26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

NEC yamwita Lissu kujieleza

 MWANDISHI WETU

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema imemuandikia barua mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ya kumuita katika kikao cha Kamati ya Maadili ya Taifa, huku ikitoa onyo kwa wagombea wengine.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Charles Mahera alisema hayo jijini Arusha wakati akizungumza na waandishi wa habari jana, ambapo alieleza kuwa mgombea huyo ametakiwa kufika mbele ya kamati Septemba 29 mwaka huu kujieleza kuhusu kutoa taarifa alizodai kuwa si za kweli, zenye lengo la kuleta taharuki na uzushi miongoni mwa Watanzania.

“Katika taratibu za kusimamia uchaguzi, Tume inasikitishwa na taarifa za uongo, uzushi na upotoshaji zilizotolewa na Tundu Lissu jana (juzi) Septemba 26 huko Musoma akisema kuwa Dk John Magufuli, mgombea urais wa tiketi ya CCM juzi (Ijumaa) Septemba 25 na jana Septemba 26 alikuwa ameitisha kikao kukutana na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote nchi nzima mjini Dodoma kwa lengo la kupanga mikakati ya kuhujumu uchaguzi.

“Lakini pia Septemba 25 (Ijumaa) kuna taarifa zilizosambaa mitandaoni zikisema Rais Magufuli alifanya kikao na Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni mimi na wasimamizi wa uchaguzi mjini Dodoma. “Ndugu wananchi, Watanzania wapenda amani, taarifa mbili hizi ni za uongo, uzushi na zenye kuleta taharuki miongoni mwa Watanzania na wapiga kura na kujenga picha kuwa uchaguzi huu hautakuwa huru na wa haki na kwamba hata wakishindwa kihalali basi watawataka Watanzania wawaunge mkono kuvuruga amani ya nchi kwa lengo na agenda zao binafsi,” alisema.

Alisema Tume imemuita Lissu baada ya kujiridhdisha kuwa taarifa alizozitoa huko Musona juzi zina lengo baya kwa nchi, sualaa mbalo halikubaliki, hivyo kwa mamlaka ya Tume iliyo nayo tayari imeshamwandikia barua ya kumwita katika kikao cha Kamati ya Maadili ya Kitaifa ili akatoe maelezo na ushahidi wa kile alichokisema katika mkutano wake huko Musoma.

“Ninataka kuwahakikishieni kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi iko imara, haitatishwa na itatangaza matokeo ya halali na Watanzania wenyewe wanaona watakayekuwa wamemchagua na atakayekuwa ameshindwa lazima akubali, na asipokubali sheria nyingine zitafuata,” alisema.

Dk Mahera alisema Tume haitaki kutishwa na mtu ambaye tayari anajiona kama ameshashinda wakati siku ya uchaguzi bado, ambaye badala ya kutangaza sera anatangaza ameshashinda na kuitisha tume.

 “Tutatumia sheria, taratibu na kanuni kuhakikisha kwamba tunatangaza mshindi ambaye Watanzania watakuwa wamemtangaza na si vinginevyo. Si kwa mashinikizo ya watu wengine kutoka nchi nyingine,” alisisitiza. 

Dk Mahera alisema katika kusimamia na kuratibu kampeni za wagomeba na hasa wa urais Tume imekumbana na changamoto kutoka wka baadhi ya wagombea kiti cha rais za kutoheshimu sheria, taratibu na maadili ya uchaguzi ikiwemo baadhi ya wagombea kutumia maneno ya kukashifu wagombea wengine na kuikashifu tume yenyewe.

Alisema kuna baadhi ya wagombea katika kampeni zao tayari wanajiona wameshashinda na kuwaaminisha Watanzania kuwa wasipotangazwa basi waingie barabarani kuvunja amani, suala ambalo ni kosa kubwa la kuvunja amani ya nchi kwa sababu uchaguzi nchini unaongozwa kwa kufuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa Tanzania Sheria zile mbili za Uchaguzi na maelekezo na kaununi na maadili ya uchaguzi.

“Uchaguzi huu unasimamiwa na sheria za Tanzania, hausimamiwi na sheria za nchi za nje na lazima tufuate utamaduni tuliojiwekea. Na Watanzania ni watu walioelimika vya kutosha na ndiyo maana kuna hamasa kubwa ya watu kujitokeza kwenda kusikiliza sera.

“Tume inawasihi wagombea kutumia fursa hiyo vizuri kwa manufaa kuhakikisha kwamba wanaokwenda kusikiliza kampeni zao wanasikiliza sera na si kusikiliza matusi.

“Kitendo cha baadhi ya wagombea wa kiti cha urais hasa mgombea wa Chadema Tundu Lissu kuikashifu Tume kwamba itaiba kura zake ni kitendo cha kuidhalilisha tume na kutaka kuitisha ili isifanye kazizake kwa uhuru wakati tume kwa mujibu wa Ibara ya 74 Ibara ndogo ya 7, Ibara ya 11, Ibara ya 12 na Ibara ya 14 ni Tume huru inayofanya kazi bila kutishwa ma mtu yeyote, chama chochote na mgombea yeyote. 

“Hili halikubaliki na kamwe Tume haitatishwa, itaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni pamoja na Katiba ya nchi,” alisema Dk Mahera.

Alihoji kama Lissu anajiona tayari ameshashinda kwa nini anafanya kampeni? Kwa nini asikae kusubiri ili aje utangazwe? Huku akisisitiza kwamba wagombea wa aina hiyo wanapaswa kupuuzwa na Watanzania kwa kuwa hizo ni dalili za mgombea mwoga anayejihami au aliyekosa sera.

 Dk Mahera alieleza kuwa tangu Septemba 25 na 26 yeye binafsi kama Mkurugenzi wa NEC amekuwa katika ziara kukagua na kuratibu maandalizi ya uchaguzi katika majimbo ya mikoa ya Manyara, akiwa tayari ameshapita Kondoa vjijini, Babati Mjini, Jiji la Arusha, Siha, kisha Hai, Moshi Mjini na Moshi Vijijini na bado anaendelea na ziara zake kwa lengo la kuangalia maandalizi ya uchaguzi yanakwendaje. 

Alisema lengo la ziara hiyo ni kuangalia kama vifaa kwa ajili ya uchaguzi walivyovipeleka na kujua wiapo kuna changamoto zipi ili ifikapo siku ya uchaguzi, Oktoba 28 wawe kwenye mazingira mazuri ya kuhakikisha uchaguzi unakwenda vizuri na kote huko alikopita amekutana na wasimamizi wa uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles