NDOTO ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayecheza katika klabu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta ya kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya, huenda ikayeyuka baada ya mabosi wake kuonyesha nia ya kuboresha mkataba wake.
Samatta alijiunga na Mazembe mwaka 2011 akitokea klabu ya Simba ya Dar es Salaam, kwa mkataba wa miaka mitano unaomalizika Mei, 2016.
Kwa hivi sasa Samatta amekuwa tegemeo katika kikosi cha Mazembe, akiwa ni kati ya wachezaji wanaowania ufungaji bora katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, huku akishika nafasi ya pili katika mbio hizo baada ya kufunga mabao sita nyuma ya Bakri Al Madina wa El Merreikh ya Sudan mwenye mabao saba, ambaye tayari timu yake imetolewa kwenye michuano hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Samatta alisema kuwa mkataba wake unamalizika mwakani, lakini tayari viongozi wake, akiwemo bosi wa Mazembe, Moise Katumbi wameonyesha nia ya kumuongezea mkataba mwingine kwa kuuboresha zaidi.
Alisema bado hajaanza mazungumzo nao, lakini bosi wake alimuita na kumuuliza juu ya kiasi anachokitaka kwa ajili ya mkataba mpya na kumuahidi kukaa mezani mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambayo Mazembe imefika hatua ya fainali.
“Kwa sasa siwezi kusema kiasi gani nimemwambia waniwekee mezani ili kuendelea nao kwa kuwa mazungumzo rasmi hayajaanza, ila sitosita kusaini iwapo watatimiza ninayotaka.
“Nimeishi vizuri na Mazembe na wao ndio walioniwezesha kuwa Samatta wa sasa, haitakuwa vizuri kama wakitimiza mahitaji yangu yote katika mkataba wangu mpya halafu nikatae kuendelea nao, ila yote yatajulikana baada ya kumalizika kwa mechi yetu ya fainali,” alisema Samatta.
Mazembe inataraji kukutana na USM Alger ya Algeria katika fainali ya michuano hiyo, mchezo wa kwanza utafanyika kati ya Oktoba 30 na Novemba Mosi, huku marudiano ukifanyika Novemba 6 na 8, mwaka huu.
Samatta kwa sasa yupo na Taifa Stars nchini Malawi ambapo timu hiyo itacheza mechi ya marudiano na wenyeji wao kesho kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia 2018.
Januari mwaka huu, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania, alifanya majaribio katika klabu ya CSKA Moscow ya Urusi nao kuonyesha nia ya kumsajili katika dirisha dogo la usajili, lakini hata hivyo hakufanikiwa na kurejea katika klabu yake ya TP Mazembe.
Samatta alifanya majaribio hayo katika kikosi hicho kilichoweka kambi nchini Hispania.
Samatta alijiunga na TP Mazembe akitokea Simba mwaka 2011 katika klabu hiyo.