23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

NDOA YENYE UHAI NI ILE ISIYOTAWALIWA NA USIRI


Na CHRISTIAN BWAYA

HUWA unajisikiaje unapogundua kuwa mtu wako wa karibu, labda rafiki unayemheshimu, anaujua udhaifu wako usiopenda ufahamike?

Mfano kuna tabia yako fulani ambayo huipendi. Sasa mara mtu wako wa karibu unayemheshimu anaigundua. Je, utachukia kwa kuhisi kudhalilika na pengine kujilinda kwa kumchukia au unachukua hatua za kujirekebisha?

Vipi unapogundua mtu wako wa karibu, uliyefikiri ni mtu wa viwango fulani, anakuwa na tabia zinazokera? Utamdharau na kumhukumu au utamvumilia kwa kumchukulia kama binadamu mwenye upungufu kama ulivyo wewe? 

Nafasi ya ukaribu katika ndoa

Fikiria watu wawili waliooana lakini wanaishi kwa mipaka. Ingawa wanapendana kwa dhati, lakini hakuna mwenye ujasiri wa kumruhusu mwenzake kufahamu maisha yake binafsi. Wapenzi hawa wanaishi na siri nyingi mioyoni mwao kwa kisingizio cha kulinda penzi lao.

Kwa upande mwingine, fikiria wapenzi wengine wasio na chochote cha kuficha kati yao, kila kitu kinawahusu wote bila mipaka, hawana kitu cha kuficha kwa sababu hawana hofu ya kuumbuka.

Kwa baadhi ya watu, usiri na kutokufahamika ndiyo nyenzo muhimu katika kulinda mapenzi. Wanafikiri kujificha, kuwanyima wapenzi wao haki ya kujua mambo yao binafsi, kutawafanya wawe na furaha. Erik Erikson, aliita hali hii upweke. Mtu mpweke anaweza kuwa amezungukwa na marafiki lakini hapati joto la kuwa karibu na mtu mwingine. Sababu moja wapo ni kutokuwa tayari kuwafungulia milango watu wengine (hasa mpenzi wake) kufahamu maisha yake ya faragha. Hakuna ndoa yenye uhai inayoweza kuzaliwa katika mazingira ya namna hii.

Ndoa yenye uhai ni uhusiano wa karibu zaidi kati ya watu wawili. Mwenza wako anapaswa kuwa mtu anayekufahamu kwa undani kuliko mwingine yeyote uliyewahi kufahamiana naye. Katika ndoa hai, mke/mume ndiye huwa mwenye idhini ya kuyaingilia maisha yako kuliko mtu mwingine yeyote.

Ingawa ni vigumu kufikia kiwango cha juu kabisa cha utayari huo wa kufahamika, bado ni muhimu kuweka mazingira mazuri ya kuondoa viambaza vya usiri kati yenu. Vinginevyo, uwezekano wa kuwa mpweke ilhali unaishi kwenye ndoa, unakuwa mkubwa. Huu mara nyingi huwa ndio mlango wa michepuko na tabia nyingine za hovyo katika ndoa. 

Kikwazo cha ukaribu

Watu wengi hawawezi kuwa karibu na wapenzi wao kwa sababu kubwa mbili. Kwanza, ni kutokujikubali. Mtu asiyejikubali anapojitazama ndani yake mara nyingi hujisikia kupungukiwa na kitu fulani anachotamani kuwa nacho. Inawezekana ni sifa fulani anayoiona kwa watu lakini yeye mwenyewe hana. Kukosa sifa hiyo, kunamfanya anapojitazama maisha yake, asipende kile anachokiona ndani yake.

Hali hii ya kutokuridhika na vile alivyo, humfanya ajihami kwa kujenga umbali na watu. Hapendi kufahamika kwa hofu ya upungufu alionao, akiamini utahatarisha hadhi anayofikiri anayo. Kwa Kiingereza neno sahihi hapa ni ‘insecure’ –hali ya mtu kujisikia hana hadhi ya kutosha.

Mtu wa namna hii anapoingia katika ndoa hatapenda kuwa wazi kwa mwenzake kwa sababu hajisikii kuwa salama akisema mambo yake. Si watu wengi huvumilia mtu msiri. Pia, huwa na wivu usio na kichwa wala miguu. Wivu, kwa kawaida ni kiashiria cha mtu kukosa kujiamini, akifikiri kuna mshindani (wa kufikirika) anayetishia penzi lake.

Kikwazo kinachowazuia watu kuwa karibu na wapenzi wao ni wao wenyewe kutojipenda. Huwezi kumpenda mtu mwingine kama ndani yako mwenyewe huna upendo. Mtu aliyepungukiwa upendo, hana nguvu ya kumpenda mtu mwingine.

Mtu wa namna hii, mwenye upungufu wa upendo, hutumia muda mwingi kutafuta upendo badala ya kuutoa. Hata pale anapopenda, kimsingi anatamani tu mtu mwingine ajaze ombwe analojisikia ndani yake. Ni tofauti kabisa na mtu anayependa kwa sababu ndani yake kunabubujika upendo kwa ajili ya watu wengine.

Mtu anayejipenda, aliyejaa upendo, hana ubinafsi ndani yake. Hakai tu akitarajia mpenzi wake afanye jitihada za kumpenda. Ndani yake huwa na msukumo wa kumfanya zaidi mwenzake kuliko kufanyiwa. Aidha, ni vigumu kwake kuwa na wivu kwa sababu nafsi yake inajisikia kuwa salama.

 Ushauri

Jikague kabla hujaingia katika ndoa. Hakikisha kwa kiwango fulani una uwezo wa kumruhusu mpenzi wako kufahamu mambo yako. Hakikisha unao upendo wa kukutosha kumgawia mwenzako. Kama bado unajisikia upweke ndani yako, usiingie kwenye ndoa ukitafuta faraja. Ukifanya hivyo, utakuwa mzigo utakaokuwa chanzo cha ghasia kwenye ndoa.

ITAENDELEA

Christian Bwaya ni mhadhiri wa Saikolojia na Unasihi, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , Simu: 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles