Na JOSEPH SHALUWA,
KOMEDIANI bei mbaya Bongo, Emmanuel Mgaya amefunga ndoa na mtoto mrembo aitwaye Monica na kusababisha gumzo nchi nzima kutokana na mambo mbalimbali ya kushangaza yaliyotokea kabla, wakati na baada ya ndoa hiyo kufungwa.
Ndoa hiyo ilifungwa wikiendi iliyopita katika Kanisa la Mito ya Baraka lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo Mchungaji Bruno Mwakiborwa alihudumu katika ibada hiyo.
Kutokana na ustaa wa Masanja na ubunifu wake katika kunogesha shughuli hiyo, kulisababisha kuibuka kwa gumzo kubwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kutokana na mambo yaliyojitokeza.
ULINZI
Siku ya harusi hiyo, muda wote ambao shughuli ilikuwa ikifanyika, eneo lote la kanisa lilizungukwa na walinzi kutoka katika Kampuni ya OK Security inayomilikiwa na msanii huyo.
Maaskari hao walitanda kina kona wakihakikisha usalama, huku wengine wakiwa na silaha za moto jambo lililozidisha urasmi wa harusi hiyo.
MAHARUSI KUHUBIRI
Ndani ya ibada, baada ya Masanja na Monica kuunganishwa kuwa mwili mmoja katika ndoa takatifu, walipewa nafasi ya kuhubiri na wawili hao walifanya hivyo kwa ustadi wa hali ya juu.
Masanja pamoja na kuhubiri vizuri, alichagiza kwa kuwavunja watu mbavu kwa kuchanganya na komedi zilizonogesha mahubiri yake na kuwafanya watu wamfuatilie muda wote aliokuwa akihubiri.
AWACHARAZA MABACHELA
Nje ya kanisa, mara baada ya ibada ya ndoa kuisha Masanja alionekana kuwaita vijana na kuwauliza kama wameoa, ambao waliosema hawajaoa aliwacharaza bakora ingawa ilikuwa katika mtindo wa kuigiza.
Wa kwanza kuonja bakora za Masanja alikuwa ni mchekeshaji maarufu nchini Mc Pilipili, kabla ya kugeukia kwa wapita njia na kuendelea na zoezi hilo lililowaacha watu hoi.
AWAVUNJA MBAVU VIGOGO
Katika hafla ya harusi hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Primrose uliopo Mbezi jijini Dar es Salaam, Masanja aliwavunja mbavu wahudhuriaji wakiwemo viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali waliokuwepo ukumbini.
Wakati akiwatambulisha Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Dk. Tulia Ackson, mawaziri, wabunge na viongozi wengine, Masanja alitumia maneno ya kuwavunja mbavu na kuwafanya wacheke muda wote.
Mbali na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Dk. Charles Tizeba na wabunge Willium Ngeleja (Sengerema), Hussein Bashe (Nzega Mjini) .
Katika mwendelezo wa komedi, Masanja alisema: “Tuna listi ndefu sana ya waheshimiwa wabunge humu ndani, na kwakweli niseme kwa listi hii hiki ni kikao halali cha Bunge. Nakuomba mshehimiwa Naibu Spika uje huku mbele uendeshe kikao cha Bunge.”
Kauli hiyo ya Masanja ilizidisha vicheko ukumbi mzima.
ASAKWA NA POLISI
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ilitangaza kuwasaka wasanii wa Orijino Komedi akiwemo Masanja kwa kosa la kuvaa sare zinazoshabihiana na za polisi wakati wa harusi hiyo.
Taarifa ya msanii huyo na wenzake kusakwa ilitolewa mapema Jumanne ya wiki hii na Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba ambaye alisema jeshi hilo halitamvumilia yeyote atakayeonekana kuvaa nguo zinazoshabihiana na za polisi.
ARUSHA ROHO MITANDAONI
Masanja akiwa honeymoon na mkewe Monica aliposti picha za mapozi mbalimbali wakifurahia maisha yao mapya ya ndoa, ambapo wadau walikuwa wakitoa maoni yao kwa kuwapongeza.
Hata hivyo wapo waliowaponda kwa mavazi waliyovaa wakidai hayana heshima, lakini Masanja hakuwavumilia, akaamua kuwajibu kwa picha nyingine akisindikiza na maneno:
“Jamani wenzenu tuko beach siyo kanisani, sasa kama mnaendaga beach na masuti basi endeleeni kutuombea. Halafu kama unakwazika usiingie hapa kwenye page yangu, nenda kwenye page ya Facebook ya kanisani kwenu.
“Hapa ni mwendo huu tu, mnajifanya mnajua eeh? Na bado! Imagine siku ya pili tu, mpaka uzeeni si mtahama taifa!”