ROSARIO, ARGENTINA
STAA wa klabu ya Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, hatimaye amefunga ndoa na mama wa watoto wake, Antonella Roccuzzo, usiku wa kuamkia jana huku mastaa mbalimbali wa soka wakihudhuria.
Ndoa hiyo imefungwa katika Mji wa Rosario uliopo nchini Argentina, wawili hao wamekuwa kwenye uhusiano tangu wakiwa wadogo.
Kabla ya kufunga ndoa tayari walikuwa wamefanikiwa kupata watoto wawili ambao wanajulikana kwa jina la Thiago na mwingine akiitwa Mateo.
Messi alionekana kupendana na Antonella tangu akiwa na umri wa miaka mitano, wakati huo Antonella akiwa na umri wa miaka minne, hivyo wazazi wao walikuwa wanaishi kwenye nyumba zilizokaribiana huko mjini Rosaria.
Katika harusi hiyo, Messi aliwapa mwaliko wageni zaidi ya 250, ikiwa pamoja na wachezaji wenzake ambao aliwahi kucheza nao pamoja ndani ya klabu hiyo ya Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina.
Baadhi ya wachezaji hao ni pamoja na Xavi Hernandez, Carles Puyol, Cesc Fabregas na Samuel Eto’o.
Wakati huo wachezaji ambao anacheza nao kwa sasa kwenye kikosi hicho na walikuwepo kwenye sherehe hiyo ni pamoja na mshambuliaji mwenzake, Luis Suarez akiwa na mke wake, Jordi Alba, Neymar, Gerard Pique, Sergio Busquets pamoja na Javier Mascherano.
Wachezaji wengine ni wale ambao wapo pamoja katika kikosi cha timu ya Taifa ya Argentina, mshambuliaji wa pembeni wa klabu ya PSG, Angel Di Maria, mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero pamoja na Ezequiel Lavezzi.
Kiungo wa Al-Sadd ya nchini Qatar, Xavi ambaye amecheza katika klabu ya Barcelona kwa miaka 17, aliungana na mke wake Nuria Cunillera, Puyol alikuwa na mke wake, Vanessa Lorenzo pamoja na kiungo wa Chelsea, Fabregas alikuwa na mke wake Daniella Semaan.
Wageni wengi waalikwa walifikia kwenye hoteli ya nyota tano ambayo inajulikana kwa jina la Pullman, ikiwa na vyumba 188, huku kulala kwa siku kiasi cha chini ni pauni 100, ambazo ni zaidi ya Sh 287,610.
Messi ni mchezaji wa pekee duniani ambaye anaongoza kwa kutwaa tuzo za mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or, huku akiwa amechukua mara tano akifuatiwa na Cristiano Ronaldo ambaye amechukua mara nne.
Msimu huu ambao umemalizika, mchezaji huyo ameweza kuifungia timu yake mabao 54 katika michezo 52 aliyocheza. Wiki moja iliyopita alisherehekea siku yake ya kuzaliwa na kufikisha miaka 30.