23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai, Tulia wagombea pekee Uspika, Unaibu bungeni

Ramadhani Hassan -Dododma

ALIYEKUWA Spika wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai  na Naibu Spika, Dk. Tulia Akson wamechukua fomu za kugombea nafasi hizo kwa Bunge la 12.

Wa kwanza kuchukua fomu hizo jana alikuwa ni Ndugai ambaye ni Mbunge Mteule wa Kongwa kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye alifika Makao Makuu ya CCM majira ya asubuhi na kuchukua fomu hizo.

Ndugai ambaye mwaka 2010-2015 alikuwa Naibu Spika wa Bunge huku mwaka 2015-2020 akishika nafasi ya uspika.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Ndugai aliwaomba Watanzania wamuombee ili chama chake kimpitishe kugombea uspika ndipo atakapozungumza na watanzania.

“Nikweli nimejitokeza kuchukua fomu leo (jana) Novemba 3 na nimefika  hapa Makao Makuu kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Uspika, nimepewa fomu, nimeijaza na kuirudisha kwa kufuata matakwa yote yanayotakiwa na chama chetu.

“Kwa sasa niwaombe mniombee chama changu kiniruhusu ili niweze kuwa Spika,” alisema Spika Ndugai kwa kifupi  huku akielekea katika gari.

ACHUKUA NA KUREJESHA  

Uchukuaji fomu katika nafasi ya Uspika na unaibu Spika lilianza juzi Novemba mwaka huu ambapo lilitarajiwa kufungwa jana ambapo mara baada ya Spika kuchukua fomu hiyo aliijaza na kuirejesha.  

“Ni utaratibu wa chama chetu wa kidemokrasia kwamba tunaenda katika utaratibu huo kwa sababu nafasi ya Spika inajazwa kwa wanaopendekezwa na vyama vya siasa. Kwa hiyo  nia yangu kama chama changu kitanikubalia kuwa Spika wa Bunge la 12 linalokuja kama nitateuliwa nitaongea na watanzania wakati huo,” alisema Ndugai.

NAIBU SPIKA MA UTUMISHI

Mwingine aliyechukua fomu jana na kuirejesha ni aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lilopita, Dk. Tulia Ackson ambaye baada ya kuchukua fomu alizungumza na Waandishi wa Habari na kusema kwamba nafasi aliyoomba ni kwa ajili ya utumishi na shauku yake kubwa ni kuona waliochaguliwa wanawawakilisha wananchi.

“Hizi ni nafasi kwa ajili ya utumishi miaka ijayo nilifanya kazi katika nafasi hiyo, naiomba tena shauku yangu ni kuona wabunge wakiwawakilisha wananchi  wao waliowachagua.Yale ambayo yameahidiwa wao kama wabunge watatakiwa kuyafuatilia ikiwa ni pamoja na mimi,” alisema.

KWANINI NAIBU SPIKA NA SIO SPIKA?

Akijibu swali aliloulizwa na Waandishi wa Habari ni kwanini Unaibu Spika na sio Spika, Dk. Tulia alisema amechukua fomu ya unaibu Spika kwa sababu atakuwa na kazi mbili, ya unaibu Spika  pamoja na kuwasemea wananchi wa Mbeya Mjini ambao wamemchagua kuwa mbunge wao hivyo hawezi kuchukua fomu ya uspika.

“Mwanzoni wakati naeleza hapa nilisema hizi nafasi ni za utumishi, kwa hiyo mtu unapokuja kuchukua fomu unakuwa umepima zile kazi ambazo zipo mbele yako, na mimi ninaomba hii nafasi kwa sababu kwa sababu nitakuwa na kazi mbili, sio Naibu Spika pekee, ni pamoja na kuwawakilisha wakazi wangu wa Mbeya Mjini.

Alipoulizwa inawezakana anaogopa ushindani wa Ndugai katika nafasi ya Spika alisema: “Hapana sio kwa habari ya ushindani kama ni ushindani sidhani kama mimi ni mmoja ya watu ambao wanaogopa ushindani unaweza kuona Jimbo ambalo nimetoka kwa kuwa Mbunge sio la kawaida na mimi ni mdada na ndio wa kwanza”.

BUNGE LILOPITA LILIKUWA GUMU

Akielezea kuhusiana na hali ya Bunge lilopita, Dk. Tulia alisema lilikuwa gumu kutokana na baadhi ya wabunge ambao walikuwa wapya kutokujua sheria lakini kadri siku zilivyozidi kwenda walizijua kanuni hizo.

“Mimi kwa sababu kazi hii tulianza mwaka 2015 kazi ilikuwa ngumu sana mwanzoni kwa sababu wabunge wengi walikuwa wapya,na walikuwa hawazifahamu sheria na kule ndani kila mmoja anafikiri kila saa anaweza kuzungumza.Ule ugumu ulitokana na kutokujua sheria lakini kadri ulivyoeenda wabunge wengi walikuja kujua kanuni,” alisema.

NENO KWA WABUNGE WAPYA

Dk. Tulia alitoa wito kwa wabunge wapya ambao wamechaguliwa  kuzisoma na kuzijua kanuni za namna ya kufanya kazi bungeni pamoja na jinsi ya kupata fursa ya kuzungumza.

“Ningetoa  wito kwa  wabunge wapya wazifuatilie zile kanuni wanazofundishwa namna ya kufanya kazi bungeni na namna ya kushirikiana na namna ya kupata fursa ya kuzungumza bungeni,” alisema.

BUNGE LA INA IPI

Alipoulizwa Watanzania  watarajie  Bunge la aina ipi, mbunge huyo mteule wa Mbeya Mjini alisema anaamini litakuwa na wawakilishi wazuri ambao watawasemea wananchi.

“Tutarajie uwakilishi mzuri mimi yule mtu ambaye nawaza mambo mazuri kwa hiyo natarajia wananchi wamewachagua wale wanaowataka wao na wenye uwezo wakuwawakilisha tutarajie uwakilishi mzuri,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles