29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugu wadaiwa kumuua shemeji yao kwa kumnywesha sumu

Na ELIUD NGONDO

 -MBEYA

WATU wawili wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Ifumbo, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, wanashikiliwa na polisi kwa kumuua ndugu yao, Osward Malambo kwa kumnywesha sumu wakiwa wamemuweka chini ya ulinzi kwa kumtisha na bastola kisha kumpora Sh milioni 55.

Kaka wa marehemu, Selemani Malambo, alisema ndugu yao ambaye ni mfanyabiashara, aliondoka nyumbani kwao kwenda Mbalizi kuuza ufuta akiwa mzima, lakini wakati akijiandaa kurudi aliombwa na watuhumiwa wakafanye mazungumzo.

Selemani alisema watuhumiwa wawili waliokamatwa ni shemeji zao na mmoja ambaye ametoroka ni mjomba yao, na kwamba awali walikuwa na kesi mahakamani ambayo inaendelea hadi sasa.

Alisema Osward aliitwa na watuhumiwa ili wakazungumze namna ya kuiondoa kesi hiyo mahakamani.

Selemani alidai kuwa watuhumiwa walimtaka ndugu yao huyo wakazungumze naye kwenye moja ya baa zilizopo katika eneo la Kabwe jijini Mbeya na alipofika akiwa na wadogo zake, walimtaka awaache wadogo zake nje ili wasisikie kinachozungumzwa.

Alidai kuwa baada ya kuingia kwenye baa hiyo, waliendelea na mazungumzo, wakimuweka chini ya ulinzi kwa kumuoneshea bastola na wakamtaka achague moja; kunywa juisi yenye sumu ama kupigwa risasi ndipo akachagua kunywa juisi.

 “Alitupigia simu kuwa anaumwa, anaomba tumpeleke hospitali na tulipofika alitueleza kila kitu walichofanya, lakini pia alitueleza kuwa walimwambia aweke fedha zote mezani wakazichukua na wakamwambia watawaua wote atakaowaambia,” alidai Selemani.

 Aidha mdogo wa marehemu, Ernest Malambo alidai kuwa familia yao inapata vitisho kutoka kwa marafiki wa watuhumiwa, akiwemo mmoja anayejitambulisha kwa jina la Hitla kuwa watawaua wote.

Alidai kuwa wanawatumia ujumbe wa simu wakiwaeleza kuwa wamemuua mmoja na wataendelea kuwaua wengine na kwamba wana mtandao mkubwa na watawaua wote.

Aliliomba Jeshi la Polisi kuwasaidia ulinzi wa familia ili wasije wakadhuriwa na watu hao wanaotoa vitisho.

Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alisema watuhumiwa hao ni Raphael Walolile na Goliat Walolile.

Alisema marehemu Osward ambaye alikuwa mfanyabiashara wa ufuta, alikuwa ananunua zao hilo katika wilaya za Songwe na Chunya na kuuza Mbalizi mkoani Mbeya.

Alisema Juni 2 Osward alitoa taarifa za kunyweshwa sumu na watuhumiwa kabla umauti haujamfika.

“Hawa watuhumiwa walishirikiana na mtu mwingine ambaye anajulikana kwa jina la Peter Mpamba ambaye alikimbia baada ya Osward kufariki, tunaendelea kumsaka na tutahakikisha anapatikana na kutiwa nguvuni.

 “Kwa sasa bado tunasubiri taarifa za daktari ili tujuwe kama kweli alinyweshwa sumu na ikibainika kuwa ni kweli tutawashtaki watuhumiwa hao kwa kosa la mauaji,” alieleza Kamanda Matei.

Ndugu wa marehemu wakati wanachukua mwili katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya, waliliomba Jeshi la Polisi kuwasaidia kwa kuwa wanapata vitisho kutoka kwa marafiki wa watuhumiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles