Ndayiragije atamba Stars kuiliza Sudan

0
951

MWANDISHI WETU KHARTOUM

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo itakuwa na shughuli pevu ugenini mbele ya Sudan katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN), utakaopigwa kwenye Uwanja wa Omdurman, mjini Khartoum.

Stars itavaana na Sudan ikitoka kulazimisha suluhu ugenini dhidi ya Rwanda katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) uliochezwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.

Timu hiyo ilitumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya mechi  hiyo ya marudiano dhidi ya Sudan.

Stars itashuka dimbani kuikabili Sudan ikiwa na kumbukumbu ya kupokea kichapo cha bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa michuano hiyo uliochezwa Septemba 22, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo itahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 ili kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo itakayofanyika mwakani nchini Cameroon.

Stars imejikuta mikononi mwa Sudan baada ya kuitupa nje Kenya ‘Harambee Stars’ kwa penalti 4-1 baada ya michezo yote miwili ya nyumbani kumalizika kwa suluhu.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije kitakuwa na mtihani mzito wa kushinda mchezo huo ili kunasa tiketi ya kwenda Cameroon, ikiwa ni mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2009 katika fainali zilizofanyika nchini Ivory Coast.

Huo utakuwa mchezo wa sita kwa Ndayiragije kuiongoza Stars tangu arithi mikoba iliyaochwa na mtangulizi wake, Mnigeria, Emmanuel Amunike.

Rekodi zinaonyesha Stars imeshakutana na Sudan mara 24 katika mashindano mbalimbali,  ikishinda michezo minne, sare nane na kupoteza 12.

Akizungumzia mchezo huo, Ndayiragije alisema kikosi hicho kiko tayari kwa mapambano ya kusaka ushindi utakaowawezesha kuibwaga Sudan kwao na kutinga hatua ya makundi.

Alisema wachezaji wanaonekana kuwa morali ya hali ya juu katika mazoezi tangu walipofika Sudan, huku mipango yao ikiwa ni ‘kupindua meza’ ugenini.

 “Kila kitu kipo sawa kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Sudan, tunafahamu umuhimu wa mchezo huu ndiyo maana tumeweka msisitizo wa hali juu ili kile tulichopanga kiweze kutimia, tunajua kazi haitakuwa rahisi kupata matokeo hapa, lakini kwa uwezo wa Mungu na maandalizi tuliyofanya, tutashida.

“Tulikuwa na mchezo mzuri wa kirafiki dhidi ya Rwanda Jumatatu, mechi ile ili kipimo sahihi kwetu na imetusaidia kujijenga kimbinu kabla ya kuivaa Sudan, tuko tayari kujitolea kwa kadri ya uwezo wetu ili kuhakikisha tunawapa Watanzania kile wanachokitaka, tunaomba watuombee ili tuweze kutimiza lengo hili la kitaifa,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here