27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NDIDI ANAONDOKA GENK, SAMATTA ATAFUATA

Na MARKUS MPANGALA


mbwana-samattaNAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, yupo katika kona nzuri ya kuibuka mchezaji wa kipekee kutoka Tanzania kutamba barani Ulaya. Samatta anakipiga katika klabu ya Genk ya Ubelgiji, ambayo imewahi kuwatoa mastaa mbalimbali wanaokipiga kwenye vilabu tofauti katika ligi mashuhuri.

Miongoni mwao ni Christian Benteke, ambaye aliichezea Genk, kisha kwenda Aston Villa na baadaye kusajiliwa na Brendan Rodgers alipokuwa kocha wa Liverpool ya England. Nasema Samatta yupo katika eneo zuri la kutamba kisoka.

Kwanza Samata ameshatamba barani Afrika na kwamba tayari amekuwa na wasifu mzuri. Kwamba ametwaa Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa ndani barani Afrika.

Hilo lina maana Samatta hana anachodaiwa barani humu, ukiondoa Kombe la Mataifa ya Afrika ambayo hushirikisha timu za taifa. Kwenye ngazi ya klabu hana deni.

Pili, majuzi nilikuwa nasoma habari za kiungo mkabaji wa klabu ya Genk, Wilfred Ndidi. Kiungo huyo anafananishwa na yule wa Chelsea, Ng’olo Kante kiuchezaji. Ndidi anakwenda kujiunga na klabu ya Leicester City ya England.

Kwa maana hiyo, utaona wachezaji wa Genk wapo kwenye rada ya mawakala na wasaka vipaji wengi ambao wanatoa uhakika na matumaini makubwa kuwa ipo siku Samatta atakuwa bonge la mchezaji katika ligi kubwa za Ujerumani, Uingereza, Hispania, Ufaransa na Italia.

Wakati fulani Samatta aliwahi kuniambia kuwa, kiu yake ni kucheza Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga. Sababu kubwa aliyotoa ni ufundi mwingi unaotumika katika ligi hiyo, huku matumizi ya nguvu yakiwa ya kiwango cha chini.

Pengine hilo linaweza kutokea, lakini bado anayo nafasi ya kucheza katika ligi nyingine. Kuna klabu nyingi ambazo hutazama wachezaji kutoka maeneo tofauti na walipo kwa lengo la kupata vipaji vipya.

Wengi wamekuwa wakiizungumzia Leicester City kama klabu iliyopotea baada ya kumuuza kiungo wake, N’golo Kante. Lakini macho ya wasaka vipaji wa Leicester City yametua Genk. Yakamwibua Wilfred Ndidi. Nyota huyo anajiunga na Leicester Januari mwaka huu kwa ada ya pauni milioni 15 tu.

Kama macho ya Genk yalitua TP Mazembe, ni kwa vipi macho ya Leicester City yasitue kwa Samatta? Kama winga machachari, Ahmed Mussa kutoka Nigeria alitua klabuni hapo akitokea Ukraine, ni kwa vipi asimwambie kocha Claudio Raineri kuhusiana na chochote juu ya mwenendo wa Samatta kisoka.

Nakumbuka wakati fulani nilimsikia Arsene Wenger akiulizia uchezaji wa Junichiro Inamoto hata kwa haiba yake, kwa mwonekano anapokuwa na kundi la wageni, wachezaji au mkusanyiko wowote.

Lengo la Wenger lilikuwa kujua tabia ya Inamoto, jambo ambalo linaweza kufanywa pia kwa Samatta. Kwa utulivu na upole wa Samatta, pia anapata sifa kubwa kama kilivyo kipaji chake.

Haiwezekani kocha akataka kusajili mchezaji mwenye tabia za ukorofi kama Mario Balotelli au Joey Barton. Haiwezekani kocha akasajili mchezaji ambaye hakufuatiliwa ipasavyo.

Kwanza anafuatiliwa kiwango na ufundi wake, kipaji na namna anavyoweza kutumika tofauti na ilivyozoeleka. Kwamba kama kocha fulani amezoea kumtumia Antonio Valencia kuwa winga, basi mwingine atampanga beki mbili.

Kama kocha fulani alizoea kumpanga Fred Mbuna kama mshambuliaji wa kati, basi mwingine atakuja kumweka namba 2 au beki wa kati. Ni hivyo kwa Samatta, anaweza kucheza kiungo wa pembeni kulia na kushoto, pamoja na mshambuliaji wa kati na nyuma ya mshambuliaji.

Sifa zote hizo zinampa nafasi ya kipekee kufuatiliwa zaidi. Kwa macho na akili yangu nimemwona Wilfred Ndidi. Hafanani sana kiuchezaji na Kante, lakini naye ni mtu wa shughuli na ana tabia zote za kiungo mkabaji. Tofauti nyingine Ndidi ni mrefu na hana kasi kama Kante.

Tofauti zote hizo hazimnyimi nafasi ya kuonyesha umahiri wake. Na hivyo ndivyo Samatta anavyoweza kujikuta akiwa klabu nyingine kubwa mno. Nilipata fununu kuwa eti yule kocha wa zamani wa Genk, Peter Maes, ndiye alimkubali zaidi Samatta kuliko kocha anayekaimu sasa.

Lakini naamini kipaji cha Samatta kitaendelea kumkuna kocha yeyote ilimradi ampatie nafasi tu. Samatta anapiga Genk, anaelekea matawi ya juu. Hivyo naamini kama Ndidi anaondoka Genk basi Samatta naye atafuata msimu mmoja baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles