24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

NEC yatangaza uchaguzi kwa Lissu, Chadema wahoji kampeni kufanyika siku 12

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza uchaguzi mdogo katika Jimbo la Singida Mashariki, utakaofanyika Julai 31, kujana nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya wiki iliyopita Spika wa Bunge, Job Ndugai kutangaza kumvua ubunge Lissu kwa kile alichodai hajajaza fomu ya mali na madeni na hajatoa taarifa za wapi alipo hivyo anahesabika kama mtoro bungeni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na NEC jana, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Semistocles Kaijage alizingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343 kwa kutangaza uchaguzi katika jimbo hilo.

Taarifa hiyo ilisema Jaji Kaijage alitoa ratiba hiyo kutokana na barua ya Spika Ndugai inayoeleza kuwa Lissu kapoteza sifa za ubunge.

“Lissu kapoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kushindwa kuwasilisha kwa Spika tamko la mali na madeni na kushindwa kuhudhuria mikutano saba mfululizo ya Bunge bila ruhusa ya Spika.

“Tumezingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, kutoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa Uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki,”ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema kuwa kwa kuzingatia Katiba na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, ratiba ya uchaguzi huo mdogo, fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya Julai 13 hadi 18.

“Uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 18 na kampeni za uchaguzi, zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30 na uchaguzi utafanyika Julai 31,”ilisema.

Aidha kupitia taarifa hiyo, Jaji Kaijage alivikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na NEC wakati wa uchaguzi huo. 

Wakati NEC wakitoa taarifa hiyo, Katibu Mwenezi wa Chama cha ACT-Wazalendo ,Ado Shaibu, amesema hawatashiriki uchaguzi huo kwa kuwa kilichofanyika ni uharamia.

Akizungumza na MTANZANIA jana alisema msimamo wao upo pale pale na wanaunga mkono Chadema kwamba hawawezi kushiriki kwa kile alichokiita kilochofanyika ni uhuni.

“Sisi tumeshasema tangu awali kuwa hatushiriki uchaguzi huo kwakuwa kilichofanyika ni uhuni hivyo tunaungana na Chadema kwa hatua watakazozichukua juu ya suala hilo, “alisema Addo.

Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), msemaje wake Tumaini Makene aliliambia MTANZANIA alihoji ni wapi kampeni za kuchagua mbunge ikafanyika kwa siku 12.

“NEC wametangaza kampeni zinaanza Julai 19 hadi 30, hizo ni siku 12. Ulishawahi kuona wapi kampeni za ubunge zinafanyika kwa siku 12? Hapo ni wazi wameshapanga kila kitu kama wanavyotaka wao…huo ni uchaguzi wa kitongoji au ubunge,”alihoji Makene.

Kuhusu endapo watashiriki uchaguzi huo, alisema kushiriki uchaguzi huo ni kama kuhalalisha kilichofanyika cha kumvua ubunge Lissu, hivyo hawatashiriki.

Akizungumzia rufaa ya ubunge wa Lissu, Makene alisema bado wako kwenye mchakato wa kwenda kupinga uamuzi huo wa Spika mahakamani.

Lissu amekuwa nje ya nchi baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017 na tangu siku hiyo amekuwa nje ya nchi kwa matibabu yaliyotanguliwa na yale aliyoyapata katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na baadaye Hospitali ya Nairobi Kenya na sasa yuko nchini Ubelgiji.

Juni 28, Spika Ndugai alitangaza bungeni kwamba Lissu amepoteza sifa za kuwa mbunge, hatua iliyomuibua Lissu akisema ataenda mahakamani kutafuta haki jambo ambalo hadi sasa hajalifanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles