Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limefuta matokeo ya watahiniwa 67 waliohusika na udanganyifu katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2024.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Januari 25, 2025, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, alisema miongoni mwa watahiniwa hao, watano waliandika lugha ya matusi kwenye karatasi za mtihani.
“Matokeo haya yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na kifungu cha 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016,” alisema Dk. Mohamed.
Aidha, NECTA imezuia kutangaza matokeo ya watahiniwa 459 waliokumbwa na matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya baadhi au masomo yote ya mtihani huo. Watahiniwa hao watafanya mtihani wa masomo waliyokosa mwaka 2025 kwa mujibu wa kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani.
Katika hatua nyingine, NECTA imekifungia kituo cha P6384 BSL Open School kilichopo mkoani Shinyanga kutokana na kuendesha mipango ya udanganyifu. “Kituo hiki kimefungwa kwa mujibu wa kifungu 4(8) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016 hadi hapo Baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani ya Taifa,” aliongeza Dk. Mohamed.
Ufaulu Waongezeka kwa 5.54%
Dk. Mohamed alieleza kuwa, jumla ya watahiniwa 221,953 walipata madaraja ya ufaulu I-III, sawa na asilimia 42.96 ya watahiniwa wote. Ufaulu huu umeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo asilimia 37.42 ya watahiniwa walipata madaraja hayo.
Aidha, alibainisha kuwa wavulana walifanya vizuri zaidi ikilinganishwa na wasichana, ambapo wavulana 119,869 walipata madaraja I-III sawa na asilimia 48.90 ya wavulana wote, huku wasichana 102,084 wakipata madaraja hayo sawa na asilimia 37.59 ya wasichana wote.
Takwimu za Jumla za Mtihani
Dk. Mohamed alisema watahiniwa 557,796 walisajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasichana 296,051 (asilimia 53.08) na wavulana 261,745 (asilimia 46.92). Kati yao, watahiniwa wa shule walikuwa 529,329, huku watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 28,467.
Matokeo haya yanaashiria maboresho katika mfumo wa elimu, lakini pia yanaibua changamoto za maadili na nidhamu zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka.