23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ndege ya Ethiopian yaua watu 157

Na MWANDISHI WETU

-ADDIS ABABA, ETHIOPIA

NDEGE ya Kampuni ya Ndege ya Ethiopian Airlines, imeanguka na kuua watu wote waliokuwamo wakiwa abiria pamoja na wahudumu.

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Adis Ababa nchini Ethiopia kuelekea mjini Nairobi nchini Kenya.

Taarifa ya Kampuni ya Ndege ya Ethiopian Airlines kupitia Msemaji wake, Asrat Begashaw iliyotolewa jana, ilieleza ndege hiyo ilikuwa na abiria kutoka nchi 33 ambao walikuwa wakisafiri na ndege hiyo kupata ajali na wote wamekufa.

“Ndege ya Kampuni ya Ethiopia aina ya Boeing 737 iliyokuwa ikisafiri kutoka Adis Ababa kuelekea Nairobi, ilianguka jana asubuhi,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilisema awali ndege hiyo ilipoteza mawasiliano dakika sita baada ya kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Adis Ababa.

Ndege ilikuwa na abiria 149 na wahudumu wanane waliokuwemo, ambapo hakuna hata mmoja aliyeweza kunusurika na wote wamefariki dunia,” alisema Begashaw wakati akizungumza na Shirika la Habari la Kitaifa la Ethiopia. 

Kampuni hiyo inasema imeanzisha kituo cha kupata taarifa kuhusu familia na marafiki wa watu waliokuwamo ndani ya ndege hiyo.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abey Ahmed, imetoa taarifa ikitoa rambirambi kwa familia za waliowapoteza wapendwa wao katika ajali hiyo.

Kituo cha ufuatiliaji wa safari za ndege kwa saa 24 kimekuwa kikitoa taarifa kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhusu ajali ya ndege hiyo ya Ethiopian Airlines.

Kituo hicho kimesema: “Kasi ya ndege hiyo ya wima haikuwa thabiti baada ya kuondoka kwenye uwanja wa ndege.”

Ndege hiyo ambayo ilitarajiwa kufika Nairobi, iliondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa saa 8:38 asubuhi kwa saa za Ethiopia, lakini ikapoteza mawasiliano majira ya saa 8:44 asubuhi kwa saa za nchini hapa.

Kutokana na ajali hiyo, Kampuni ya Kenya Airways imetoa rambirambi kwa ajali hiyo kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kenya Airways, Sebastian Mikosz ambaye alitoa salamu hizo kupitia ukurasa wa Twitter kwa familia za waliopoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo.

Katika taarifa yake, alisema miongoni mwa waliopoteza maisha ni raia 32  wa Kenya, raia 18  wa  Canada, tisa wa nchi hii, nane kutoka nchini za  Italia, China, Marekani, raia saba kutoka nchi za Uingereza na Ufaransa.

Alisema abiria wengine waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni sita kutoka Misri, watano Uholanzi, wanne ni raia wa nchi za India na  Slovakia, watatu ni kutoka nchi za Austria, Swiden na Urusi na wawili ni  raia wa  Morocco, Poland na Israel.

Mikosz alisema  nchi nyingine ambazo zimepoteza raia mmoja ni Ubelgiji,  Indonesia, Somalia, Norway, Serbia, Togo, Msumbiji, Rwanda, Sudan, Uganda na  Yemen.

Alisema pia katika ajali hiyo, kuna abiria wanne waliokuwa wakitumia hati  za kusafiria za Umoja wa Mataifa, hivyo mataifa yao hayakuweza kufahamika kwa haraka.

Mkurugenzi mkuu huyo mtendaji alisema rubani aliyekuwa akiendesha ndege hiyo ni mwenye rekodi nzuri katika fani hiyo na hakuna tatizo la kiufundi ambalo lilibainika. 

Naye Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, pia ametoa salamu zake za rambirambi kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa watu waliopoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo.

Familia na marafiki wanasubiri taarifa mjini Nairobi kuhusu hatima ya wapendwa wao waliokuwa wamesafiri kwa ndege ya Ethiopia iliyopata ajali jana asubuhi.

Ndege hiyo ilitarajiwa kuwasili mjini Nairobi kwenye Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta saa 4:30 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki.

MTANZANIA ANUSURIKA

Kutokana na ajali hiyo, Mtanzania Antu Mandoza ambaye pia ni mjasiriamali wa urembo, alieleza namna alivyonusurika katika ajali hiyo.

Katika ukurasa wake wa Twitter, alisema alinusurika kukata tiketi katika ndege hiyo kabla ya kubadili safari ya Addis Ababa na baada ya kushuka, ndipo alipokutana na taarifa hizo mbaya huku akipokea ujumbe mwingi na simu kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki waliotaka kujua hali yake.

“I almost took the Ethiopian plane that crashed today, I changed the route to Addis, I’m just landing and seeing the news and so many calls from the few people who knew I’m traveling with Ethiopia worried. God is good. Ningekuwa marehemu saa hivi. Mungu mkubwa,” alisema Antu katika ukurasa wake wa Twitter akiwa anatokea nchini Ghana.

ABIRIA WALIOKUWAMO

Taarifa zinaeleza kwamba, ndege hiyo ilikuwa na abiria kutoka mataifa 33 kama zinavyosomeka nchi na idadi kwenye mabano, Kenya (32), Canada (18), Ethiopia (9), China (8), Italia (8), Marekani (8), Ufaransa (7), Uingereza (7), Misri (6), Ureno (5), Umoja wa Mataifa (4), India (4), Urusi (3), Hispania (2), Morroco (2), Poland (2), Israel (2), Ubelgiji (1), Uganda (1), Yemeni (1), Sudan (1).

Abiria wengine kutoka nchi za Togo (1), Msumbiji (1), Norway (1), Djibouti (1), Indonesian (1), Irish (1), Rwanda (1), Saudi Arabia (1), Sudan Kusini (1), Somalia (1), Nepal (1) na Nigeria (1).

BOEING 737 Max-8 ILIKUWA MPYA

Kampuni ya Boeing ambayo iliitengeneza ndege hiyo iliyoanguka, imesema kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba inafuatilia kwa karibu hali ya mambo.

Ndege ya 737 Max-8 ni mpya angani, ikiwa ilizinduliwa kwa mara ya kwanza 2016. Iliongezwa kwenye safari za ndege za Ethiopian Airlines Julai mwaka jana.

Ndege nyingine iliyotengenezwa kwa muundo wake ilianguka miezi mitano iliyopita, wakati safari ya ndege ya Lion Air ilipoangukia baharini karibu na Indonesia ikiwa imewabeba wasafiri 190.

Kampuni hiyo iliiambia BBC kuwa taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo zitatolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles