32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Ndumbaro ataka kampuni nyingi za Ubelgiji kuwekeza nchini

Na Mwandishi Wetu -Dar es Salaam


NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Damas Ndumbaro amesema kampuni 32 kutoka Ubelgiji zilizowekeza Tanzania ni chache ukilinganisha na wingi wa fursa za uwekezaji zilizopo ambazo bado hazijatumika kikamilifu.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaan jana katika maadhimisho ya Siku ya Mfalme wa Ubelgiji.

“Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, ujenzi wa miundombinu, nishati, madini, teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, viwanda vya uzalishaji, mafuta na gesi ambazo hazijatumika ipasavyo.

“Ubelgiji na Tanzania zikijizatiti zinaweza zikafanya biashara na uwekezaji mkubwa na wenye manufaa kwa pande zote mbili,” alisema.

Ndumbaro alisema ujio wa kampuni kubwa zaidi ya 40 za Ubelgiji una tija na kampuni za Tanzania zinazohusika na uwekezaji kwa siku tatu zilizopita utaimarisha kiwango cha biashara.

Kuhusu biashara kati ya Tanzania na Ubelgiji, alisema ameridhishwa na urari uliopo na alisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi.

Pia alitoa mfano wa programu mbalimbali za maendeleo zinazogharamiwa na Serikali ya Ubelgiji kwa kiasi cha euro milioni 20.

Programu hizo zinajumuisha upatikanaji wa maji safi vijijini na uendelezaji endelevu wa sekta ya kilimo mkoani Kigoma na utekelezaji wake umesaidia kuboresha usimamizi mzuri wa vyanzo vya maji, usimamizi wa rasilimali na mnyoro wa thamani katika kilimo.

Kwa upande wake, Balozi wa Ubelgiji hapa nchini, Peter van Acker, alisema nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kubadilisha maisha ya watu masikini.

Alisema jitihada hizo zitaunga mkono juhudi za Tanzania za kuleta utulivu wa kisiasa eneo la Maziwa Makuu ikiwamo usuluhishi wa mgogoro wa Burundi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles