23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NDEGE BINAFSI YA KISASA ZAIDI DUNIANI

MAENDELEO ya sayansi na teknalojia yanaendelea kufanya maisha kuwa rahisi na kuvutia zaidi. Wenye vipato vikubwa pengine ndiyo wanaofurahia zaidi ugunduzi katika nyanja mbali mbali za maisha ya kila siku kutokana na ukweli kuwa mara nyingi bidhaa au huduma za kipekee huwa na gharama kubwa sana na kuwafanya wenye ukwasi wa kutosha kuzifurahia.

Katika kuonyesha kuwa teknalojia imekuwa na pesa ni kila kitu, kampuni kubwa ya kutengeneza ndege ya Boeing ya Marekani, imetengeneza ndege binafsi ya kifahari zaidi kuwahi kutengenezwa duniani.

Ndege hiyo aina ya Boeing 747-8 VIP inaelezwa kuwa ndiyo ndege ya kifahari zaidi duniani na muundo wake wa ndani ni kama hoteli ya kifahari. Unaposafiri na ndege hiyo ni kama vile hausafiri bali upo ndani ya hoteli ya kifahari yenye kupaa angani

Kampuni ya Boeing ilitengeneza ndege hiyo ya aina yake kwa oda maalumu na walichokifanya ni kusaidiana na washirika wake kubadilisha muundo wa ndani wa iliyokuwa ndege kubwa abiria aina ya Boeing 747-8 kuwa ndege binafsi ambayo iligharibu Dola za Marekani milioni 380 sawa na Sh bilioni 700 na milioni 266 za Tanzania.

Kwa kipindi kirefu Boeing walikuwa wakificha mmiliki wa ndege hiyo mpaka ulipofika wakati wa kuikadhi kwa mmiliki wake ambaye ni familia ya kifalme ya Qatar, nchi ambayo inashikilia namba moja kwa utajiri duniani.

Ndege aina ya Boeing 787-8 ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 450 ndiyo ambayo kampuni ya Greenpoint Technologies ya Marekani ilibadilisha muundo wake wa ndani na kutengeneza ndege binafsi  ambayo ni kama kasri kwa ndani kwa ajili ya matumizi binafsi ya familia ya Kifalme.

Greenpoint Technologies ni kampuni maarufu nchini Marekani kwa utengenezaji wa muonekanano wa ndani wa ndege binafsi pamoja na ndege za wakuu wa nchi kupitia kampuni ya Boeing

Utengenezaji wa ndege hiyo umekuwa ni gumzo kubwa na suala la nani alikuwa mmiliki wake ilikuwa ni siri kubwa. Ndege hiyo, inagharimu mara na tatu nusu ya ndege binafsi ya kifahari ya milionea na mfanyabiashara ambaye kwa sasa ni rais wa Marekani Donald Trump. Utengenezaji wa ndani ulifanyika Marekani na kumaliziwa nchini Ujerumani

Ndege hiyo kwa ndani ni kama upo kwenye jumba la kifahari. Kuna makabati ya kuwekea vitu mbali mbali, kuta zenye picha, silingi bodi. Pia ndege hiyo ina sebule kubwa na ya kifahari, sehemu ya kulia chakula (dining room), ofisi pamoja na vyumba vya kulala.

Ndege hiyo ya aina yake, inaelezewa kuwa ndiyo ya kwanza kutengenezwa kwa namna ya pekee huku mabilioni ya Dola yakitumika tangu wazo la kuwa na ndege ya kifahari zaidi duniani kuijia familia Kifalme.

Kabla ya kuanza kutengenezwa, mmiliki alikutana na wataalamu mbalimbali ambao walionekana wangekuwa na uwezo wa kutengeneza muonekano wa ndani. Baadhi ya makampuni hayo ni pamoja na BMW, Design works USA na Giugiaro Design kabla ya kuamua kuichagua kampuni ya Greenpoint Technologies kufanya kazi hiyo.

Marekani pamoja na kuwa na matajiri wakubwa kama kina Bill gates, Warren Buffet na wengineo, bado hakuna tajiri ambaye ameweza kuvunja rekodi kwa kuwa na ndege ya kifahari kama hiyo.

Pamoja na ukubwa wake, ndege hiyo inaelezewa kuwa ni ndege yenye mwendo kasi kuliko kawaida huku ikiwa na uwezo wa kubeba watu 100. Wataalamu wanasema, kwa kutumia ndege hiyo, mtu anaweza kuwa London nchini Uingereza jioni na kuondoka kwenda kufanya starehe kama kwenda Club katika jiji la New York nchini Marekani. Wakati wa kurudi, ndege hiyo haitahitaji kuongeza mafuta kwa ajili ya safari ndefu ya kuvuka bahari ya Atlantic kama ambavyo ndege nyingine zingehitaji

Uwezo wa kutua kwenye viwanja tofauti tofauti pamoja na kutumia vifaa vya kawaida sana vinavyosaidia ndege kutua ni kati ya sifa zinazofanya ndege hiyo kuwa ya kipekee.

Naam, familia ya kifalme ya nchi tajiri zaidi duniani ya Qatar ndiyo wamiliki wa ndege hii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles