33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Necta yawafutia matokeo wanafunzi kwa kuandika matusi

SARAH MOSES-DODOMA

BARAZA la Taifa la Mitihani (Necta), limetangaza matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la nne na kidato cha pili iliyofanyika kuanzia Novemba 23, mwaka jana na limewafutia matokeo wanafunzi tisa baada ya kuandika matusi.

Akizungumza jijini hapa jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema ufaulu wa watahiniwa umeongezeka kulinganisha na mwaka juzi.

Pia alisema katika matokeo hayo hakuna shule ya Serikali iliyojitokeza katika shule 10 bora zilizofanya vizuri.

Huku katika matokeo ya kidato cha pili, jumla ya wanafunzi 47 walifutiwa matokeo yao yote kutokana na udanganyifu, kati yao tisa kutokana na kuandika matusi katika karatasi zao za majibu.

“Kwa hawa wanafunzi tisa walioandika matusi kwenye skripti zao tumeziagiza bodi za shule wanakotoka wawachukulie hatua za kinidhamu ili tukio hilo lisijirudie tena kwa sababu bodi za shule ndizo zenye mamlaka ya kutoa adhabu kwa wanafunzi,” alisema Msonde.

Pia alisema limewafutia matokeo kwa mujibu wa kifungu cha 17(1) kinachokataza mwanafunzi kuandika matusi katika karatasi yake ya majibu.

Alisema jumla ya watahiniwa 506,235 wa kidato cha pili walisajiliwa kufanya mtihani sawa na asilimia 92.87 huku wanafunzi 38,842 sawa na asilimia 7.13 hawakufanya mtihani kutokana na ugonjwa na utoro.

Alisema matokeo ya mtihani huo yanaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 452,273 sawa na asilimia 89.68 wamepata alama za ufaulu zitakazowawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu huku 52,073 sawa na asilimia 10.32 wameshindwa kupata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.

“Mwaka 2017 wanafunzi 433,453 sawa na asilimia 89.32 walipata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, hivyo ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.36,” alisema.

Alizitaja shule kumi zilizofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha pili kuwa ni St Francis Girls ya Mbeya, Thomas More Machrina ya Dar es Salaam, Bright Future Girls ya Dar es Salaam, St. Monica Moshono Girls ya Arusha, Bethel Sabs Girls ya Iringa, Centennial ya Pwani, St. Augustine-Tagaste ya Dar es Salaam, Anwarite Girls ya Kilimanjaro, St. Mary’s Ulete ya Iringa na St. Aloysius Girls ya Pwani.

Huku shule 10 za mwisho kitaifa kuwa ni Ocean ya Mtwara, Mdando ya Tanga, Kwashemshi ya Tanga, Miteja ya Lindi, Thaqalain ya Dar es Salaam, Korona ya Arusha, Imbafi ya Dodoma, Magindu ya Pwani, Mashindei ya Tanga na Luagala ya Mtwara.

Katika matokeo ya darasa la nne, alisema kati ya watahiniwa 1,302,461 sawa na asilimia 95.58 waliofanya mtihani huo na kufaulu kwa kupata daraja A, B, C, na D ni 1,213,132 sawa na asilimia 93.16 huku 89,093 sawa na asilimia 6.84 wamepata daraja E lenye ufaulu usioridhisha.

“Hata hivyo, jumla ya watahiniwa 151 wamefutiwa matokeo yao yote baada ya kubainika kufanya udanganyifu katika upimaji wa kitaifa kwa mujibu wa kifungu 32 (2) (b) cha kanuni za mitihani.

“Baraza limezishauri mamlaka zinazohusika kuwachukulia hatua wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kusababisha kutokea kwa udanganyifu katika upimaji wa darasa la nne kwa mujibu wa kanuni za utumishi na sheria za nchi,” alisema.

Pia alisema ufaulu umeongezeka kulinganisha na mwaka 2017 kwa kuwa matokeo ya jumla ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kwa mwaka 2018, yanaonyesha wanafunzi wamefanya vizuri kutokana na takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa ufaulu wa watahiniwa kwa masomo yote uko juu ya wastani.

Pia alisema ubora wa ufaulu umezidi kuimarika kwa kuwa watahiniwa waliofaulu kwa daraja la A, B, na C wameongezeka kwa asilimia 0.03 ukilinganisha na mwaka 2017.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles