29.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 30, 2024

Contact us: info@mtanzania.co.tz

NEC TUNATEKELEZA KATIBA YETU INAVYOTAKA- KAILIMA

Na, ABDULWAKIL SAIBOKO


NCHI  jirani ya Kenya imemaliza moja ya uchaguzi wake wa kihistoria hivi karibuni, pamoja na upungufu uliojitokeza baada ya uchaguzi na kusababisha kufutwa kwa matokea ya Rais, bado kuna kundi kubwa la watu ambao wanaamini kwamba uchaguzi wa Kenya ulikuwa wa kipekee. Pia wanaamini kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inalo la kujifunza.

Katika vipindi mbalimbali tangu ulipomalizika uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani amekutana na kufanya mahojiano na waandishi wa habari juu ya suala hilo na ameweza kutoa maoni yake.

“Ningependa kuwakumbusha wadau wetu kwamba NEC inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoundwa mwaka 1977, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (sura ya 343), Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Sura ya 292) na sheria nyingine mbili za Serikali za Mitaa; ile ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) (Sura ya 287) na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) (Sura ya 288) pamoja na kanuni zake,” alisema Kailima.

Mkurugenzi huyo alisema Tume imepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wake ambao wanahoji juu ya ni kwanini NEC haiendeshi mambo yake kama Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya.

Kwa mfano, alisema swali ambalo limeulizwa sana ni kuhusu uchaguzi wa Rais kwamba ni kwanini matokeo hayapingwi mahakamani?  Kailima alisema suala hilo lipo kisheria na linatokana na ibara ya 41 ya Katiba ambayo inaeleza kwamba NEC ikishamtangaza mshindi hakuna pingamizi litakalowekwa mahakamani.

“Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake,” inasomeka ibara ya 41 (7) ya Katiba.

“Lazima itambulike kwamba Katiba ni sauti ya watu na kwa sasa Katiba iliyopo ndiyo inayowakilisha maoni ya Watanzania angalau kwa sasa, tunalazimika kuifuata Katiba ipasavyo. Kama Katiba au ibara husika itabadilishwa, Tume nayo itabadilika,” alisema.

 

Kailima alisema kwamba Katiba inapozungumzia kushinda inakusudia mgombea ambaye atapata kura nyingi hata kama ni kura moja tu na kwa kupitia uwiano wa kura wanapatikana madiwani na wabunge wa Viti Maalumu kwa kila chama. Kwa msingi huu inamaana hata kama mgombea wa nafasi ya Urais atapata ushindi wa kura moja atakuwa ameshinda na hatapingwa mahakamani.

“Mgombea yeyote wa kiti cha Rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa Rais iwapo tu amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote,” inasema ibara ya 41 (6) ya Katiba.

Akizungumzia suala la mgombea binafsi kwa kulinganisha na uchaguzi wa Kenya na kwa kuzingatia juhudi mbalimbali ambazo wananchi wamefanya kuhakikisha suala hilo linafanikiwa na wengine kufikia hatua ya kwenda mahakamani bila mafanikio, Mkurugenzi huyo wa uchaguzi alisema kwamba ni muhimu Watanzania wakaisoma Katiba kwa umakini.

“Mtu anapoisoma ibara yoyote ndani ya Katiba ni muhimu kuisoma kwa ukamilifu wake ili apate uelewa mzuri. Katiba inasema kwamba ni haki ya mwananchi kupiga na kupigiwa kura lakini ibara ya 67 inasema mgombea lazima apendekezwe na kufadhiliwa na chama cha siasa na kwa msingi huo NEC inatambua wagombea waliotimiza kigezo kilichowekwa na ibara hiyo,” alisema.

“Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo; (a) ni Raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka 21 na ambaye anajua kusoma na kuandika  Kiswahili au Kiingereza; (b) ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa…..” inasomeka Ibara ya 67 (1) ya Katiba.

Kailima alisema tume itakuwa tayari kutekeleza maelekezo mengine yoyote ya kisheria ambayo yatawekwa kwenye Katiba na wananchi kupitia Bunge.

Alikataa kutoa msimamo wake binafsi kwenye suala la mgombea binafsi kwa kuwa msimamo huo unaweza kutafsiriwa kuwa ni msimamo wa tume. Lakini akisisitiza kwamba mabadiliko yoyote yakijitokeza yatatekelezwa na tume bila kusita.

Wafungwa nchini Kenya wanaruhusiwa kupiga kura, suala hili linaonekana kuwa la kipekee miongoni mwa Watanzania kwa kuwa hapa nchini wafungwa hawaruhusiwi kupiga kura, vile vile suala la Wakenya waliopo Ughaibuni kupiga kura limewavutia wengi.

Kailima alisema hapa Tanzania tunachagua Rais kupitia kwenye majimbo, vituo vya kupigia kura vinatakiwa kuwa ndani ya majimbo ya uchaguzi, vituo hivyo vinapatikana ndani ya halmashauri. Tuna majimbo 264 na hakuna mahali kwenye Katiba au kwenye sheria ambako wananchi wanaoishi Ughaibuni au wafungwa wanatambulika kama wapo kwenye majimbo ya uchaguzi, endapo tutaongozwa na sheria kwenye jambo hili tutalifanyia kazi”.

Alisema ibara ya 74 (6) (C) inaielekeza Tume kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye majimbo kwa minajili ya kuchagua wabunge na Rais. Na akaongeza kwamba kwa kuwa mamlaka ya Tume yanaishia ndani ya mipaka ya nchi, haitaweza kuvuka mipaka.

“Majukumu ya Tume ya Uchaguzi yatakuwa ni; (a) kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Jamhuri ya Muungano; (b) kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge; (c) kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge; (d) kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura na uendeshaji wa uchaguzi wa madiwani; (e) kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge,” inasomeka Ibara ya 74 (6) ya Katiba.

“Kama sheria za nchi zingeeleza kwamba Tume inapewa jukumu la kuandaa uchaguzi Ughaibuni, tungefanya hivyo bila kusita,” alisema  Kailima .

Aliongeza kusema kwamba kwa mtu kuwa na sifa za kupiga kura lazima ajiandikishe kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura na kwa mujibu wa sheria zilizopo, ni muhimu kwa vyama vya siasa kuwa na wawakilishi kwenye mchakato wa uandikishaji  na kwa kuwa vituo vya kujiandikishia ndio vituo vya uchaguzi, sheria haijaruhusu kuwa na kituo cha kujiandikishia gerezani au kwenye balozi za Tanzania nje ya nchi.

Kailima aliongeza kwamba kwenye mchakato wa kupiga kura, vyama vya siasa pia vina wakala wao na sheria zilizopo bado hazijaweka utaratibu kama huo kwa wanaoishi Ughaibuni na wafungwa kwa sababu Katiba haijatoa haki kama hiyo kwa watu waliopo kwenye makundi hayo.

Kuhusu uwezo wa tume kuwa na ushawishi katika masuala ambayo wadau wanayazungumzia ambayo yapo kisheria,  Kailima alisema kwamba Tume haina ushawishi wowote bali inategemea zaidi wadau wanaohusika na masuala ya kurekebisha sheria washughulikie mambo hayo wakiwamo wananchi ambao ndio wadau wakuu katika kutoa maoni juu ya Katiba kupitia Bunge na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia suala la Teknolojia na Mahusiano yake na uwezo wa Tume kuwaandikisha Watazania wanaoishi Ughaibuni pamoja na wafungwa. Kailima alisema “Tatizo si teknolojia, IEBC haina teknolojia ya juu kuishinda NEC, Kenya kuna vituo vya kupigia kura 40,000 na zaidi kidogo, kati ya hivyo 11,000 havikuwa katika mfumo wa mtandao, walikuwa wanatumia daftari. Hapa Tanzania tuna vituo zaidi ya 65,000, vituo 1504 vipo Zanzibar na vilivyobaki  vipo Tanzania Bara, tunatumia daftari letu la Kudumu la Mpiga Kura…..

Ukilinganisha na Kenya, tupo wazi zaidi kwa wapiga kura wetu na wadau kwa ujumla, kila inapofikia mwenzi mmoja kabla ya uchaguzi tunavikabidhi vyama vya siasa daftari. Sina uhakika kwamba hali iko hivi huko Kenya. Daftari tunalowapatia vyama vya siasa wanawapa wawakilishi wao kwenye vituo vya kupigia kura, wanatumia daftari hilo kuhakiki usahihi wa majina wanayoyakuta vituoni”.

Alisema kwamba mifumo ya NEC ipo wazi zaidi na ni madhubuti zaidi na kwa mantiki hiyo inapunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko yanayohusiana na uendeshaji wa uchaguzi.

“Tunayo teknolojia, tuko vizuri sana kwenye eneo hilo kama Tume na kama mtu anataka kulinganisha uwezo wetu na IEBC kwenye kutangaza matokeo kwa haraka, sisi tupo vizuri zaidi, uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 tulitangaza matokeo ya Rais ndani ya saa 72.  Kwenye kutangaza matokeo kuna matokeo ya awali na matokeo yaliyothibitishwa, wakati sisi huwa tunatangaza matokeo yaliyothibitishwa, IEBC wanatangaza matokeo ya awali bila kuangalia kilichopo kwenye fomu namba 34A kwenye kituo cha kupigia kura na 34B kwenye jimbo, ambazo ndio zinabeba matokeo yaliyothibitishwa,” alisema.

Aliongeza kwamba “Hapa Tanzania, tunatangaza matokeo yaliyothibitishwa ambayo yapo kwenye Fomu namba 24A, matokeo hayo yanakuwa yamethibitishwa na mawakala wa wagombea pamoja na msimamizi wa uchaguzi ambaye ndiye anayeyatuma kwetu na yanapotufikia sisi hatubadili chochote, tunachofanya ni kuonyesha fomu kwa wadau. Baada ya hapo fomu zinawekwa kwenye mfumo wa kielektroniki”.

Kailima alisema kwamba ili kuhakikisha kuna uwazi na kupunguza uwezekano wa kupata malalamiko ya wagombea au wanasiasa, tume inawakaribisha wanasiasa kwenye eneo ambako majumuisho na utangazaji wa washindi unafanyika ili waweze kushuhudia mchakato unavyokwenda.

Aliongeza kwamba kituo cha kutangaza matokeo kinashughulikia majumuisho ya kura za wabunge na Rais na kura za madiwani zinashughulikiwa kwenye ngazi ya kata.

Kailima alisema kwamba kwenye vituo vya kupigia kura kuna Fomu namba 21A, ambayo ina matokeo ya Rais, wawakilishi wa vyama vya siasa wanapewa nakala, na matokeo yote yanajumlishwa kwenye ngazi ya jimbo na kuwekwa kwenye Fomu namba 24A.

Alisema “Inategemewa kwamba mawakala watakuwa na fomu zao ili kuhakiki matokeo yanayosomwa kwenye ngazi ya jimbo na kwenye ngazi ya Taifa. Hali ya Kenya ilikuwa tofauti, kwa mfumo wao ambao watu wanadhani ni madhubuti sana, walitangaza matokeo yasiyo rasmi na hiyo ndiyo maana baadaye walilazimika kujifungia ndani na kuanza kupitia fomu moja baada ya nyingine. Nataka watu wajue kwamba mfumo wa Analojia unatumika hata Uingereza, sisemi kwamba ndio mfumo bora, lakini matumizi ya matokeo yasiyo rasmi yanasababisha makosa, ni bora kukawia lakini ufike, kuliko kuharakisha halafu ukutane na vikwazo”.

Alielezea mipango ya NEC kwamba itaweka mifumo ya Kidijitali ambayo itakuwa inaonesha matokeo yaliyothibitisha kadri yanavyoifikia tume kwenye kituo cha kutangazia matokeo.

“Tunataka kuhakikisha kwamba muda mfupi baada ya matokeo kutangazwa na Mwenyekiti wa Tume kwamba mgombea fulani ameshinda kwenye jimbo fulani, punde matokeo hayo yanawekwa kwenye mfumo wa elektroniki,” alisema.

Akizungumzia uhuru wa tume, Bw. Kailima alisema kwamba inasikitisha kwamba malalamiko kwamba NEC haipo huru yanatokea wakati wa uchaguzi tu.

“Sijawahi kumsikia mwanasiasa akilalamikia kushindwa kwa tume kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa kwa mujibu wa Katiba, wanalalamika wakati wa uchaguzi tu kwamba tume haipo huru. Hii si sawa. Tungependa kuona wanasiasa wakija na ushahidi wa kuthibitisha madai yao kwa NEC, vinginevyo malalamiko ya jumla tu yanaweza kutafsiriwa kwamba ni shutuma zisizo na msingi,”alisema.

Kuhusu vyombo vya habari kuwa na mwamko mkubwa kwenye uchaguzi wa Kenya tofauti na ilivyo hapa Tanzania, Kailima alisema vyombo vya habari vinalo la kujifunza kutoka kwa wenzao wa Kenya kwa kujituma zaidi katika kuwapa wananchi taarifa zinazohusiana na uchaguzi hasa kipindi cha uchaguzi.

Kailima alisema kwamba vyombo vya habari vya Kenya vilikuwa na programu nyingi sana zinazoshabihiana na uchaguzi na miongoni mwa programu hizo nyingi zilifanywa kwa kupitia mahojiano na watu mbalimbali ambapo wengine hawakuwa watumishi IEBC jambo ambalo linaweza kuigwa na vyombo vya habari vya Tanzania. Aliongeza kwamba NEC itajitahidi kadri iwezekanavyo kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari.

“Nataka niwahakikishie wadau wetu kwamba, uchaguzi wa mwaka 2020 utakuwa wa aina yake, kuna mikakati yetu tumeiweka kuhakikisha kwamba tunaboresha sana mifumo ya Teknolojia ya kutangaza matokeo,” alisema.

Mwandishi wa Makala haya ni Afisa habari wa NEC

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles