BARAZA la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), limevitaka vikundi vya kijamii vilivyo katika mifumo isiyo rasmi kujisajili katika mamlaka za Serikali za Mitaa ili viweze kutambuliwa na kupata fursa mbalimbali.
Hayo yalisemwa na Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na vikundi vinavyotakiwa kuanza kujisajili kwa ajili ya kutambuliwa na kunufaika na fursa zinazolenga kutolewa na Serikali na taasisi mbalimbali.
“Tunapenda kuona vikundi vikijisajili kwenye Serikali za Mitaa ili kuweza kupata mafunzo na mikopo kwa riba nafuu,” alisema wakati wa kufungua mkutano wa wadau wa kujadili mwongozo wa uwezeshaji wa upatikanaji wa taarifa za asasi na vikundi vya kifedha.
Alisema Serikali itasaidia kutoa mafunzo kwa vikundi hivyo pale itakapohitajika na kudhamini benki kutoa mikopo kwa vikundi vya kijamii vinavyojishughulisha na masuala ya kijasiriamali.
Alivitaja vikundi hivyo kuwa ni pamoja na vile vinavyonunua hisa, kuweka akiba na vikipata faida vinagawana au kukopeshana au kujiingiza katika shughuli za kibiashara kupitia akiba wanayoweka.
Beng’i, alisema kwa muda mrefu pamekuwa na ugumu kuwa na taarifa na takwimu za vikundi na ukubwa wa mifumo hiyo nchini, lakini kupitia mfumo huo mpya wataweza kupata na kupanga mipango ya kuviwezesha.
Alisema Serikali iliunda kikosi kazi kilichojumuisha wajumbe toka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, halmashauri za wilaya, taasisi zinazojihusisha na usimamizi wa vikundi vya kifedha vikiwemo Vicoba na kuja na mwongozo ambao wadau wanaujadili ili kufikia malengo yanayokusudiwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro Vicoba Network (KIVINET), Mathia Mwingira, alisema asasi yake inahudumia vikundi 348 katika mkoa huo vilivyosambaa katika vijiji mbalimbali katika wilaya zote.
“Tunafanya kazi ya kuvisaidia vikundi hivi kupata elimu ya kijasiriamali, sasa vinatakiwa kwenda mbali zaidi ili visajiliwe na kupata mikopo,” alisema Mwingira.
Alisema vikundi vyote ambavyo havina wasimamizi vinatakiwa kujiunga ili viweze kunufaika na fursa mbalimbali zikiwemo za mafunzo.