ELIUD NGONDO, MBEYA
KAMATI za mitihani zimetakiwa kuhakikisha taratibu zote za uendeshaji wa upimaji wa mitihani ya kitaifa kwa wanafunzi wa darasa la nne na kidato cha pili zinazingatiwa ipasavyo ili kuondoa udanganyifu wowote.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Dk.Charles Msonde mkoani Mbeya jana, alipozungumza na waandashi wa habari na kuwaasa wasimamizi wa upimaji, wamiliki wa shule,walimu na wananchi kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu.
Dk.Msonde alisema Novemba leo na kesho kutakuwapo na upimaji wa kitaifa kwa wanafunzi wa kidato cha pili na sekondari 4,796 zitakuwa, Novemba 20 hadi 21 kutakuwa na upimaji wa wanafunzi wa darasa la nne ambapo shule 17,483 za msingi zitafanya mtihani huo.
Alisema kamati zihakikishe mazingira ya vituo vya upimaji yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu wa mitihani hiyo na kupelekea wanafunzi kufutiwa matokeo yao baada ya kufanya mitihani.
Alisema kamati zihakikishe usalama wa vituo teule unaimarishwa na vituo vitumike kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na baraza la mitihani la Tanzania.
“Baraza linatoa wito kwa wasimamizi wote kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu na wasimamizi wanaelekezwa kufanya kazi yao kwa weledi na kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa,” alisema.
Alisema wasimamizi wahakikishe wanalinda haki za watahiniwa wenye mahitaji maalumu ambazo ni kuwapatia mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokolezwa kwa watahiniwa wenye uono hafifu.
Alisema watahiniwa wote wenye mahitaji maalumu waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa masomo ya Hisabati na dakika 10 kwa kwa masomo mengine kama mwongozo wa baraza unavyoelekeza.
Alisema baraza linaamina walimu wamewaandaa vizuri wanafunzi kipindi chote cha miaka miwili kwa elimu ya sekondari na miaka mine kwa wanafunzi wa shule za msingi.
“Matarajio ya Baraza la Mitihani, ni wanafunzi watafanya upimaji huo kwa kuzingatia kanuni za upimaji ili matokeo yaoneshe uwezo wao halisi kulingana na maarifa na ujuzi waliopata kutoka kwa walimu.
“Baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa upimaji wa taifa, pia jamii inatakiwa kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha upimaji wa kidato cha pili na darasa la darasa nne unafanyika kwa amani na utulivu,” alisema Dk. Msonde.