Na Mwandishi Wetu-Serengeti
WATU wa saba waliokuwa kwenye ndege moja aina ya Cessna Caravan yenye namba za usajili F 406 yenye uwezo wa kubeba abiria 12 mali ya Kampuni ya Air Excel.
Ndege hiyo ilikuwa inatoka katika Uwanja wa Sasakwa Singita Grumeti, karibu na hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wamenusurika kifo, baada ya ndege hiyo kuanguka na kuteketea kwa moto.
Tukio hilo lilitokea jana na kuthibitishwa na Meneja Uhusiano wa Singita Grumeti na Wadau wa Maendeleo Ami Hamidu Seki, alisema ajalihiyo ilitokea juzi saa tano asubuhi, baada ya ndege hiyo kuruka na kuanguka nje kidogo mwa uwanja huo.
Seki alisema wakati ndege hiyo ikiruka muda mfupi ilipata hitilafu na kuanguka katika eneo hilo, ambapo abria watano ambao wote ni watalii waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walinusurika kifo wakiwamo na marubani wawili wa ndege hiyo.
“Tayari wataalamu wa anga wako hapa wanafanya utaratibu ili kujua chanzo cha ajali ya ndege hiyo ila siwezi kujua chanzo chake ni nini,” alisema Seki
Alisema majeruhi wote wa ajali hiyo wamesafirishwa Nairobi nchini Kenya kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philip Kalangi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo alisema siku ya ajali hiyo ndege ilikuwa na abiria watano ambao ni familia ya baba, mama na watoto watatu ambao wote ni raia wa Marekani.
Aliwataja abiria waliokuwamo kuwa ni Greg Martin Perelman (60), Susan Perelman (52), Sara Milessa Perelman (23), Danielle Jaffe Perelman (21) na Emma Stephanie Perelman (19) ambao wote wamenusurika kwenye ajali hiyo.
Kwa upande wa marubani waliokuwa wakirusha ndege hiyo ni Mohammed Seleman akiwasaidiwa na Fahd Saleh ambao wote walikimbizwa Nairobi nchini Kenya kwa ajili ya matibabu.