katika kulinda na kutunza mazingira, kulinda afya za watu na viumbe wengine.

 “NEMC katika kipindi cha miaka mitano tumetoa elimu kupitia vyombo vya habari na kuandaa mikutano mbalimbali ya wadau wa mazingira na wananchi kwa ujumla wake. Tumepata mafanikio makubwa kwani takwimu zinaonesha magonjwa ya milipuko kama kipindupindu kasi ya kuenea kwake imepungua sana, sikumbuki kama tumekumbana na kipundupindu miaka mitano iliyopita,’’ alikiambia kikundi cha watu alichokikuta kinasafisha eneo lao kwa hiyari.

Dk. Gwamaka aliongeza kwamba chanzo kikubwa cha magonjwa ya milipuko nchini ni utiririshaji wa maji taka katika maeneo ya makazi ya watu pamoja na maji ya kemikali zenye sumu kutoka viwandani ambayo huelekezwa katika mito na makazi ya watu.

“Kwa kiasi kikubwa kipindupindu husababishwa na uchafu ambao huzalishwa majumbani, tumekuwa na utaratibu mzuri wa kudhibiti maji taka katika makazi ya watu lakini pia tumeweza kukutana na wenye viwanda na kuwapa elimu juu ya kudhibiti mifumo ya utiririshaji maji yenye kemilkali zenye sumu kutoka kwenye viwanda,’’ alieleza Dk. Gwamaka.

Dk. Gwamaka, mbali ya kuwashukuru viongozi wa kitaifa, alishukuru taasisi zote za elimu, Wizara ya  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa namna walivyoshirikiana na Baraza hilo kwa mafanikio.

“Mafanikio yaliyopatikana yametokana na ushirikiano tuliopata kutoka Serikali Kuu mpaka Tamisemi, TMDA, Taasisi zote za elimu, Shirika la Viwango (TBS) pamoja na wananchi kwa ujumla. Tutaendelea kusimamia kanuni na sheria za mazingira ili ziwaletee tija Watanzania,’’ alisema.

Alisema kutokana na mwitiko chanya wa wananchi, NEMC imeunda kikosi kazi cha dharura ambacho kinafanya kazi kwa saa 24 ambapo kazi yake ni kuhakikisha changamoto za kimazingira zinashughulikiwa kwa wakati.

“Mafanikio haya hayawezi kusemwa vizuri kama hatutaweza kutambua mchango wa wananchi ambao wamekuwa wakitoa taarifa za mara kwa mara juu ya uharibifu wa mazingira unaotokea katika maeneo mbalimbali jambo ambalo lilitulazimu kuunda kikosi kazi cha dharura ambacho kinafanya kazi kwa saa 24,’’ alieleza.

Licha ya mafanikio yaliyopatikana, Dk. Gwamaka aliwaonya baadhi ya wenye viwanda na wananchi wanaoendelea kutitirisha maji machafu kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa NEMC wapo imara na wanapokea taarifa zote muhimu kutoka kwa wananchi wema na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria watakapobainika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,735FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles