26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai atoa neno msamaha wa kina Nape

ANDREW MSECHU – DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amepongeza hatua ya wabunge watatu waliojitokeza kumwomba msamaha Rais Dk. John Magufuli, akisema ni hatua ya kijasiri inayostahili kuigwa na wabunge wengine.

Akizungumza bungeni jana mara baada ya kipindi cha kutambulisha wageni, Spika Ndugai alisema kwa binadamu wa kawaida kuomba radhi si jambo rahisi hivyo wabunge hao wamefanya jambo jema.

“Kama kiongozi wa Bunge, ninawapa pongezi kwa niaba ya wabunge wengine, igeni mfano huo hata kwa watu ambao ni wadogo na chini zaidi katika jamii yetu. Japokuwa mmetenda jambo ambalo mliona kabisa mlikosea, kiubinadamu basi lazima muombe radhi,” alisema.

Spika Ndugai pia alimpongeza Rais Magufuli kwa ustahimilivu na kuwasamehe wabunge hao watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nachukua nafasi hii pia kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwasamehe wabunge wetu hawa, hii ni hatua ya kuanza upya, kwa hiyo niseme tu kwamba huu ni mfano mzuri na wa kuigwa na vijana wengine,” alisema.

Wabunge waliosamehewa ni William Ngeleja (Sengerema), January Makamba (Bumbuli) na Nape Nnauye (Mtama).

Waliomba radhi kwa Rais baada ya kusambaa sauti zao zilizokuwa na mawasiliano yaliyodaiwa kumdhalilisha.

Ndugai alisema yapo magazeti mengine yaliyowachora baadhi ya wabunge hao na kuweka picha za ajabu ajabu, akisema inaonekana yanafurahia kuona watu wanalumbana ili wao waweze kuuza magazeti na mitandao.

Aliongeza kuwa wabunge hao wamefanya jambo la uungwana, hivyo aliwapongeza na kuwatia moyo na kuwataka wengine kuiga.

NGELEJA AZUNGUMZIA MSAMAHA

Kwa upande wake, Ngeleja, alizungumza kwa mara ya kwanza akielezea hatua ya msamaha alioupata kutoka kwa Rais Magufuli.

Ngeleja alisema kwa kawaida kibinadamu msamaha siku zote huleta faraja, kwa hiyo naye kwa sasa anajisikia kuwa mtu mwenye faraja.

 “Kwa hiyo, mimi kwa niaba ya wananchi wa Sengerema, napenda kumshukuru Rais na pia kutumia nafasi hii kuelezea faraja niliyonayo kwa kupata msamaha huo. Pia, nashukuru kwa namna Spika  alivyoliweka suala hili hapa,” alisema.

SERUKAMBA AOMBA RADHI

Wakati huohuo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) ameomba radhi kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni Juni, mwaka huu.

Alisema wakati akihitimisha hoja yake alitumia neno “Ujamaa” katika muktadha ambao baadaye ulisababisha taharuki iliyotokana na tafsiri ambayo alimaanisha.

”Mheshimiwa Spika, sentensi ya mwisho katika hoja ilikuwa ni maneno yafuatayo ‘kama kuna jambo siliamini ni ujamaa’,” alisema.

Alifafanua kuwa msingi wa hoja yake haikuwa kupinga ujamaa kwa itikadi ya kisiasa kujenga uchumi wa kitaifa na badala yake ililenga kuchochea mjadala wa kujenga uchumi wa kijamaa ili kuwa uchumi binafsi na juhudi za mchango wa sekta binafsi katika kukwamua kilimo.

”Mheshimiwa Spika, mimi ni zao la Chama Cha Mapinduzi ambacho kinaamini katika dhana ya ujamaa na kujitegemea, na hivyo haiwezekani mimi nikakariwa kwa makosa na hata kutafsiriwa ninaukana msingi wa kuwapo kwangu bungeni na ndani ya CCM.

”Mimi ni jamaa yako na takwa hilo ni kwa ajili ya masilahi mapana, napenda tena kukiomba radhi chama changu, viongozi wote wa CCM kwa ujumla kwa usumbufu uliotokana na matamshi yangu ambayo yalitafsiriwa katika muktadha usio sahihi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles