NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza kusogeza mbele uandikishaji wapigakura kutoka Februari 16 hadi 23, mwaka huu.
Uamuzi huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, katika kikao na viongozi wa vyama vya siasa hali ambayo iliibua hoja nzito.
Jaji Lubuva, alisema wamesogeza mbele uandikishaji ili wapate muda wa kufanya maandalizi ya kutosha, na vyama viweze kuandaa mawakala pindi kazi hiyo itakapoanza.
Hatua hiyo ilipingwa na viongozi wa vyama vya siasa, hasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao kwa pamoja walitaka kupata maelezo ya kina kuhusu uamuzi huo.
MBOWE
Akichangia kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema kusogezwa mbele kwa muda wa uandikishaji hakutokani na kuvisaidia vyama vya siasa kuweka mawakala.
“Jambo la kuweka mawakala kwa vyama vya siasa ni la kisheria kwa kuwa kila chama kinahitajika kupeleka majina siku saba kabla ya zoezi hilo kuanza, na wala hamtuelezi ukweli kama vifaa vimefika au bado, kwa taarifa tulizopata mnasogeza mbele ili kusubiri vifaa ambavyo havijafika viweze kufika,” alisema.
Alisema pamoja na NEC kupitia mwenyekiti wake Jaji Lubuva kutangaza mabadiliko hayo ya tarehe ya kuanza kwa uandikishaji Mkoa wa Njombe, lakini imeshindwa kueleza muda wa kumalizika.
“Tuna wajibu wa kujiandaa, sasa tunawezaje kujipanga katika jambo kama hili? Na kwanini tume inaendelea kuweka usiri? Hilo linachangia baadhi ya watu kuhusisha tume hii na kulinda Serikali,” alisema.
Akizungumzia suala la utoaji wa elimu kwa wanasiasa kuhusu mashine za BVR, Mbowe alisema hadi sasa hakuna elimu iliyotolewa hali inayosababisha kuwapo na hali ya kutoiamini tume.
“Tunaingia katika utumiaji wa teknolojia mpya ya matumizi ya mashine za uandikishaji wa kielektroniki ya BVR, lakini hatujui ni ‘system’ gani, ‘hardware’ au ‘software’ gani inatumika. Hata mkituita wanasiasa wote tukae hapa siku nne, hatutaelewa matumizi ya BVR,” alisema.
“Hatuoni tatizo lolote kujua nani anasambaza vifaa, haya mambo tume wekeni wazi, ni shirika au kampuni gani inatuletea ‘software’, akina nani wanahusika. Haya mambo yakiwa wazi itatusaidia sisi,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa Chadema, alihitimisha kwa kutaka kujua msimamo wa NEC kama bado ina mpango wa kutumia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), katika uandikishaji.
NAPE
Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, ametoa wito kwa NEC kuacha kutoa majibu mepesi kwenye maswali mazito hali anayoielezea kwamba inachangia wadau wengine kukihusisha chama chake na kadhia hiyo.
“Wadau ambao wapo katika orodha ya kuchukua lawama kama mambo yakienda ndivyo sivyo, sisi CCM ndio tunaohusishwa, na ndiyo maana huwa napiga kelele, na katika jambo hili ili mambo yaende sawa, lazima kuwapo na kuaminiana, na ili kuwapo na kuaminiana, lazima uwazi upewe nafasi,” alisema Nape.
Aliwatupia lawama NEC kukaa kimya pindi wadau wanapokuwa wanaonyesha hisia za wasiwasi kuhusu mambo makubwa ya teknolojia ya BVR.
“Nashangaa wakati hayo yanapotokea, tume imekuwa ikikaa kimya na badala yake Waziri Mkuu ambaye si msemaji wa tume ndiye anajitokeza kusema, hivyo tume tengenezeni utaratibu wa kutolea ufafanuzi kabla ya kusambaa kwa jambo na kuwa kubwa,” alisema.
Alisema NEC wanatakiwa kutolea ufafanuzi masuala makubwa pindi yanapoanza kwa uhakika wa ndani zaidi, kama ambavyo wadau wanavyokuwa wanaulizana kwa vielelezo sahihi.
“Kunapokuwa na malalamiko, mwenyekiti mnatakiwa kujipanga kwa kutoa majibu yanayokidhi na yanayolingana na kiwango cha swali husika. Swali ‘Centigrade 200, majibu ‘Centigrade’ 50 lazima mlalamikiwe, na mnapojibu vizuri hata sisi mnatuweka mahali pazuri,” alisema.
LIPUMBA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema anashangaa kuona vituo vya kupigia kura vimepungua kutoka 40,000 hadi kufikia 36,000 vya sasa.
Pia alitaka kujua kama Aprili 30 ndiyo siku ambayo imeridhiwa na NEC, kwa sababu siku hiyo ilitangazwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye hatambuliwi na sheria kufanya hivyo.
MBATIA
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema tatizo linaloikabili NEC ni ukosefu wa fedha ambapo ilitarajiwa kupewa zaidi ya Sh bilioni 900 ambazo hadi sasa serikali haijatoa.
Kutokana na ukosefu huo wa fedha, kumechangia hadi sasa kuwapo kwa vifaa vinavyofikia 250 wakati ambavyo havijafika ni 7,750.
Akihitimisha hoja hizo, Jaji Lubuva, alisema masuala yote yanatarajiwa kukamilika kwa daftari la kura ya maoni kwa sababu bila ya hilo hakuna kinachoweza kuendelea.
Alisema daftari hilo litasaidia kutoa mustakabali wa masuala mengine ambayo ni kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu.