29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

NEC yajikanganya

MwenyekitiJONAS MUSHI NA VICTORIA PATRICK, DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa taarifa yenye mkanganyiko kuhusu wapigakura ambao wanaruhusiwa kupiga kura na wale wasioruhusiwa kupiga kura; pamoja na kuruhusu watu wenye vitambulisho vyenye namba totauti na zile zilizo kwenye Daftari la Kupiga Kura.

Katika taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari iliainisha makundi ya watu ambao wanaweza kupiga kura licha ya kasoro kwenye mfumo wa Daftari la Wapiga Kura na wale
ambao hawataweza kupiga kura, hata kama wana vitambulisho vya kupigia kura.

Kipengele cha nne cha taarifa hiyo kinajikanganya na kile cha sita ambavyo vyote vinawataja watu wenye vitambulisho, lakini majina yao hayamo kwenye Daftari lakini kimoja (cha nne) kinaruhu watu hao kupiga
kura huku kingine (cha sita) kikiwakataza kufanya hivyo.

Katika taarifa hiyo, kipengele namba nne Lubuva alisema: “Wapiga kura ambao hawaonekani kwenye mfumo wa Daftari lakini wana vitambulisho vilivyotolewa na Tume na fomu zao za kuandikishwa kufikishwa Tume na majina yao kuandaliwa katika mfumo wa orodha bila picha na kupelekwa kituoni wataruhusiwa kupiga kura.”

Katika kipengele namba sita ambacho ndicho kinachokinzana na cha nne alisema: “Wapiga kura ambao wana kadi ya kupiga kura lakini hawamo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kituoni hawataruhusiwa kupiga kura.”
MTANZANIA ilimtafuta Jaji Lubuva ili kupata ufafanuzi wa taarifa hiyo ambapo alisema Tume imejaribu kutafuta namna ya kuyafanya makundi hayo yaweze kupiga kura licha ya kuwapo kwa kasoro ndogo ndogo.

“Sisi tuliwafikiria watu hao kuwa wanaonekana wamejiandikisha na wana vitambulisho, lakini tatizo ni kutokuwapo
kwenye Daftari au namba ya kitambulisho kutofautiana wasishindwe kupiga kura kwa sababu inaonekana kabisa wamejiandikisha,” alisema Lubuva.

Hata hivyo, Jaji Lubuva alitoa maelekezo ya kumtafuta Mwanasheria wa NEC, Emmanuel Kawishe, ili aweze kuelezea mkanganyiko huo.

“Maswali yako ni mazuri, ningependa umpigie Mwanasheria wetu Kawishe umwambie nimeongea na Mwenyekiti kuwa nimekuelekeza kwako ili unipe ufafanuzi wa maswali uliyoniuliza,” alisema Lubuva.

MTANZANIA ilifanikiwa kumpata Mwanasheria huyo Kawishe ambaye kwa bahati mbaya hakuweza kufafanua vizuri huku akidai kubanwa na shughuli nyingi.

Akizungumzia kuhusu mtu mwenye kadi yenye namba tofauti na ya kwenye daftari kuruhusiwa kupiga kura alisema ndiyo busara za Tume.

Mtanzania: “Kwanini mmeruhusu mtu mwenye kadi yenye namba tofauti na kwenye Daftari kupiga kura?”

Kawishe: “Hiyo ndio busara ya Tume.”

Mtanzania : “Huoni kwamba hilo linatoa mwanya kwa mtu mwenye kadi feki kupiga kura?”

Kawishe: “Ajaribu kupiga na kadi feki aone… nina mambo mengi ya kufanya,” alisema na kukata simu.

Mtanzania ilimpiga tena ili kupata ufafanuzi wa kipengele cha nne kukinzana na kile cha sita ambapo alijibu: “Watu hao wana tofauti”.
Alipotakiwa kutoa tofauti hizo alijibu haraka: “Jiulize mwenyewe” na kukata simu.
Awali Ofisa wa NEC, Athuman Masesa, katika mahojiano na MTANZANIA, kwamba Tume imekusanya fomu zote zilizotumika wakati wa uandikishaji ili kuhakikisha kila mtu aliyejiandikisha anakuwapo kwenye Daftari.

Mtanzania ilipotaka kujua kama kutakuwapo na Daftari jingine la Wapiga Kura lenye majina hayo, Ofisa huyo alisema kitakachofanyika ni kuhakikisha kila mwenye kadi ya kupiga kura lazima atapiga kura, na kwamba wametoa
maelekezo hayo kwa wasimamizi wote wa uchaguzi nchini.

“Naomba uchukue hii kutoka kwangu kwamba mtu yeyote ambaye ana kadi halali iliyotolewa na NEC lazima atapiga kura. Kuna mchakato tunaufanya wa kukusanya zile fomu zote zilizoandikisha wapigakura ili kuangalia ni majina gani hayapo kwenye Daftari ili yaweze kupelekwa vituoni,” alisema Masesa.

Hata hivyo alisema watu ambao hawataruhusiwa kupiga kura ni wale ambao majina yao yapo kwenye Daftari lakini hawana kadi ya kupigia kura.

“Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inasema ili mtu aweze kupiga kura kwanza lazima awe na kadi ya kupiga kura, hivyo unaweza kuona kitu cha kwanza ni kuwa na kadi, hivyo kama hauna huwezi kupiga kura,” alisema Masesa.

MTANZANIA pia ilizungumza na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu ya Mpiga Kura na Habari wa NEC, Clarence Nanyaro, kutaka kujua kama mtu anaweza kupigia kura rais sehemu yeyote atakapokuwa siku ya kupiga kura.

Nanyaro alifafanua kuwa kila mtu atatakiwa kupigia kura zote (urais, ubunge na udiwani) katika kituo alichojiandikisha, isipokuwa wale waliopewa kibali maalumu kutoka NEC.

Alitaja makundi yaliyopewa kibali hicho kuwa ni pamoja na mawakala wa vyama vya siasa, wasimamizi na wasaidizi wa wasimamizi wa vituo, wagombea wa ngazi zote za udiwani, ubunge na urais pamoja na watumishi wa NEC.

Alisema watu walio katika makundi hayo watalazimika kujaza fomu namba 18 na 19 zilizopo katika vituo vya kupiga kura kabla ya kupiga kura.

Alisema watu hao wataweza kupiga kura ya rais wakiwa sehemu yeyote, lakini kwa upande wa diwani na mbunge lazima awe katika kata au jimbo alilojiandikishia.

Kuhusu makosa yaliyobainishwa kwenyeDaftari la Kudumu la wapiga Kura, ikiwamo kuwepo kwa picha na majina yasioendana na wapigakura, alisema Tume inazifanyia kazi kasoro hizo.

Wakati haya yakijiri, NEC imebandika majina ya wapigakura katika vituo vyote vya kupigia kura na kuwataka wapigakura waende kwenye vituo vyao walipojiandikisha kupiga kura ili kuhakiki kama majina yao yapo kwenye mbao za matangazo au la kwenye vituo husika.

Tangu kutolewa kwa tangazo hilo kupitia njia mbalimbali, zikiwamo nyumba za ibada, mwishoni mwa wiki iliyopita, wapigakura wamekuwa wakienda kwenye vituo vyao vya kupiga kura kuhakiki majina yao kama walivyoelezwa na NEC.

Baadhi ya watu wamekuta majina hayapo kwenye mbao za matangazo. “Cha kushangaza, unakuta mtu ambaye jina lake halipo, siku alipokwenda kujiandikisha alifuatana na mke/ mume wake na watoto wao waliofikia umri wa kupiga kura, lakini baadhi ya majina ya familia hiyo iliyojiandikisha siku moja hayapo na mengine yapo,” alisema juzi Frederick

Massawe, Mkazi wa Mbweni JKT (Ndege Beach), nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Alisema, kwa mfano, katika kituo cha kupigia kura cha New Era Primary & Sekondary, Mtaa wa Malindi Estate, kata ya Mbweni jijini Dar es Salaam juzi, watu walikwenda kwenye kituo hicho na kukuta majina yao hayapo wakati walijiandikisha katika kituo hicho hicho na wana vitambulisho vya kupiga kura vilivyotolewa na NEC mahali hapo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles