27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘NDAMA’ AHUKUMIWA MIAKA MITANO JELA

Na MANENO SELANYIKA

-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara maarufu, Shabani Hussein (44), maarufu kwa jina la ‘Ndama mtoto ya Ng'ombe’, kulipa faini ya Sh milioni 200 au kifungo cha miaka mitano jela, baada ya kukiri shtaka la sita la kutakatisha fedha dola za Marekani 540,000.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Victoria Nongwa, baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Christopher Msigwa, kumsomea maelezo ya awali (PH) ya mashtaka yake ambapo alikiri.

Hakimu Nongwa alisema mahakama imezingatia hoja za pande zote mbili, ambapo upande wa mashtaka uliomba mahakama kwa mujibu wa sheria ya kutakatisha fedha kifungu cha 13 (a) cha Sheria ya kuzuia utakatishaji fedha, kumpa adhabu kali mshtakiwa, kwa kuwa makosa hayo yanalenga kudidimiza uchumi wa nchi.

"Katika sheria hii mshitakiwa anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka isiyopungua mitano ama isiyozidi 10 ama kulipa faini isiyopungua Sh milioni 100 ama isiyozidi Sh milioni 500. Lakini ni haki ya mahakama kuzingatia faini au kifungo pale mshtakiwa anapokuwa na makosa ya kujirudia rudia," alisema Hakimu Nongwa.

Alisema serikali inasisitiza kulipwa faini badala ya kifungo, lakini mshtakiwa anastahili faini kwa kuwa ameipunguzia gharama mahakama kuhusu shughuli za uendeshaji, ikiwamo gharama za kuleta mashahidi katika mashtaka hayo na kwamba familia yake imekosa huduma kwa kipindi cha mwaka mmoja alipokuwa gerezani.

"Sheria hii ipo kwa ajili ya kuonesha kuwa makosa hayo hayatakiwi kumnufaisha mkosaji, hivyo utatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 200 na usipolipa tutaandika hati ya kifungo cha miaka mitano jela," alisisitiza.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili Msigwa alidai hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa na ni rai ya Jamhuri kwamba mahakama imuadhibu mshtakiwa kuzingatia sheria ya kuzuia utakatishaji fedha yenye lengo la kuzuia makosa yenye kudidimiza uchumi wa nchi na uzito wa makosa hayo.

Wakili wa utetezi, Wabeya Kung’e, aliomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, pia mshtakiwa hakuonesha usumbufu na kwamba kukiri kosa ni ishara ya kusikitishwa pamoja na kutegemewa na familia yake.

Katika shitaka la sita, Ndama anadaiwa kuwa kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic, alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo zimepatikana kwa njia ya udanganyifu.

Awali, Wakili Msigwa akisoma maelezo ya mshitakiwa, alidai Ndama ni mkazi wa Mbezi Beach na kwamba Mei 14, 2013, Bushoboka Mutamola na Majibu Taratibu walisajili Brela Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Co. Limited na kupata hati ya usajili namba 992449 kwa ajili ya kujishughulisha na biashara ya madini.

Alidai Septemba 16, 2013, kampuni hiyo ilifungua akaunti ya fedha za kigeni Benki ya Stanbic tawi la Viwanda na kupewa akaunti 9120000085152.

Msigwa alidai katika ufunguzi wa akaunti hiyo, Ndama alijitambulisha kuwa Mwenyekiti wa kampuni hiyo na ndiye mtiaji saini pekee kwenye benki hiyo, ambapo aliwasilisha nyaraka mbalimbali, ikiwamo barua ya utambulisho wa Kampuni, leseni ya biashara, namba ya utambulisho wa biashara (TIN) ambazo zilipokelewa mahakamani hapo.

Licha ya kukubali mashitaka hayo, Ndama alikana makosa mengine, yakiwamo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Wakili Msigwa alidai upelelezi wa mashitaka hayo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, Hakimu Nongwa alisema mashitaka mengine yaliyobaki yana dhamana, atatakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini kulipa fedha taslimu zaidi ya Sh milioni 540,390 au hati isiyohamishika yenye kiasi hicho.

Aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 16 mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles