23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai, Chadema nani yuko sahihi?

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

NCHI hii haiishi gumzo, likitoka hili linaingia jingine, na sasa ishu kubwa inayozungumzwa kila mahali ni kauli na pengine uamuzi uliochukuliwa na pande mbili, Spika wa Bunge anayeongoza Bunge la Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania na Chama Kikuu cha Upinzani, Chadema.

Msingi wa mjadala wa sasa ni uamuzi wa Chadema kujiweka karantini baada ya kile wanachosema ni kujikinga na maambukizi ya  virusi vya corona baada ya wabunge wenzao watatu kufariki dunia hivi karibuni.

Ingawa hawajaweka wazi kama wabunge hao wamekufa kwa virusi vya corona wanatilia shaka shughuli za mazishi yao zilivyokwenda haraka na hivyo kuchukua hatua hiyo kulilazimisha Bunge kupima wabunge wote au  kuchukua hatua za kujilinda dhidi ya maambukizi hayo.

Hata hivyo, agizo la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe la kutoingia bungeni limepata mtikisiko kutoka kwa Spika wa Bunge ambaye hakubaliani na hoja zao  na ambaye amekwenda mbali zaidi na kutoa tishio la kuzuia mafao yao wakati ukiwa umebaki muda mfupi tu kufikia ukomo wa ubunge wao wakati Taifa likijiandaa na uchaguzi mwingine uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Lakini pia mtikisiko mwingine ni agizo hilo kutoitikiwa na wabunge wote wa Chadema kwani baadhi wameendelea kuhudhuria vikao vya Bunge ambao Ndugai amesema hawatahusika kwenye kurejesha fedha.

Wabunge hao ni pamoja na Peter Lijualikali wa Kilombero, David Silinde (Momba), Jafary Michael (Moshi Mjini) na Wilfred Lwakatare (Bukoba mjini).

Wengine ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini na  Antony Komu (Moshi vijijini) ambao wametangaza kuhamia NCCR Mageuzi baada ya Bunge kwisha.

Wengine ni wabunge wa viti maalumu; Ratifa Chande,  Sabrina Sungura, Suzan Masele na Mariam Msabaha.

Mjadala umekwenda mbali zaidi ya hapo baada ya Spika, Job Ndugai kuwataka wabunge wa Chadema waliojiweka karantini ya wiki mbili warudi bungeni ama warejeshe fedha walizochukua.

Ni kama kiongozi huyo amewaongezea mtihani akienda mbali zaidi akisema huenda wakapoteza mshahara wa Mei na mafao mengine.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangazia wabunge wa Chadema kutoingia bungeni wala kusogea katika mazingira ya Bunge Dar es Salaam na Dodoma.

Badala yake aliwataka wote wakae ndani kwa wiki mbili mjini Dodoma ili kujilinda na virusi vya corona huku akiwataka pia wasiende majimboni mwao.

Ndugai anaona tangazo la Mbowe ni batili na mapema wiki hii aliwataka wabunge hao kurudi bungeni ama kurejesha fedha za wiki mbili, zaidi ya Sh milioni 110 ambazo walikuwa wamelipwa kama posho ya kujikimu.

Pia alisema wakikaidi agizo lake hilo, wiki mbili walizojipa zikiisha watalazimika kwanza kupimwa corona kisha ndiyo waingie bungeni wakishalipa fedha walizochukua.

Akizungumza kabla ya kuhitimisha Bunge katikati ya wiki hii, Ndugai alisema kuna mambo matano wabunge wanatakiwa kuyazingatia badala ya kudhani chama pekee ndicho chenye hatma ya ubunge wao.

 “Wabunge wengi ni wa mara ya kwanza, hasa wa upinzani, hivyo viongozi wao wamekuwa wakiwateka nyara kwa u-mara wa kwanza wao, wamewajaza imani ya kufikiri kwamba chama chao peke yake ndicho chenye ‘Alfa na Omega’ katika kazi zao za ubunge kitu ambacho si kweli kiasi hicho.

“Mbunge anapofanya shughuli zozote zile za kibunge, ana mambo kama matano ya ‘ku-balance’ (kuweka kwenye uwiano), kwanza lazima aangalie taratibu za kibunge, kwa maana ya sheria na kanuni, lakini pili lazima aangalie je jambo linaloendelea ambalo inatakiwa yeye afanyie kazi lina masilahi gani kitaifa.

“’Balance’ ya tatu lazina aangalie jimbo lake, wananchi waliomtuma. Je, hili lina masilahi kwa wananchi wangu? Suala la nne ni chama kilichomtuma. Je, katika jambo hili kina mtizamo gani? Suala la tano ni mbunge mwenyewe, wewe mwenyewe, hiyo barua ya Mbowe wewe unaona ina mantiki? 

“Na wananchi wa jimbo langu wanakubali wewe ukae ndani usifanye shughuli za Bunge? Je, hilo jambo lina masilahi kitaifa? Je, hilo jambo limetokana na vikao vya chama chako au ni amri ya mtu tu? Maana mtu si chama, sasa wabunge ni watu wazima, lakini kwa sababu ni mara ya kwanza wanajazwa vichwani mwao kwamba bwana Mbowe akitaka unakuwa mbunge au auwi mbunge.

“Katika hayo ‘usipoya-balance’ vizuri, wewe ukabeba moja tu itakula kwako, wamekuwa (Chadema) wakitaka nchi iwekwe kwenye ‘lockdown’, sasa wananchi wengi kule Kongwa na kwingineko hawaelewi ‘lockdown’ ndo nini, labda ni jambo jema hilo kwanini wanakataa hawa?

 “’Lockdown’ maana yake wananchi wote muwekwe rumande ya hiyari, kila mtu akae kwakwe, atakayekuwa Morogoro ubanishwe hapohapo, Tabora ubanishwe hapohapo, hakuna kutoka, kuzunguka, kufanya biashara wala kwenda mashambani, inabidi mkae ndani, sasa kukaa rumande nani anataka?

 “Na pia hata hizo rumande mabunge ya nchi nyingi ndiyo yameishauri Serikali, kama Bunge kama taasisi, sisi hatujashauri Serikali jambo hilo na hatudhani kama wananchi wetu wanataka jambo hilo, kama wanataka wasema tuishauri Serikali ishauri ‘lockdown’ hata ya siku saba Watanzania hawa waelewe, hiyo rumande ni hatari kubwa. Kwa hiyo tunadhani mwongozo wa Serikali ni suala la maana,” alisema Ndugai.

 “Sasa nilielezea jana (juzi) kuhusu kuchukua fedha, maana wamelipwa tangu Mei 1 – hadi 17, halafu wakaamua kuwa watoro na kutokufanya kazi, naendelea kusisitiza ambao hawatarudisha fedha hizo tutawachukulia hatua manake tutahesabu ni wizi wa kuaminiwa.

“Ulipewa fedha kwamba umeaminiwa zitakusaidia kufanya kazi, wewe unaamua kutoroka, nilisema jana ni utoro na warudishe, wakirudisha hatuna maneno, habari ya kusema tutakata baadaye haipo hiyo.

 “Pia natoa tangazo tumeshapokea kutoka taasisi mbalimbali za fedha nchini taarifa za bakaa ya mikopo ya wabunge wote, mikopo mbalimbali ambayo itatumika katika kukokotoa na kulipa mafao ya kazi ya ubunge.

 “Kesho nitaelekeza watu wangu wa uhasibu watoe barua kwa wabunge waliopo kwa kumkabidhi kwa ‘dispatch’ siyo kwa e-mail wala kupeleka kwenye ‘tablet’ kwa sababu hii hatutaki liwe tangazo, atapewa mbunge mmoja mmoja kwa waliopo, hawa wasiokuwepo waendelee kukaa hukohuko wakose hizi ‘information’.

“Na mwisho wa mwezi huu kuna shughuli inaendelea ambayo wao wanaifahamu vizuri kuliko mwananchi mwingine, watashangaa kwa yatakayoendelea, nawahasa wabunge hawa warudi, wapo kwenye mtihani mkubwa kwelikweli wa kuendelea kumtii huyo jamaa yao ama warudi tuendelee kwa taratibu zinazotakiwa,” alisema Ndugai.

Wakati Ndugai akisema hayo, Tundu Lissu naye ameandika kumjibu na hili hapa ni andiko lake ambalo limehaririwa kidogo bila kuondoa mantiki ya hoja yake;

“Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimemsikiliza Spika Ndugai akiweka msimamo wake kuhusu hatua yenu ya kuondoka Bungeni kwa muda. 

Spika Ndugai anastahili kujibiwa rasmi na hadharani, na napendekeza yafuatayo kuwa sehemu ya majibu yenu. 

1. Je, Wabunge wa Chadema ni watoro?

Kwa kadri ninavyofuatilia mijadala ya Bunge, ni Wabunge wa Chadema peke yenu ambao tangu mwanzo mmedai wabunge wote wapimwe ili kuona kama kuna yeyote mwenye maambukizi ya coronavirus. 

Nimemsikia KUB akisema hivyo mara kadhaa. Nimemsikia, Goddie Lema akisisitiza umuhimu wa Wabunge kupimwa, n.k.  

Maombi na madai yenu ya kupimwa yamepuuzwa na uongozi wa Bunge na wa Serikali na hadi sasa hakuna Mbunge hata mmoja aliyepimwa. 

Ushahidi wa hili ni kauli yake mwenyewe Spika Ndugai leo kwamba mkapimwe kwanza ndio mruhusiwe kurudi Bungeni. Maana yake ni kwamba anajua hamjapimwa. 

Wabunge wa Chadema  wamechukua hatua za kujilinda wao na wale walio karibu nao. Na wametangaza hivyo hadharani. Utoro wao unaanzia wapi? 

2. Kati ya Wabunge wa Chadema na (anamtaja kiongozi mmoja mkubwa ambaye hatuwezi kumtaja kwa sababu ya kiusalama) mtoro ni nani??? 

Kama, kwa kauli ya Spika Ndugai, Wabunge wa Chadema ni watoro, basi mtoro wa kwanza ni (anamtaja kiongozi huyo). 

Na kama Wabunge wa Chadema ni wezi kwa kuchukua posho za vikao na kuondoka Bungeni, basi mwizi wa kwanza ni  (anamtaja kiongozi huyo). 

Tangu janga la coronavirus lilipoanza kuwa kubwa hapa nchini, (kiongozi huyo) ametoroka na kujificha nyumbani kwake. 

(anataja eneo) sio makazi rasmi ya  kiongozi huyo. 

Kwa hiyo kama Wabunge wa Chadema ni watoro na wezi, (anamtaja kiongozi huyo) naye ni mtoro na mwizi. Hakuwezi kukawa na ubaguzi kwenye jambo hili. 

Na kama suala ni kurudisha pesa kwa sababu ya kutokuwepo Bungeni kwa sababu halali kama hii ya kujikinga na coronavirus, basi na Rais Magufuli naye arudishe pesa zote alizopokea au kupewa kwa kipindi chote ambacho ametorokea Chato. Nasisitiza hakuwezi kukawa na kauli mbili tofauti juu ya suala hili. 

3. Je, Wabunge wa Chadema ni wezi kweli? 

Mwizi ni yule anayechukua mali ya mwingine bila ridhaa yake na bila haki ya kufanya hivyo. Hii ndio tafsiri rahisi ya wizi kwa mujibu wa sheria zetu.

Je, Wabunge wa Chadema walichukua fedha bila ridhaa ya Bunge na hawakuwa na haki nazo??? 

Posho na mishahara ya Wabunge huingizwa kwenye akaunti zao na Bunge lenyewe bila hata Wabunge wenyewe kuziomba au kujua. 

Hawa wa Chadema wanakuwaje wezi kwa kuingiziwa posho kwenye akaunti zao na uongozi wa Bunge? 

Na je, sio halali kupewa posho za kujikimu??? Kuna posho za aina mbili zinazotolewa kwa Wabunge. Posho za kujikimu (per diem) na posho za vikao (sitting allowance). 

Kila Mbunge aliyeko Dodoma analipwa posho za kujikimu, hata kama haingii Bungeni. Kama Spika Ndugai anabishia hili aseme wazi wazi na hadharani. 

Posho za vikao zinalipwa kwa kuhudhuria Bungeni, na hulipwa baada, sio kabla, ya mahudhurio ya vikao. Kama Spika Ndugai anabishia hili aseme wazi wazi na hadharani pia. 

Wabunge wa Chadema  wamelipwa ‘per diem’ kwa sababu wako Dodoma kwa ajili ya vikao vya Bunge. Wangekuwa wamelazwa hospitalini bado wangelipwa per diem.

 Wako in isolation kujikinga na corona na kwa hiyo wanastahili kulipwa ‘per diem’. 

Sijamsikia Spika Ndugai akizungumzia malipo ya sitting allowance. Kama Wabunge wa CHADEMA wamelipwa sitting allowance na hawajahudhuria vikao vya Bunge basi aseme ili tuulize wamelipwaje kabla ya mahudhurio ya vikao? Hii ni kwa sababu hawapaswi kulipwa sitting allowance kama hawajahudhuria vikao vya Bunge.

4. Tabia ya Spika Ndugai kutaja taja hadharani malipo ya Wabunge wa upinzani wenye ugomvi naye au na Serikali 

Hii sio mara ya kwanza kwa Spika Ndugai kutaja mamilioni waliyolipwa Wabunge wa Chadema  wenye ugomvi naye au na Serikali ya Magufuli. Hatujawahi kuona kwa miaka yote ya kabla Rais Magufuli kuingia madarakani. 

Spika Ndugai hajawahi hata mara moja kutaja fedha anazolipwa yeye mwenyewe au Wabunge wa CCM. 

Je, ina maana ni Wabunge wa Chadema  peke yao ndio hulipwa mamilioni haya? 

Spika Ndugai mwenyewe amelipwa mabilioni mangapi kwa sababu hii au ile? Mbona hajawahi kuzungumzia mabilioni aliyolipwa kwa ajili ya matibabu yake India ambayo hata CAG aliyahoji kwenye taarifa yake ya mwaka jana? 

Spika Ndugai anataka watu wasiojua waamini kwamba Wabunge wa Chadema wamelipwa fedha hizo bila halali yoyote. Kama hiyo ni kweli, je, kwa nini Bunge linawalipa fedha hizo haramu?  

5. Spika Ndugai ametishia kuwachukulia hatua nyingine ambazo hajazitaja lakini amesema hiki ni kipindi cha mwisho cha Bunge. Kama hamjaelewa, hapa anamaanisha kwamba watazuia malipo ya kiinua mgongo cha Wabunge wa Chadema . 

Hii ni ‘blackmail’ ya moja kwa moja. Kiinua mgongo ni haki ya kisheria ya kila Mbunge aliyetumikia kipindi fulani cha Ubunge. Kiinua mgongo sio fadhila ya Spika Ndugai au ya Kuhani Mkuu kwa Wabunge wenye tabia njema kwao. Ni haki ya Wabunge wote. 

6. Ushauri wangu kwenu ni huu: 

a. Msirudi Bungeni hadi muda wa kujitenga kwa hiari wa siku 14 utakapoisha. Baada ya muda huo kwisha rudini Bungeni wakawazuie kuingia ili dunia nzima ifahamu. 

b. Msirudishe posho za kujikimu mlizolipwa kwa sababu mko kwenye eneo la kibunge Dodoma na mko nje ya Bunge kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya corona. Hivi ndivyo inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na WHO. 

Aidha, kulipa madeni ya Bunge sio, na haijawahi kuwa,  sharti la Mbunge kuruhusiwa kuingia bungeni. Kama wanafikiri wanawadai basi wawakate kwenye mishahara, lakini sio kuwazuia kuingia Bungeni. 

c. Kuhusu kutishiwa kuripotiwa polisi, hii haitakuwa ajabu kwa katika zama hizi. 

Kumbukeni tu kwamba hamjafanya kosa lolote lile la jinai kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. 

Kama Jeshi la Polisi litawakamata, haitakuwa ni kwa sababu ya kufanya kosa lolote lile. 

d. Kuhusu kupimwa corona Muulizeni Spika Ndugai au Waziri wa Afya awaelekeze mahali palipotengwa kwa ajili ya kupimia corona. 

Na sisitizeni hadharani kwamba kila Mbunge na mtumishi wa Bunge akapimwe kama utaratibu wa WHO unavyosema. 

Sio Wabunge wa CHADEMA peke yao wanaopaswa kupimwa; ni Wabunge wote. 

Je Ndugai na Chadema nani yuko sahihi katika hili? mjadala bado ni mrefu mitandaoni, wiki ijayo tutachapisha kwa ufupi maoni ya watu mbalimbali juu wenye mtazamo tofauti katika hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles