Ndugai akerwa ufukuzwaji wabunge

0
661

ndugaiNa MWANDISHI WETU

– DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amevishauri vyama vya siasa vya upinzani, visiwe na utaratibu wa kuwafukuza wabunge wao pindi wanapokosea.

Ili viweze kutimiza malengo hayo, Spika Ndugai alivishauri vyama hivyo kuiga wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho alisema hakina utaratibu wa kufukuza wabunge wake.

Spika Ndugai alitoa ushauri huo bungeni jana muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika.

“Waheshimiwa wabunge, napenda kuvishauri baadhi ya vyama vya upinzani kwani vina utaratibu fulani ambao huwa haunipendezi.

“Kumfukuza mbunge, tena wa jimbo si jambo jema kwa sababu kumpata mbunge wa aina hiyo ni gharama kubwa.

“Naviomba vyama hivyo viwe na utaratibu wa kuvumiliana na nawashauri wakiige Chama Cha Mapinduzi ambacho kina utaratibu wa kuwavumilia wabunge wake.

“Siyo kwamba wabunge wa CCM hawafanyi makosa, hao nao wanafanya makosa, lakini wanavumiliana tu,” alishauri Spika.

Hata hivyo, baada ya Spika kutoa ushauri huo, Mbunge wa Tandahimba, Ahmed Katani (CUF), aliomba mwongozo akitaka kupinga ushauri huo, lakini kabla hajamalizia kauli yake, Spika alimkatisha na kusema kauli yake haiwezi kuhojiwa kwa kuwa yeye ndiye kiongozi wa Bunge.

Ingawa Spika hakutaja jina la chama kilichowafukuza wabunge, kauli yake ilionekana kukigusa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho hivi karibuni kimewasimamisha uanachama wabunge wake wawili.

Wabunge hao waliosimamishwa uanachama pamoja na wanachama wengine 10 ni Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya na Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma.

Wabunge hao walisimamishwa uanachama wao, baada ya kudaiwa kuwa chanzo cha vurugu zilizosababisha kuvunjika kwa Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here