27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

NDUGAI: NIMEPOKEA BARUA YA KUJIUZULU YA DK. POSSI

Dk. Abdallah Possi
Dk. Abdallah Possi

Na AGATHA CHARLES – dar es Salaam

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amepokea barua ya kujiuzulu ubunge ya Dk. Abdallah Possi, aliyeteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kuwa balozi.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano-Ofisi ya Bunge, ilisema Ndugai alipokea barua hiyo juzi.

Ndugai alisema kutokana na kujiuzulu huko, ilimlazimu kumwandikia Rais Magufuli barua ili kumjulisha kuwa hivi sasa bungeni kuna wabunge wa kuteuliwa saba, hivyo nafasi zilizobaki wazi ni tatu.

“Kutokana na barua hiyo ya kujiuzulu ubunge wa Dk. Possi iliyozingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara ya 67 (1) (g) ikisomwa pamoja na ibara ya 149 (1) (d), Spika wa Bunge amemwandikia rasmi rais kuwa hivi sasa wabunge wa kuteuliwa na rais waliopo bungeni ni saba na hivyo nafasi zilizo wazi ni tatu baada ya Dk. Possi kujiuzulu,” alisema.

Ndugai aliyazungumza hayo ikiwa ni siku moja baada ya MTANZANIA Jumapili kuzungumza na Dk. Possi aliyeteuliwa Alhamisi wiki hii kuwa balozi na kusema tayari alikuwa ameandika barua ya kujiuzulu ubunge.

Dk. Possi alikuwa miongoni mwa wateule wa ubunge wa Rais Magufuli ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa balozi, kuliibuka mjadala kwamba matakwa ya kikatiba ya kukidhi uwiano wa kijinsia hayakufuatwa.

Mjadala huo ulijitoleza baada ya Rais Magufuli kuwateua wabunge wawili wapya ambao ni Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo na kufanya idadi ya wabunge wa kuteuliwa kwa wakati huo kuwa wanane huku kati yao wawili wakiwa wanawake.

Uamuzi huo wa Dk. Possi anayesubiri kupangiwa kituo chake cha kazi, angalau ulipunguza nguvu ya mjadala wa madai ya Rais kushindwa kufuata matakwa ya katiba.

Hata hivyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alikaririwa na gazeti la MTANZANIA juzi akisema Rais Magufuli hakuvunja sheria kufanya uteuzi huo.

Mbali na Dk. Possi na kabla ya uteuzi wa Profesa Kabudi na Bulembo, waliokuwa wameteuliwa kuwa wabunge ni Dk. Philip Mpango, Balozi Dk. Agustine Mahiga na Profesa Makame Mbarawa huku wanawake wakiwa ni Profesa Joyce Ndalichako na Dk. Tulia Ackson.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles