33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Necta, TCU mguu sawa

 FARAJA MASINDE Na TUNU NASSORO– DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ametangaza wanafunzi wa vyuo vyote nchini na kidato cha sita, watarudi darasani Juni mosi huku Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), likieleza lilivyojipanga kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha sita wanafanya mtihani bila shida.

Machi 17, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kufungwa kwa shule, vyuo, kusitisha warsha mbalimbali na michezo ikiwa ni njia ya kudhibiti maambukizi ya corona.

Jana Rais Magufuli mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Dodoma, alitangaza kufungua vyuo na kidato cha sita na kusema hali ikionekana kuwa sawa hatua nyingine za kufungua shule na shughuli nyingine zitaendelea.

Rais Magufuli alizitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya Fedha na Mipango kuhakikisha zinafanya maandalizi ili pale vyuo vitakapofunguliwa kusiwe na kero kwa wanafunzi.

“Sasa kutokana na hii hali kwamba inaenda vizuri na waziri amezungumza hapa, tumeamua vyuo vyote vifunguliwe Juni mosi, mwaka huu.

“Kwa hiyo niwaombe wizara zinazohusika, hasa ile Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya Fedha na Mipango ambayo inahusika sana katika kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi, leo (jana) tuna siku tisa, hivyo zijiandae ili hivi vyuo vitakapofunguliwa pasije tena pakawa na kero nyingine, ili kama mwanafunzi anastahili kupata mkopo wake uwe umeshaandaliwa mapema.

“Sababu kwa wizara ambayo iko makini haiwezi ikashindwa kumaliza haya na kufanya maandalizi na ndiyo maana nimetangaza mapema kwamba walau siku tisa hizi zitatusaidia kujipanga vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, mbali na wanafunzi hao wa elimu ya juu, Rais Magufuli pia alitangaza kuanza masomo kwa wanafunzi wa kidato cha sita ili kutokuathiri ratiba ya kujiunga na Chuo Kikuu.

“Lakini mbali ya vyuo hivyo, vijana waliokuwa kidato cha sita nao watarudi kwenye shule zao Juni mosi, mwaka huu na Wizara ya Elimu ipange mikakati yao ili vijana hawa wafanye mtihani wao wa kidato cha sita bila kuharibu utaratibu wao wa kuingia chuo kikuu kama ilivyokuwa imepangwa, ugonjwa wa corona usiwacheleweshe vijana hawa.

“Kwa zile shule zingine za sekondari na za msingi tujipe muda kidogo, tuangalie awamu hii ya vyuo kwa sababu wanachuo ni watu wanaojitambua, ni watu wazima tofauti na mtoto mdogo wa darasa la kwanza, tujipe muda tutaona hali inavyoenda na wao baadaye tutawapa nafasi kadiri tutakavyokuwa tunaendelea kupambana na ugonjwa huu wa corona,” alisema Rais Magufuli.

BARAZA LA MITIHANI

Akizungumzia maelekezo hayo yaliyotolewa na Rais Magufuli, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk. Charles Msonde, alisema wao walishajipanga muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuratibu mafunzo kwa njia ya vyombo vya habari, uamuzi aliosema kuwa umekuwa na mashiko.

“Sisi tulishajipanga siku nyingi, si unaona watoto wanaendelea na kusoma kwa njia ya televisheni wakiwa nyumbani? Hivyo sisi tulishajipanga na tunamshukuru Rais kwa uamuzi huo na hata wadau wamefurahi sana.

“Lakini ukweli ni kwamba mpango huu wa kusoma kwa njia ya tv ilikuwa ni fursa nzuri kwani tumekuwa na mrejesho mzuri kutoka kwa wanafunzi ambao wamekuwa wakitupongeza kila kukicha wakiwamo wazazi, hivyo kama Baraza tuko tayari muda mrefu,” alisema Dk. Msonde.

Katika hatua nyingine, Dk. Msonde alisema kuwa watatangaza rasmi tarehe ya kuanza kwa mitihani ya kidato cha sita baadaye mwaka huu.

BODI YA MIKOPO

Nayo Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu nchini (HESLB) ilisema tayari imenza kufanya malipo kwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema tayari wameanza kuwaingizia fedha za mikopo wanufaika hao na kwamba hadi kufikia Mei 28, watakuwa wamekamilisha.

“Tumeanza kufanya malipo yenye Sh bilioni 63.7 ikiwa ni fedha za chakula na malazi kwa ajili ya robo ya tatu ya mwaka wa masomo 2019/2020 na fedha hizo zitawafikia wanufaika wote kupitia vyuo vyao ifikapo Alhamisi, Mei 28, mwaka huu.

“Hatua hii ya kuanza kufanya malipo inafuatia maelekezo ya kufunguliwa kwa Taasisi za Elimu ya Juu ifikapo Juni mosi, mwaka huu ambayo yametolewa leo (jana) na Rais, jijini Dodoma. 

Serikali ilifunga vyuo Machi 16, kama sehemu ya jitihada za kupambana na maambukizo ya virusi vya corona na ugonjwa wa Covid-19,” alisema Badru.

Aidha, alifafanua zaidi kuwa kwa utaratibu uliopo, fedha za chakula na malazi hulipwa kwa mwanafunzi mnufaika mara nne katika kila mwaka wa masomo, yaani kila baada ya siku 60 za masomo ambazo mwanafunzi anapaswa kuwepo chuoni.

“Hadi wakati vyuo vinafungwa, wanafunzi wanufaika walikuwa wameshalipwa malipo ya robo ya kwanza ambayo yalilipwa Novemba, 2019 na robo ya pili yaliyolipwa mwezi Januari.

“Wakati huohuo, pamoja na malipo ya fedha za chakula na malazi kwa wanafunzi, bodi pia inakamilisha malipo yenye thamani ya Sh bilioni 59.1 ya ada za wanafunzi wanufaika ambayo yatalipwa kwa taasisi zaidi ya 70 za elimu ya juu zilizopo nchini,” alisema Badru. 

Alisema malipo ya ada hulipwa vyuoni mara mbili kwa mwaka, yaani mwanzoni mwa muhula wa mwaka wa masomo mara baada ya bodi hiyo kupokea uthibitisho wa usajili wa wanafunzi vyuoni na mwanzoni mwa muhula wa pili, mwezi Machi.

“Lengo la malipo haya ni kuziwezesha taasisi za elimu kumudu gharama za uendeshaji na hivyo kutoa elimu inayokusudiwa kwa wanafunzi wanaosoma katika taasisi zao, malipo ya ada yatakuwa yamevifikia vyuo vyote vilivyowasilisha hati za madai HESLB ifikapo Ijumaa, Mei 29.

“Katika mwaka wa masomo 2019/2020, Serikali inatoa mikopo ya elimu ya juu yenye jumla ya thamani ya Sh bilioni 450 kwa wanufaika 132,119 wanasoma katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu hapa nchini. 

“Fedha hizi zinagharamia vipengele sita ambavyo ni chakula na malazi; ada; vitabu na viandikwa; utafiti; mafunzo kwa vitendo na mahitaji maalum kwa baadhi ya vitivo,” alisema Badru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles