26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

NDONDO CUP IMERUDISHA HESHIMA YA SOKA LA MTAANI

Na Mohamed Mharizo

SOKA ni mchezo unaopendwa duniani na wenye mashabiki wengi kuliko mwingine, tena hukusanya wadhamini wengi ambao huufanya mchezo huo kuwa na mvuto wa kipekee zaidi.

Katika kila nchi mashabiki wa soka hupenda kufuatilia ligi kuu za nchi zao na hata ligi kubwa barani Ulaya kama vile Ligi Kuu England (EPL), Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), Ligi Kuu ya Italia (Seria A), Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na nyinginezo.

Lakini misimu ya ligi zote zinapomalizika, mashabiki wa soka hukosa burudani ya kuburudisha nafsi zao kutokana na mahaba yao katika mchezo huo pamoja na kukosa kuona ligi hizo, hupata fursa ya kusikia taarifa za usajili za timu zao wanazozipenda.

Kila shabiki wa timu fulani hupenda kusikia taarifa nzuri ya timu yake kusajili wachezaji bora na wenye kiwango cha juu, hakuna shabiki anayependa kuona usajili wa kuungaunga katika timu yake.

Hata Tanzania mambo huwa ni hekaheka msimu wa usajili, wakati huo ligi zimeisha na kila timu inajiandaa na usajili, hapa huwa hakuna ligi na wachezaji hupewa likizo kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi.

Kwa sasa baada ya ligi kumalizika, Jiji la Dar es Salaam limekuwa na mzuka na shamrashamra za michuano ya Ndondo Cup.

Kwa mara ya kwanza mashindano hayo yalizinduliwa rasmi mwaka 2014 na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani, mashindano hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza chini ya udhamini wake Dk. Mwaka, kutoka Kituo cha Foreplan Kliniki.

Hatua ya mafanikio ya ndondo ilianza kama masihara na sasa hivi imeshika kasi, mashabiki wa soka mara Ligi Kuu inapomalizika husubiri kwa hamu kushuhudia Ndondo Cup, ambayo soka la ushindani huonekana kwa wachezaji wasio na majina kuonyesha uwezo wao na hata wengine hupata fursa ya kusajiliwa na timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa hakika hamasa imekuwa kubwa katika mashindano haya ya Ndondo Cup, yaani kwa lugha nyingine unaweza kusema heshima ya soka la mtaani imerudi tena, Ndondo Cup ndio mpango mzima, watu wameshtuka. Kila shabiki hujitokeza viwanjani hasa Kinesi kuona uhondo wa mashindano haya.

Kinesi umekuwa uwanja maarufu kwa sasa kutokana na kufanyika mashindano ya Ndondo Cup, hapo utapata burudani ya soka la kisasa kutoka kwa wachezaji wa timu mbalimbali, ngoma za ushangiliaji na hata visa na matukio ya kufurahisha.

Tumeshuhudia msimu wa kwanza wa mashindano hayo mwaka 2014, timu ya Abajalo ikitwaa ubingwa, msimu wa pili mwaka 2015 Faru Jeuri walitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga Kauzu FC huku msimu wa tatu mwaka 2016 ubingwa ulichukuliwa na Temeke Market baada ya kuifunga Kauzu FC mabao 3-1 katika Uwanja wa Bandari, maarufu kama Wembley.

Kwa msimu huu Ndondo Cup imekuwa na msisimko zaidi asikwambie mtu, mashindano haya yana raha yake.

Nusu fainali ya Ndondo Cup itachezwa Agosti 9 mwaka huu kwa Misosi FC kucheza na Keko Furniture huku Goms United ikiumana na Kibada One, katika Uwanja wa Kinesi.

Kwa msimu huu fainali ya mashindano haya yatafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Agosti 13.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles