25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

NDIVYO BUNGE LINAVYOTAKIWA KWA MUJIBU WA KATIBA

BUNGE  la  Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania hatimaye limeshtuka kwa kuona kuwa linadharaulika.. Bunge limesimama na kutenda kwa kauli moja  pale lilipohisi kudharauliwa na wateule wa Rais. Mmoja akiwasema kuwa wabunge kazi yao ni kusinzia tu na mwingine akiwaita ni wapuuzi.

Kauli ya Spika wa Bunge nayo imeonyesha kuwa Bunge si chombo cha kuchezewa kwani  wabunge wanayo heshima yao .Spika amesema kuwa mbunge akitakiwa na mtu inabidi Spika apewe taarifa. Vile vile  Mbunge Zitto Kabwe ametolea ufafanuzi kanuni ya 51 kanuni ndogo ya 51(1)-51(4) kuhusu  Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge akioanisha na  hali ya kukamatwa kwa wabunge pamoja na kuelezea  Bunge la Tanzania kama sehemu ya Jumuiya ya Madola hivyo kuzingatia taratibu za Jumuiya hiyo pamoja na uamuzi wa Spika waliopita katika Bunge la Tanzania.

Kuna gazeti lililoonesha kuwa kwa mara ya kwanza Bunge limeweka historia kwa kuwa na kauli moja katika  kutetea hoja iliyowekwa mbele na mbunge wa upinzani na ikaungwa mkono na wabunge wote bila kujali itikadi zao. Hapa walikubaliana kwa umoja wao  kuwaita wateule wawili wa Rais ili kuwahoji kutokana na matamshi waliyoyafanya dhidi ya Bunge.

Ukweli ni kuwa Bunge ndivyo linavyotakiwa kuwa na si vinginevyo.  Bunge ni chombo cha kikatiba ambacho kwa mujibu wa ibara ya 63(2)  ya Katiba ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.

Bunge kwa kiasi kikubwa limekuwa likijitahidi sana kufanya kazi ya kuisimamia Serikali na ndio maana tumekuwa tukiona Bunge likiunda tume kuchunguza utendaji wa Serikali na matokeo pia tumeyaona wakati wa Richmond, Escrow, Operesheni  Kimbunga  nakadhalika. Katika maeneo haya mara nyingi Bunge limefanya kazi yake kwa umoja wao bila kusimamia itikadi za vyama vyao.

Hata hivyo kuna wakati Bunge hili  halikuweza kusimama  kama Bunge na hii imekuwa ikileta shida pale hoja ya kitaifa inapoibuliwa na ikakosa kuungwa mkono na hasa ikitolewa na wabunge wa kambi ya upinzani. Mfano suala la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo hata mbunge alitolewa bungeni bila staha kutokana na hoja hiyo.

Kuhusu suala la kuwa wabunge wanastahili heshima na hawapaswi kudharauliwa  tumeona jinsi ambavyo humo ndani ya Bunge baadhi ya wabunge wanavyotendewa kwa mfano kuna wakati Mbunge alitolewa bungeni kwa kuburutwa na hata mbwa waliingia bungeni kuwatoa wabunge.  Mambo kama haya ndio nadhani huweza kuonesha kumbe wabunge wanaweza kutendewa vyovyote. Chombo kinachopata amri ya kuwaburura wabunge toka bungeni hakitaweza kuwapa heshima wabunge wakiwa nje ya Bunge hata wawapo katika majimbo yao.

Tumeona siku za hivi karibuni wabunge wakichukuliwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kusafirishwa tena usiku na kufikia vituo vya polisi. Hii iliwahi kutokea kwa Mbunge wa Bunda na mara kadhaa Mbunge wa Singida Mashariki na Mbunge wa Arusha Mjini.

Sikumbuki  kuliona Bunge likisimama kama Bunge na kukemea hali hii. Mbunge wa Singida Mashariki alipochukuliwa mara ya mwisho nje ya Bunge na kusafirishwa usiku usiku hadi Dar es Salaam, baadhi ya wabunge wa upinzani walijaribu kuhoji lakini majibu hayakuwaridhisha na hivyo wabunge wote ya kambi ya upinzani walisusia kikao.

Pamoja na wabunge pia kuna matukio mengi yanayotokea kwa jamii ambayo Bunge hupaswa kwa umoja wao kuyaulizia na ikibidi kuyakemea lakini  umoja huu tuliouona wakati fulani hivi karibuni hatuuoni. Mfano wapo walimu ambao wamefanyiwa vitendo ambavyo ni dharau kwao kama walimu, kama kutakiwa kusafisha darasa mbele ya wanafunzi.

Wapo watendaji  serikalini waliosimamishwa kazi kwa tuhuma tu na majina yao yakatajwa katika kadamnasi na ikasemekana watachunguzwa na ikibainika si kweli watarejeshwa wakati tayari wameshatajwa hadharani. Haya yaliyojitokeza ya dawa za kulevya mkoani  Dar es Salaam ni mwendelezo tu. Bunge kwa kazi lililopewa kikatiba lina wajibu huu wa kuishauri na kuisimamia Serikali na vyombo vyake.

Pale vyombo hivyo vinavyotenda ndivyo sivyo,  kwa niaba ya wananchi wa Tanzania Bunge linatakiwa kufanya kitu. Bunge lisiwe na sura mbili kwamba pale ambapo baadhi ya wabunge wanatendewa isivyofaa hata kama ni nje ya Bunge  wanakaa kimya na  wengine wakitendewa ndipo wazungumze, si sahihi. Bunge ni la wananchi macho yao yanatakiwa  kuwa kwa wananchi na wakiona wananchi wanafanyiwa isivyo stahili na mtendaji ni Serikali au chombo chake Bunge lina wajibu wa kukemea.

Bunge ni chombo cha heshima kubwa kwani ndicho husimama badala ya  wananchi wenyewe. Na wabunge wengi wamechaguliwa na wananchi na ni sauti ya wananchi. Na wanapokaa kama chombo nguvu yao ni kubwa sana. Pale Bunge litakapokamata nafasi yake kama chombo kwa umoja wao mambo mengi hapa nchini yatarekebishwa. Mifano mizuri ni kama pale Bunge liliposimamia kidete masuala ya ubadhirifu , uvunjifu wa haki za binadamu nakadhalika.

Bunge linapohoji pale linapoguswa lenyewe kama chombo na lisijali pale wabunge katika ubinafsi wao wanapodhalilishwa hapo kuna kasoro kwani Bunge ni wabunge hata mmoja tu anapodhalilishwa ni sawa na Bunge kudhalilishwa.  Vyombo vya Serikali vinatakiwa kujua kuwa lipo Bunge ambalo ni makini na hivyo  vyenyewe vifanye kazi yake kwa weledi.  Bunge lisiwe na vipimo vya kubadilika badilika.

Kwa sasa watu wengine wamedhani kuwa Bunge limechukua hatua hiyo kwa sababu tu limeguswa, lakini pia inaonekana kama vile kuna kujihami baada ya majina kuwa yanatajwa tajwa. Sitaki kuamini hivyo ila msisitizo ni kuwa Bunge  lisimamie weledi wake.Wabunge wawapo bungeni  wapatiwe heshima stahiki na wawapo nje ya Bunge heshima yao iambatane nao.

Bunge liendelee kuisimamia Serikali si kwa masuala yanaloligusa Bunge lenyewe moja kwa moja tu bali hata kwa masuala mengine yote yanayoonekana kwenda kinyume na utawala wa sheria na yanayoonekana kuvunja haki za binadamu.

Katiba imetoa mamlaka kwa Bunge ili kuhakikisha Serikali na watendaji wake kama vyombo vya Serikali vinapata ushauri pale vinapokuwa nje ya mstari , Bunge litimize wajibu wake si kama fungamano la chama cha siasa bali kama Bunge katika umoja wake. Inawezekana kama tulivyoshuhudia hivyo tunasubiri kuona mengi zaidi.

Imeandaliwa na Dk. Helen Kijo-Bisimba Mkurugenzi Mtendaji  LHRC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles