Na Aziaza Masoud, DAR ES SALAAM
MARUBANI wawili wa kikosi cha jeshi la anga wamefariki baada ya ndege ya mafunzo ya Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) kupata hitilafu na kuanguka eneo la Silversands Msasani katika kisiwa cha Mbudya, Dar es Salaam.
Taarifa za kuanguka kwa ndege hiyo zilianza kusambaa kupitia mitandao ya jamii jana asubuhi zikieleza kuwa wavuvi walikuwa wa kwanza kutambua ajali hiyo baada ya kuona kofia ngumu.
Akizungumza na Mtanzania Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema tukio hilo lilitokea jana saa 3:30 asubuhi baada ya injini ya ndege hiyo ya mafunzo kupata hitilafu na kuanguka katika kisiwa hicho.
“Baada ya hitilafu walijaribu kuruka na vifaa vya usalama walivyokuwa navyo kwenye ndege, lakini walipofika chini kulikuwa na maji walipojaribu kuogelea wakazama,”alisema Kanali Lubinga.
Kanali Lubinga aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Luteni Kanali Karikisio Ndongolo ambaye alikuwa mkufunzi na Kapteni Gaudenci Hamisi aliyekuwa rubani, wote wa kikosi cha anga.
Alisema ndege hiyo ilikuwa haina jina wala namba kwa kuwa ilikuwa ya mafunzo.
Msemaji huyo wa jeshi alisema taratibu za kuitafuta miili hiyo zilikuwa zikiendelea mpaka jana ambako kikosi cha wana maji wakiwa na boti maalum na vifaa vingine kilikuwa katika eneo hilo.