25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai: Afya yangu kwa sasa imeimarika

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amesema kwa sasa ana nafuu kubwa kiafya na anaweza kufanya kazi nyingi, huku akiwaomba Watanzania waendelee kumwombea.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Rais Dk. John Magufuli, aliyemtembelea nyumbani kwake kumjulia hali.

“Lakini niwahakikishie Watanzania, kwamba kwa sasa nina nafuu kubwa sana, naweza kufanya kazi nyingi tu sasa, lakini tuendelee kuombeana.

“Kwa kweli nimefarijika sana, kwanza naomba nimshukuru sana mheshimiwa Rais kwa sababu nilipopata matatizo haya ya maradhi alikuwa karibu sana na mimi nikiwa hapa nchini na hata nilipopelekwa nchini India alinipigia simu mara kwa mara na kunifariji sana na hapa amekuja kuniona kwa niaba ya Watanzania kwa kweli namshukuru sana na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa moyo huu,” alisema Spika Ndugai.

Pamoja na kumjulia hali Rais Magufuli aliyeandamana na mkewe Janeth Magufuli, wamemwombea Spika Ndugai kwa Mwenyezi Mungu apone na kupata nguvu haraka ili waweze kuendelea na majukumu yake ya kawaida katika ujenzi wa Taifa.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa nchi alimtembelea Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela ambaye pia alimwombea kwa Mwenyezi Mungu ili apone haraka.

Akizungumzia hali yake, Malecela alimshukuru Rais Magufuli na mkewe Janeth kwa kumtembelea ambapo alieleza afya yake inazidi kuimarika huku akiwashukuru madaktari wanaompatia matibabu.

“Mheshimiwa Rais nakushukuru sana, namshukuru pia Mama Janeth kwa kunitembelea na kunifariji, naendelea vizuri na matibabu na afya yangu imeimarika kwa kiasi kikubwa,” alisema Malecela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles