24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NEC yapuliza kipenga jimbo la Nassari 

Na MWANDISHI WETU   –  DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza Mei 19 mwaka huu kuwa ni tarehe ya kufanyika uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arumeru Mashariki.

Akizungumza   mkoani Morogoro jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, alisema tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha sheria ya taifa ya uchaguzi aliiarifu tume kuwapo   nafasi wazi ya ubunge katika jimbo hilo.

“Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi na imetokana na aliyekuwa mbunge wake, Joshua Nassari kupoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo bila ruhusa ya Spika.

“Kwa kuzingatia masharti ya vifungu vya 37 na 46 vya Sheria ya Uchaguzi tume inauarifu umma kuhusu ratiba ya uchaguzi wa jimbo hilo, kampeni za uchaguzi zitafanyika kati ya Aprili 29 hadi Mei 18, 2019 na siku ya uchaguzi itakuwa ni Mei 19,”alisema Jaji Kaijage.

Alisema fomu za wagombea zitatolewa kati ya Aprili 15 au 19 na uteuzi wa wagombea utafanyika Aprili 19, mwaka huu.

Jaji Kaijage alivitaka vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo ya uchaguzi wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo.

Taarifa hiyo ya kufanyika kwa uchaguzi wa Jimbo la Arumeru Mashariki,  inatokana na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, kukubaliana na uamuzi wa Spika Ndugai kutangaza kuwa Joshua Nassari amepoteza sifa za kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Nassari alivuliwa ubunge na Spika Ndugai Machi 14 mwaka huu kwa kilichodaiwa kuwa ni kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu mfululizo bila taarifa rasmi.

Kwa mujibu wa Spika Ndugai, mikutano mitatu ambayo Nassari hakuhudhuria ni pamoja na Mkutano wa 12 wa Septemba 4-14 mwaka jana, Mkutano 13 wa Novemba 6-16 mwaka jana na Mkutano wa 14 wa Januari 29- Februari 9 mwaka huu.

Alipoulizwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu endapo chama chao kitashiriki katika uchaguzi huo wa Arumeru Mashariki, alisema msimamo wao wa kutoshiriki uko pale pale mpaka   Nassari atakaporudishiwa haki yake.

“Mahakama ilitoa hukumu juzi Ijumaa lakini leo (jana) Jumapili tume ilikuwa na haraka gani kutangaza kama siyo nia ovu? Hii haraka ni ya nini kwani kuna dharura gani mpaka atangaze siku ambayo siyo ya kazi?

“Kwa sasa tunaendelea na dhamira ya kukata rufaa  haki iweze kutendeka,”alisema Mwalimu. 

Wakati Mwalimu akiyasema hayo, juzi Kamati Kuu ya Chadema ilikutana   Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine   ilijadili suala la hatima ya ubunge wa Nassari.

Kikao hicho maalumu cha siku moja chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kilijadili ubunge wa Nassari ikiwa ni siku mbili tu baada ya Mahakama Kuu ya Kanda ya Dodoma kukubaliana na uamuzi huo wa Spika Ndugai.

Pamoja na uamuzi huo wa Mahakama, Nassari alisema atakata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema chama chao kitakaa na kutafakari kama kitashiriki au la.

“Chama kitakaa na kutafakari na tutawapa mrejesho.  Kwa sasa sina comment,”alisema Shaibu.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema atakutana na viongozi wenzake wa chama kujadili kuhusu ushiriki wao katika uchaguzi huo.

“Kwa sasa nipo jimboni, ngoja niwasiliane na wenzangu  tujadiliane kuhusu ushiriki wetu halafu tutawajulisha,” alisema Sakaya.

Machi 14, mwaka huu aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), alivuliwa ubunge kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo, huku mwenyewe akisema alipokea taarifa hiyo akiwa kwenye kazi za ubunge mkoani Kilimanjaro na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Kuvuliwa ubunge wa Nassari kunafanya Chadema kupoteza wabunge wanane tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kati yao saba walijiuzulu uanachama wa chama hicho na baadaye kuteuliwa tena kuwania nafasi zao kupitia CCM.

  Spika wa wa Bunge, Job Ndugai, alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, kumuarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki liko wazi.

Taarifa hiyo ilieleza sababu za Nassari kuvuliwa ubunge kuwa ni kutohudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo.

Taarifa hiyo ilitaja mikutano hiyo kuwa ni mkutano wa 12  wa Septemba 4 hadi 14, 2018), mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16, 2018 na ule wa 14 wa Januari 29 hadi Februari 9 mwaka huu.

“Uamuzi huo wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1) (c). Ibara hiyo inaeleza kuwa ‘Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

“Ibara hiyo pia imefafanuliwa katika kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016 kuwa ‘kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge, mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Arumeru Mashariki,” ilieleza taarifa hiyo ya Spika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles